LINDI, OKTOBA 26, 2026
Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Juma Zuberi Homera, amezindua Shule ya Awali na Msingi Likong’o, iliyopo mkoani Lindi, iliyojengwa kupitia mpango wa Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) wa Mradi wa Kusindika Gesi Asilia kuwa Gesi Asilia Kimiminika (LNG), ikiwa na uwezo wa kuhudumia wanafunzi 400.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa shule hiyo, Oktoba 26, 2026, Dkt. Homera amesema Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeendelea kusisitiza kuwa maendeleo ya sekta ya nishati lazima yaendane na manufaa ya moja kwa moja kwa wananchi wanaozunguka miradi mikubwa ya kimkakati.
Amesema ujenzi wa Shule ya Awali na Msingi Likong’o ni mfano wa utekelezaji wa dhamira hiyo kupitia mpango wa CSR unaotekelezwa na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), kwa kushirikiana na washirika wa Mradi wa LNG.
Ameeleza kuwa shule hiyo imejengwa kwa gharama ya Shilingi bilioni 1.278, huku Serikali ikitoa msamaha wa kodi kwa ajili ya mradi huo, hatua inayodhihirisha dhamira ya kuhakikisha rasilimali za taifa zinachangia maendeleo endelevu ya wananchi.
“Nimeelezwa na kujionea mwenyewe kuwa mradi huu umekamilika kwa asilimia 100, ukiwa umezingatia viwango vya ubora, usalama na masharti ya kimkataba. Shule hii iliyojengwa kisasa itahudumia wanafunzi takribani 400, wakiwemo wanafunzi 350 wa shule ya msingi na 50 wa shule ya awali, kwa kutoa mazingira bora ya kujifunzia yanayolenga kupunguza msongamano wa wanafunzi madarasani na kuongeza kiwango cha ufaulu,” amesema Dkt. Homera.
Ameongeza kuwa shule hiyo ina madarasa yenye nafasi stahiki, majengo ya utawala pamoja na nyumba za walimu kwa lengo la kuboresha mazingira ya kazi na makazi yao na kuongeza ufanisi katika ufundishaji.
Aidha, shule hiyo imejengwa kwa kuzingatia mahitaji ya watu wenye ulemavu, ikiwemo vyoo maalumu na miundombinu inayowezesha watu wenye mahitaji maalumu kufika na kutumia huduma hizo kwa urahisi. Pia, imewekewa mfumo wa usimamizi wa taka kwa ajili ya kulinda afya na usalama wa wanafunzi na walimu.
Dkt. Homera amefafanua kuwa manufaa ya mradi huo yamevuka mipaka ya elimu na kugusa moja kwa moja maendeleo ya kiuchumi na kijamii ya wananchi wa Likong’o na vijiji jirani.
Amesema wakati wa ujenzi wa shule hiyo, zaidi ya wananchi 150 walipata fursa za ajira katika hatua mbalimbali za utekelezaji wa mradi, huku taasisi na kampuni za ndani ya Manispaa ya Lindi zikipatiwa kipaumbele katika usambazaji wa vifaa na utoaji wa huduma mbalimbali.
Vilevile, mradi huo umewezesha ujenzi wa bomba la maji safi lenye urefu wa takribani kilomita 1.5 kutoka kwenye miundombinu ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Lindi (LUWASA). Miundombinu hiyo itahudumia shule na kunufaisha pia kaya zinazozunguka eneo hilo.
Katika kuimarisha uhifadhi wa mazingira, TPDC kwa kushirikiana na wawekezaji, Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), walimu, wanafunzi na wazazi, imeratibu zoezi la upandaji wa miti 2,000 kuzunguka shule hiyo. Hatua hiyo inalenga kuhamasisha utunzaji wa mazingira na kujenga utamaduni wa uhifadhi miongoni mwa jamii.
Akihitimisha, Dkt. Homera ameitaka jamii inayozunguka shule hiyo kutunza na kulinda miundombinu iliyojengwa ili iendelee kutoa huduma bora kwa watoto wa sasa na vizazi vijavyo.











EmoticonEmoticon