GLOBAL MEDICARE yaongeza nguvu uwekezaji wa teknolojia TIBA JKCI

November 01, 2026
NA Mwandishi wetu Arusha ARUSHA

Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na Global Medicare inaendelea kuimarisha Hospitali ya JKCI-ALMC (Selian ya Mjini) Arusha kupitia uwekezaji wa miundombinu, teknolojia na vifaa tiba vya kisasa, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya huduma za afya kuelekea mashindano ya AFCON 2027 na kuboresha huduma za kudumu kwa wananchi wa Kanda ya Kaskazini.

Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Dkt. Peter Richard Kisenge, amesema maandalizi hayo yanahusisha uwekezaji mkubwa katika huduma za dharura, Sports Medicine, vifaa vya uchunguzi, teknolojia za ufuatiliaji wa wagonjwa pamoja na kuongeza uwezo wa hospitali kutoa huduma za kibingwa na kibobezi.

Amesema ushirikiano na Global Medicare umechangia katika maboresho ya miundombinu na uwekezaji wa teknolojia za vifaa tiba, huku baadhi ya vifaa vipya vikiwa katika hatua mbalimbali za kuwasili na kufungwa katika JKCI-ALMC.

“Tumeshirikiana na wenzetu wa Global Medicare katika kuhakikisha hospitali hii inaboreshwa katika miundombinu na vifaa tiba. Madaktari wetu tayari wamekwenda kuona baadhi ya vifaa na sasa viko katika mchakato wa kufungwa,” amesema Dkt. Kisenge.

Dkt. Kisenge amesema zaidi ya Sh bilioni nane tayari zimetumika katika maboresho mbalimbali ya JKCI-ALMC, ikiwemo ukarabati wa miundombinu, ununuzi wa vifaa tiba, kuimarisha huduma za mifupa na kuandaa vyumba maalumu vya VIP.

Amesema baadhi ya vyumba hivyo vina vifaa vinavyowezesha kutoa huduma za kiwango cha juu na vinaweza kubadilishwa kutoa huduma za ICU kulingana na hali ya mgonjwa.

Dkt. Kisenge amesema moja ya malengo makubwa ya uwekezaji unaoendelea ni kuifanya JKCI-ALMC kuwa Smart Hospital, ambapo teknolojia itatumika katika hatua mbalimbali za huduma za mgonjwa.

“Tunataka kila kitu kiwe automated. Mgonjwa akifika aweze kusajiliwa kwa kutumia teknolojia, vipimo na monitoring vifanyike kwa mifumo ya kisasa na madaktari watumie kompyuta zenye Artificial Intelligence kuwasaidia katika kazi zao,” amesema.

Hospitali hiyo pia inatarajia kuongezewa vifaa vya kisasa vya MRI, CT Scan na Cardiac Catheterization Laboratory (Cath Lab) ambavyo vitaongeza uwezo wa uchunguzi na matibabu ya magonjwa mbalimbali, hususan ya moyo.

Dkt. Kisenge amesema JKCI pia inaendelea kutumia teknolojia za ufuatiliaji wa wagonjwa zinazoweza kutambua mabadiliko ya viashiria muhimu vya afya kama shinikizo la damu, mapigo ya moyo na kiwango cha oksijeni.

Aidha, taasisi hiyo inapanga kutumia vifaa vya kisasa vya kujipima afya katika baadhi ya maeneo watakayofikia wageni wakati wa AFCON ili kusaidia kutambua mapema matatizo ya kiafya.

Mkurugenzi wa Hospitali ya JKCI-ALMC, Dkt. Tatizo Waane, amesema hospitali hiyo imejiandaa kutoa huduma kwa wananchi, wachezaji na wageni watakaofika Arusha wakati wa mashindano ya AFCON 2027.

Amesema JKCI-ALMC ni miongoni mwa hospitali zilizofanyiwa tathmini katika maandalizi ya huduma za afya wakati wa mashindano hayo.

“Tumeimarisha huduma za dharura, tumeboresha wodi na tuna maeneo maalumu ambayo yako tayari kuhudumia wananchi, wageni na wanamichezo watakaopata matatizo wakati wa mashindano,” amesema Dkt. Waane.

Amesema hospitali imejiandaa kukabiliana na majeraha yanayoweza kutokea kwa wanamichezo, yakiwemo ya mifupa, viungo, ubongo, mishipa ya fahamu na changamoto nyingine zinazohusiana na michezo.

Kwa mujibu wa Dkt. Waane, JKCI-ALMC tayari inatoa huduma za kibingwa katika magonjwa ya moyo, upasuaji wa ubongo, mifupa, tumbo, watoto, macho na masikio, pamoja na huduma za magonjwa ya ndani.

Hospitali pia inatoa huduma kwa watoto chini ya miaka 18, watoto wachanga na njiti pamoja na kuwa na maabara na huduma mbalimbali za uchunguzi.

Share this

Related Posts

Latest
Previous
Next Post »