Showing posts with label michezo. Show all posts
Showing posts with label michezo. Show all posts

MALIASILI YAZIDI KUNG'ARA MWANZA YAITANDIKA TIMU YA NETBALL YA KATIBA NA SHERIA 38-8 SHIMIWI 2025

September 03, 2025 Add Comment


Na John Bera – Mwanza


Timu ya netiboli ya Wizara ya Maliasili na Utalii imeendelea kuonesha ubabe kwenye Mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) kwa kuichapa kwa kishindo Wizara ya Katiba na Sheria kwa mabao 38–8, katika mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, jijini Mwanza.

Timu hiyo ilianza kwa kasi na kutawala mchezo kutoka mwanzo hadi dakika ya mwisho, ikionesha uelewano mzuri, umakini mkubwa na nidhamu ya hali ya juu uwanjani. Ushindi huo umeiweka Maliasili katika nafasi nzuri ya kusonga mbele kwenye hatua za mtoano.

Kocha wa timu hiyo, Bi. Rehema Kapela, amesema ushindi huo si wa bahati nasibu, bali ni matokeo ya maandalizi ya muda mrefu na ari ya wachezaji wake waliodhamiria kuweka historia mwaka huu.

“Tumekuwa tukifanya mazoezi kwa bidii na leo tumeona matokeo. Wachezaji wameonesha kujituma, umoja na uthabiti. Tuna malengo makubwa, na huu ni mwanzo mzuri kwetu,” alisema Kocha Kapela.

Mchezaji wa timu hiyo, Julia Kepha, ambaye aling’ara katika mchezo huo kwa kucheza kwa kiwango cha juu katika safu ya ulinzi, amesema walijiandaa kisaikolojia na kimwili kuhakikisha wanapata ushindi.

“Ushindi huu umetokana na kazi ya pamoja. Kila mmoja alitimiza majukumu yake. Tuliingia uwanjani tukiwa na malengo, na tulihakikisha tunayatimiza kwa vitendo,” alisema Julia.

Kwa upande wake, Kaimu  Mratibu wa Timu ya Wizara ya Maliasili na Utalii, Bw. George Rwezaura, amechukua fursa hiyo kuipongeza timu kwa ushindi huo wa kuvutia na kuahidi kuwa wataendelea kushirikiana na benchi la ufundi kuhakikisha timu inasonga mbele zaidi.

“Leo tumeandika historia dhidi ya timu ngumu. Ushindi huu umetupa hamasa kubwa na tunawaahidi watumishi wenzetu kwamba tutapambana hadi mwisho. Hakuna majeruhi, morali ni kubwa, na tumejiandaa vyema kwa mechi zijazo,” alisema George.

Katika michezo mingine ya leo, timu ya wanaume ya Maliasili iliibuka na ushindi wa bao 2–0 dhidi ya Tume ya Haki za Binadamu kwenye mchezo wa kuvuta kamba, huku timu ya wanawake ikipoteza kwa bao 1–0 dhidi ya timu ya Mkoa wa Geita (RAS Geita).


Kesho michezo hiyo itaendelea kwa timu Kamba ME kukutana na RAS Pwani na Kamba KE kukutana Maji wakati Netball watacheza na TAMISEMI

SHIMIWI NI MAHALA PA KAZI- BI ZIANA MLAWA

August 31, 2025 Add Comment


📌 *Asema Wizara ya Nishati ipambane irudi na ushindi*


📌 *Asema Wizara ya Nishati iwe mfano kwa Wizara zingine*


Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu Wizara ya Nishati, Bi. Ziana Mlawa leo amesema kushiriki michezo mbali mbali inasaidia katika kujenga afya ya mwili na akili hivyo mtumishi anapopata nafasi ya kushiriki michezo yeyote aitumie ipasavyo pia husaidia hali itakayowajengea uwezo kujiamini zaidi ikiwemo katika maeneo ya kazi.

Bi. Mlawa ameyasema hayo alipokuwa akiwaaga watumishi wa Wizara ya Nishati watakao shiriki michezo ya SHIMIWI itakayofanyika jijini Mwanza kwanzia tarehe 1 Septemba 2025


" Pamoja na kushiriki michezo ambapo ni mbali na eneo la kazi mkumbuke mkiwa huko ni eneo la kazi nidhamu na uadilifu uwe kipau mbele mdaa wote muwapo kwenye michezo  hiyo." Amesisitiza Bi. Mlawa


Ameongeza kuwa watumishi hao wajitahidi wapate ushindi ambapo kwa ushindi huo Wizara itapata heshima njee na ndani ya Wizara

DED MUHEZA ATOA AHADI NONO KWA WACHEZAJI WA TIMU YA HALMASHAURI HIYO

August 25, 2025 Add Comment

 


Na Oscar Assenga,TANGA

MKURUGENZI wa Halmashauri ya wilaya ya Muheza Mkoani Tanga Dkt. Juma Mhina ametoa ahaidi ya kununua kila goli litakalofungwa na timu ya mpira wa Miguu ya Halmashauri hiyo wa kiasi cha 20,000 ikiwa ni kutoa motisha kwa wachezaji wa Halmahauri hiyo wanaoshiriki katika Michuano ya Shimisemita inayoendelea Jijini Tanga.

