Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Hamad Yusuf Masauni, ameliagiza Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kushirikiana kwa karibu na Halmashauri zote nchini kudhibiti uchafuzi wa mazingira na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu usimamizi, udhibiti na urejelezaji wa taka pamoja na suala la usafi wa Mazingira.
Mhe. Masauni ametoa agizo hilo wakati wa ziara ya ukaguzi wa mazingira jijini Dar es Salaam, iliyolenga kufuatilia utekelezaji wa maelekezo ya Serikali kuhusu usafi wa mazingira, uhifadhi wa mito na mifereji pamoja na udhibiti wa taka. Awali aliongoza zoezi la usafi wa mazingira Soko la Kariakoo.
Mhe. Masauni amesema Serikali ipo kwenye mchakato wa kuifanyia marekebisho Sheria ya Mazingira ili kuipa nguvu zaidi na haitasita kuchukua hatua dhidi ya wanaokiuka taratibu za uhifadhi na utunzaji wa mazingira.
Kwaupande wake, Kaimu Meneja wa Kanda ya Ilala, Bi. Zainabu Kuhanwa, amesema NEMC inaendelea kushirikiana na Halmashauri zote nchini kuhakikisha usafi, uhifadhi na utunzaji wa mazingira unatekelezwa kwa ufanisi.
Aidha, Mhe. Masauni amewataka wananchi kuzingatia tahadhari na maelekezo ya Serikali kuhusu mvua za El Niño, ikiwemo kuepuka kutupa taka kwenye mito na mifereji ili kupunguza athari za mafuriko. Ziara hiyo ilihusisha Mnazi Mmoja, Mchafukoge, Mto Msimbazi, Kipawa, Karakata, Goba, Mto Ng’ombe Tandale, Mtaa wa Muhalitan na Daraja la Mkwajuni.





EmoticonEmoticon