TVLA YAIMARISHA USHIRIKIANO NA WAUZAJI WA PEMBEJEO KULINDA AFYA YA MIFUGO

October 23, 2026


Na Daudi Nyingo – Sumbawanga

WAKALA ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) imeendelea kuimarisha juhudi za kulinda afya ya mifugo kwa kutoa elimu kuhusu huduma zake pamoja na utambuzi, uhifadhi na matumizi sahihi ya chanjo kwa wauzaji wa pembejeo za mifugo katika mikoa ya Rukwa na Songwe.

Elimu hiyo imetolewa katika ziara iliyofanyika kuanzia Oktoba 19 hadi 22, 2026, kupitia Kituo cha TVLA cha Kanda ya Kusini Magharibi kilichopo Sumbawanga, kinachohudumia mikoa ya Rukwa, Katavi na Songwe.

Ziara hiyo imeongozwa na Meneja wa Kituo hicho, Dkt. Rajabu Mlekwa, kwa kushirikiana na wataalamu wa masoko kutoka TVLA Makao Makuu ambapo timu hiyo imewatembelea wauzaji wa pembejeo katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi, Halmashauri ya Mji wa Tunduma, Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga na Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga.

Katika ziara hiyo, wauzaji wamepatiwa elimu kuhusu huduma zinazotolewa na Wakala, zikiwemo uchunguzi na utambuzi wa magonjwa ya wanyama, uzalishaji na usambazaji wa chanjo za mifugo, uhakiki wa ubora wa vyakula vya mifugo, usajili na udhibiti wa ubora wa viuatilifu vya mifugo, utafiti wa magonjwa ya wanyama na wadudu wanaoeneza magonjwa hayo, pamoja na utoaji wa ushauri na mafunzo kwa wadau wa sekta ya mifugo.

Kwa upande wa chanjo, wauzaji wameelimishwa kuhusu namna ya kuzitambua chanjo zinazozalishwa na TVLA, uhifadhi sahihi, kuzingatia maelekezo ya matumizi na kufuata taratibu za kitaalamu ili kudumisha ubora na ufanisi wake.

Zoezi hilo limelenga kuwajengea uwezo wauzaji wa pembejeo kama kiungo muhimu cha kuwafikia wafugaji, ili waweze kutoa elimu sahihi kuhusu chanjo na kuwaelekeza kupata huduma nyingine za TVLA kulingana na mahitaji yao.

Uelewa wa huduma hizo unawasaidia wauzaji kuwafahamisha wafugaji kuhusu umuhimu wa uchunguzi wa magonjwa katika maabara, uhakiki wa ubora wa vyakula vya mifugo na kupata ushauri wa kitaalamu katika kukabiliana na changamoto za afya na uzalishaji wa mifugo.

Kupitia ziara hiyo, TVLA imeendelea kuimarisha ushirikiano na wauzaji wa pembejeo, kutangaza bidhaa na huduma zake na kusogeza elimu karibu na wadau, kwa lengo la kulinda afya ya mifugo na kuongeza tija katika ufugaji nchini.
Meneja wa Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA), Kanda ya Kusini Magharibi, Dkt. Rajabu Mlekwa, akitoa elimu kuhusu huduma za Wakala na matumizi sahihi ya chanjo kwa muuzaji wa pembejeo za mifugo eneo la Mlowo, wilayani Mbozi, mkoani Songwe, Oktoba 19, 2026, ili kuwajengea uwezo wa kuwafikishia wafugaji elimu sahihi.
Meneja wa Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA), Kanda ya Kusini Magharibi, Dkt. Rajabu Mlekwa, akifafanua namna sahihi ya kuhifadhi na kutumia chanjo kwa muuzaji wa pembejeo za mifugo mjini Tunduma, mkoani Songwe, wakati wa ziara ya Oktoba 20, 2026, kwa lengo la kudumisha ubora wa chanjo na kuimarisha huduma kwa wafugaji.
Afisa Masoko wa Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA), Bw. Fihiri Mbawala, akitoa maelezo kuhusu bidhaa na huduma za Wakala kwa muuzaji wa pembejeo za mifugo eneo la Vwawa, wilayani Mbozi, mkoani Songwe, Oktoba 19, 2026, ili kuongeza uelewa na kuimarisha ushirikiano katika kuwafikia wafugaji.
Meneja wa Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA), Kanda ya Kusini Magharibi, Dkt. Rajabu Mlekwa, pamoja na Afisa Masoko wa TVLA kutoka Makao Makuu, Bw. Fihiri Mbawala, wakiwa katika picha ya pamoja na wauzaji wa pembejeo za mifugo mjini Tunduma, mkoani Songwe, Oktoba 20, 2026, baada ya kutoa elimu kuhusu huduma za Wakala na matumizi sahihi ya chanjo za mifugo kwa lengo la kuwajengea uwezo wa kuwahudumia wafugaji.
Matukio mbalimbali yakiwaonesha wataalamu wa Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) wakitoa elimu kuhusu huduma za Wakala, utambuzi, uhifadhi na matumizi sahihi ya chanjo, pamoja na kubandika mabango ya elimu katika maeneo ya biashara za wauzaji wa pembejeo za mifugo katika halmashauri za Mbozi, Tunduma, Sumbawanga Wilaya na Sumbawanga Manispaa, Oktoba 19–22, 2026, ili kuwajengea uwezo wauzaji hao wa kuwahudumia wafugaji na kurahisisha upatikanaji wa taarifa za bidhaa na huduma za TVLA.

Share this

Related Posts

Latest
Previous
Next Post »