Aliyasema hayo leo mara baada ya kutembelea timu hiyo kabla ya kuanza mchezo wa mpira wa miguu dhidi yao na Halmasahauri ya Mpimbwe ikiwa ni michuano ya Shimisemita inayoendelea kwenye viwanja v ya Shule ya Sekondari Ufundi Mkoani Tanga

Alisema kwamba anaridhishwa na kiwango na mwenendo wa timu hiyo katika mashindano hayo hivyo akaendelea kutoa hamasa kwao kuhakikisha wanaendelea kufanya vizuri na kuibuka na ubingwa.

“Hongereni sana mmefanya kazi kubwa sana kwa kuendelea kufanya vizuri naomba tuendelea kuwa na nidhamu msichoke tupo pamoja na tutaendelea kuwasapoti “Alisema Mkurugenzi huyo

Hata hivyo aliwataka kuendelea kuhakikisha wanaendelea kupambana ili kuweza kusonga hatua nyengine kwenye mashindano hayo huku akisisitiza nidhamu na kujituma

MUHEZA YAIGARAGAZA BUMBULI MAGOLI 3-2 MICHEZO SHIMISEMITA

August 24, 2025 Add Comment







Na Oscar Assenga,TANGA

TIMU ya Mpira wa Miguu ya Halmashauri  ya Wilaya ya Muheza imebamiza Halmashauri ya wilaya ya Bumbuli mabao 3-2 katika michuano ya Shirikisho la Michezo la Mamlaka za Serikali za Mitaa kaika mchezo uliochezwa kwenye viwanja vya Shule ya Ufundi Tanga.

Shirikisho hili la Michezo linahusisha watumishi waliopo katika Mamlaka za Serikali za Mitaa ( Halmashauri) waliopo kwenye idara na vitengo mbalimbali.

Katika mchezo huo ambao ulikuwa na upinzani mkubwa kutokana na kila timu kutaka kupata ushindi lakini Halmashauri ya wilaya ya Muheza iliweza kuhimili na kuutawala vyema mchezo huo na hatimaye kuweza kuibuka na kidedea
Mashindano ya Shirikisho la Serikali za Mitaa Tanzania ( SHIMISEMITA) yalianza rasmi Agosti 15, 2025 na yanatarajiwa kukamilika Agosti 29, 2025 huku yakilenga kuwakutanisha watumishi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa, kushirikiana pamoja, kufahamiana, kubadilishana mawazo, kujenga Afya za watumishi ili kuepukana na magonjwa yasiyoambukiza yakiwemo kisukari na shinikizo la damu.
Michezo hii inaendelea katika Viwanja mbalimbali vya Michezo vilivyopo Jijini Tanga huku yakiwa yamebeba Kauli mbiu ya SHIMISEMITA 2025  " Jitokeze kupiga Kura kwa maendeleo ya Michezo".

DKT. TULIA AKOSHWA NA CRDB BANK MARATHON IKIKUSANYA BILIONI 2 KUSAIDIA AFYA NA UWEZESHAJI JAMII

August 17, 2025 Add Comment

 


Dar es Salaam, 17 Agosti 2025 - Maelfu ya wakimbiaji na wapenda michezo kutoka ndani na nje ya Tanzania wamejitokeza leo katika viwanja vya The Green, Oysterbay, kushiriki CRDB Bank Marathon 2025, mbio za hisani ambazo mwaka huu zimekusanya Shilingi Bilioni 2 ili kusaidia matibabu ya watoto wenye matatizo ya moyo, wakinamama wenye ujauzito hatarishi, na vijana kupitia programu ya iMBEJU.

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Tulia Ackson Mwansasu, aliongoza maelfu ya washiriki kwenye msimu huu wa sita wa CRDB Bank Marathon.
Akitoa salamu zake, Dkt. Tulia alipongeza ubunifu wa CRDB Bank Foundation katika kuunganisha jamii kupitia michezo na kusaidia wenye uhitaji, akieleza kuwa mbio hizo ni mfano wa vitendo vya huruma vinavyogusa maisha ya wengi.

