KATIBU SUK RABIA: TANGA INA MISINGI IMARA, TUONGEZE KASI YA KAZI

November 01, 2026



Asema amekuta msingi imara wa chama, ataja mafanikio ya Samia, Bandari ya Tanga yazidi kufungua uchumi

Na Oscar Assenga, TANGA

Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Idara ya Mambo ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa (SUKI), Rabia Abdalla Hamid amesema amepokea jukumu la kulea mkoa huo kwa furaha kubwa, akieleza kuwa amekuta mazingira mazuri ya kisiasa yaliyowekwa na viongozi waliomtangulia.

Amesema kabla ya kuwasili Tanga, alifahamu kuwa hatakuwa na kazi kubwa ya kuimarisha chama kutokana na misingi imara iliyojengwa na Mwenyekiti wa CCM Mkoa Rajab Abdurhaman pamoja na mlezi aliyekuwepo awali.

Rabia ambaye pia ni Mlezi Mpya wa chama hicho Mkoa wa Tanga aliyasema hayo leo wakati akizungumza na viongozi na wanachama wa CCM mkoani humo mara baada ya kupokelewa rasmi ambapo amefika Tanga kwa kazi maalumu aliyopewa na Makao Makuu ya chama, ikiwamo kuhakikisha viongozi na wananchi wanatambua nafasi ya CCM katika kusimamia maendeleo ya mkoa na taifa kwa ujumla.

Alisema alitumia uzoefu alioupata wakati akiulea Mkoa wa Kilimanjaro kwa miaka mitatu, akibainisha kuwa Tanga imekuwa na mazingira tofauti ya kisiasa na kijamii yaliyompa furaha kubwa katika utekelezaji wa majukumu yake.

Alieleza kuwa jukumu lake kubwa ni kuhakikisha chama kinaendelea kuwa karibu na wananchi na kusimamia utekelezaji wa majukumu yake kwa kuzingatia misingi na maadili ya CCM.

Katika hatua nyingine, Rabia aliwataka viongozi wa chama na Serikali kuelewa kuwa utendaji wao haupimwi kwa maneno mengi, bali kwa matokeo ya kazi wanazozifanya.

Alisema CCM ni chama kinachopaswa kuwa kazini saa 24, huku akisisitiza kuwa ni sikivu, mwadilifu na kinachozingatia utu katika kuwahudumia wananchi.

Aliongeza kuwa kaulimbiu ya chama ya mwaka huu, Kazi na Utu Tunasonga Mbele, inaakisi dhamira ya kuendeleza huduma na maendeleo kwa Watanzania.

Akizungumzia uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, alisema moja ya sifa kubwa zinazomtambulisha ni utu, akieleza kuwa falsafa hiyo inaonekana katika matendo na utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayofanyika maeneo mbalimbali nchini.

Alisema tangu nchi ipate uhuru, viongozi waliotokana na CCM wamekuwa wakichangia maendeleo ya taifa kulingana na uwezo na mazingira ya vipindi vyao vya uongozi.

Rabia alisisitiza kuwa maendeleo hayapaswi kubagua maeneo, akieleza kuwa serikali imeendelea kusambaza miradi katika mikoa na kata mbalimbali nchini.

Aidha, alizungumzia umuhimu wa kulinda amani na mshikamano wa kitaifa, akiwataka Watanzania kutofautisha ushindani wa kisiasa na masuala yanayohusu masilahi mapana ya nchi.

Alisema wananchi wanaweza kuwa na mitazamo tofauti ya kisiasa, lakini hawapaswi kuruhusu tofauti hizo kuathiri umoja na usalama wa taifa.

Katika kuelezea hali ya uhusiano wa Tanzania na mataifa mengine, Rabia alisema baadhi ya changamoto zilizokuwepo katika mahusiano ya kimataifa zimeendelea kushughulikiwa, huku akisisitiza kuwa Tanzania inaendelea kuwa nchi yenye amani na usalama.

Alitumia nafasi hiyo kuwataka wananchi kuendelea kuilinda nchi na kutanguliza masilahi ya taifa badala ya misimamo ya kisiasa.


RAJAB: TANGA NI NGOME IMARA YA CCM

Awali, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tanga, Rajab Abdurahman, alisema mkoa huo umeendelea kuwa ngome ya chama hicho, akieleza kuwa kipaumbele cha sasa ni kuimarisha umoja na kusimamia maendeleo ya wananchi.

Alisema kazi kubwa iliyopo mbele yao si kujikita katika malumbano ya kisiasa, bali kuhakikisha Tanga inasonga mbele kiuchumi na kijamii.

Hata hivyo, akizungumzia kauli za wapinzani kuhusu mipango yao ya kufanya shughuli za kisiasa mkoani humo, Rajab alisema CCM iko tayari kuendelea kuimarisha chama chake na kuonyesha mafanikio ya utekelezaji wa shughuli za maendeleo.

Alisema wananchi wa Tanga wana nafasi ya kujionea mabadiliko yanayotokana na miradi inayotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan.

Akitoa mfano wa mafanikio hayo, alitaja uwekezaji wa Sh bilioni 429.1 katika Bandari ya Tanga, akisema umechangia kuboresha miundombinu ya bandari hiyo, ikiwamo kuongeza kina cha maji ili kuruhusu meli kubwa kutia nanga.

Alisema kwa muda mrefu wakazi wa Tanga walikuwa na kilio cha kuboreshwa kwa bandari hiyo ili kuongeza shughuli za kiuchumi na kufungua fursa za biashara.

Rajab alisema baada ya maboresho hayo, Bandari ya Tanga imeanza kuvutia meli kubwa ambazo awali zilikuwa zikielekezwa zaidi katika bandari nyingine, hatua aliyoeleza kuwa imeanza kuchochea shughuli za kiuchumi mkoani humo.

Aliongeza kuwa ongezeko la shughuli za kiuchumi limeambatana na ongezeko la magari na shughuli za usafirishaji, hali inayofanya baadhi ya wananchi kuanza kutoa malalamiko kuhusu udogo wa barabara ikilinganishwa na mahitaji ya sasa.

Alisema hali hiyo ni ishara ya kuongezeka kwa shughuli za kiuchumi na umuhimu wa kuendelea kuboresha miundombinu ili kwenda sambamba na kasi ya maendeleo ya mkoa.










Share this

Related Posts

Previous
Next Post »