NA EMMANUEL MBATILO, BAGAMOYO
MKUU wa Wilaya ya Bagamoyo amewataka wadau mbalimbali kuongeza ushirikiano katika kufanikisha Tamasha la Kimataifa la Sanaa na Utamaduni Bagamoyo ili liendelee kudumu na kukuza sekta ya sanaa nchini.
Akizungumza katika kilele cha Tamasha la 44 la Kimataifa la Sanaa na Utamaduni lililofanyika katika viwanja vya Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa), Mkuu huyo wa Wilaya amesema ushirikiano wa wadau ni muhimu katika kukabiliana na changamoto za maandalizi na uendeshaji wa matamasha makubwa.
Amesema TaSUBa imefanya kazi kubwa ya kuhakikisha tamasha hilo linaendelea kufanyika kwa miaka 44 mfululizo, hatua inayopaswa kupongezwa kutokana na mchango wake katika kuhifadhi, kukuza na kuendeleza sanaa na utamaduni wa Tanzania.
Ametoa pongezi kwa Kaimu Mkuu wa Taasisi hiyo, uongozi, wafanyakazi, wanachuo na kamati zote za tamasha kwa juhudi wanazozifanya kila mwaka kuhakikisha tukio hilo linaendelea kufanyika.
Aidha, amewataka waandaaji wa tamasha hilo na matamasha mengine nchini kuendelea kufungua milango kwa wadau wengi zaidi ili washirikiane katika kugharamia na kuendesha matukio hayo muhimu kwa Taifa.
Katika hatua nyingine, amewapongeza wasanii wote walioshiriki tamasha hilo, akieleza kuwa baadhi yao walijigharamia wenyewe ili kuhakikisha wanakuwa sehemu ya tukio hilo.
Amesema kujitolea kwa wasanii hao ni ishara ya uthubutu na mshikamano katika kudumisha na kuendeleza sanaa na utamaduni wa Taifa.
Vilevile, aliwahamasisha wananchi wa Bagamoyo na Watanzania kwa ujumla kujitokeza kwa wingi kuhudhuria na kushiriki matamasha yajayo ili kuwapa moyo wasanii na kuthamini kazi zao.
Amewashukuru wadhamini na taasisi mbalimbali zilizojitokeza kusaidia kufanikisha tamasha hilo kwa namna tofauti.
Wadhamini hao ni Azam Media Limited, ITV na Radio One, EGA, Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi la Polisi Tanzania (TPFCS), SUMA JKT, Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Hospitali ya Wilaya ya Bagamoyo, Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, Malkia Events Management and Tents Limited na Coca-Cola.
Wengine ni Bagamoyo Friendship Society, Ofisi ya Hakimiliki Tanzania (COSOTA), BRELA, TwiBhok Bagamoyo, Shule ya Sekondari Baobab, Bonge Hardware, Klimario Hardware, Salehe Mguu Hardware, Stella Maris Hotel, TANLAPIA, Ofisi ya Ardhi Bagamoyo, DAWASA Bagamoyo na Travellers Lodge, pamoja na vikundi mbalimbali vilivyojigharamia kushiriki tamasha hilo.











EmoticonEmoticon