“Ushiriki wetu katika CRDB Bank Marathon ni tendo la huruma linaloleta faraja kwa watoto na wakinamama na familia zao. Ni ushahidi kwamba tukishirikiana, tunaweza kubadilisha maisha,” alisema.
Akitoa salamu zake, Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi, aliipongeza Benki ya CRDB na CRDB Bank Foundation kuendelea kuandaa mbio hizo.

Alisema, “CRDB Bank Marathon si tu imekuwa ikikuza afya na mshikamano wa kijamii, bali pia imekuwa ikifungua milango ya ajira na fursa za kiuchumi kwa vijana wetu. Michezo ni sekta inayoweza kubadili maisha, na ninapongeza sana kitendo cha kuweka zawadi nono kwa washindi. Hizi ni fursa ambazo zinaweza kuwa mtaji wa kuanzisha biashara na kuimarisha maisha ya vijana wetu. Serikali itaendelea kushirikiana na wadau kama CRDB Bank Foundation kuhakikisha michezo inakuwa chachu ya maendeleo ya taifa.”

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela, alibainisha kuwa msimu wa sita wa CRDB Bank Marathon umefanyika sambamba na maadhimisho ya miaka 30 ya Benki ya CRDB, na kuendelea kupanua wigo wa matokeo yake ndani na nje ya Tanzania. Kwa mara ya pili, mbio hizi zimefanyika pia nchini Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), zikikusanya fedha kwa ajili ya miradi ya afya na ustawi wa jamii katika nchi hizo.

Nsekela alisema kuwa mbio za mwaka huu zimeweza kuvutia zaidi ya washiriki 16,000, na kufanikisha lengo la kukusanya shilingi bilioni 2 ambapo pamoja na kusaidia maandalizi ya mbio hizo, shilingi milioni 450, zimeelekezwa kusaidia wenye uhitaji katika jamii.

Kati ya hizo shilingi milioni 100 zimekwenda hospitali ya CCBRT kusaidia wakinama wenye ujauzito hatarishi kujifungua salama, shilingi milioni 100 zimekwenda Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) kusaidia upasuaji wa Watoto wenye matatizo ya moyo, na shilingi 250 zitaelekezwa katika uwezeshaji wa vijana.
Akizungumza wakati wa kutangaza matokeo ya mbio hizo, Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation, Tully Esther Mwambapa, alieleza kuwa safari ya msimu wa sita imeanzia Lubumbashi, DRC, ambako zilikusanywa Dola za Marekani 70,000 kwa ajili ya kuboresha huduma za afya katika hospitali ya Jeshi la Ruashi, na kuendelea Bujumbura, Burundi, ambapo zilipatikana Faranga za Burundi milioni 175 kusaidia bima ya afya kwa zaidi ya watu 58,000 wasiojiweza.

Mwambapa alisisitiza kuwa mafanikio haya ni matokeo ya mshikamano wa kipekee wa serikali za nchi shiriki, wadhamini na washiriki, akiwashukuru wadau wote waliotoa jitokeza kuchangia ikiwamo kampuni za bima za Sanlam Life na Alliance Life ambao wamekuwa sehemu ya mbio hizi tangu kuanzishwa kwake.

Washindi wa mbio za mwaka huu upande wa Tanzania kwa Kilometa 42 upande wa wanawake ni Joyloyce Kemuma kutoka Kenya, upande wa wanaume mshindi ni Abraham Kiptum kutoka Kenya. Kilometa 21 upande wa wanawake ni Catherine Syokau kutoka Kenya, na upande wa wanaume ni Joseph Panga kutoka Tanzania. Kilometa 10 upande wa wanawake ni Silia Ginoka kutoka Tanzania, na upande wa wanaume ni Boayi Maganga kutoka Tanzania.

Joseph Panga mshindi wa mbio za Kilometa 21 upande wa wanawake ameeleza furaha yake kushiriki katika mbio hizo na kusema kuwa ushindi wake ni sehemu ya kusaida matibabu ya watoto wenye matatizo ya moyo na matibabu ya wakinamama wenye ujauzito hatarishi hospitali ya CCBRT.

“Mimi kama Mtanzania najisikia fahari kubwa kushiriki kusambaza tabasamu kwa watoto na wakinamama. Ni muhimu watu kufahamu kuwa afya bora ni haki ya kila mtoto, na hakuna mama anayestahili kupoteza maisha wakati wa kujifungua. Tunawashukuru CRDB Bank Foundation kwa kutuleta pamoja katika harakati hizi za kuokoa maisha,” amesema.
CRDB Bank Marathon imekuwa jukwaa muhimu la kuchochea ustawi wa kijamii katika ukanda huu wa Afrika ya Mashariki na kati hivi karibuni ikipata heshima ya kutambuliwa kimataifa kwa kushinda tuzo ya jukwaa bora la taasisi za fedha katika kusaidia kusaidia jamii.