SHULE YA VUGA BAZO YANUFAIKA NA HOSTELI, VYOO 14

November 17, 2026


Wadau wa maendeleo waombwa kuongeza vitanda, nyumba za walimu na miundombinu mingine ili kuboresha mazingira ya kujifunzia na kuinua ufaulu wa wanafunzi.

Na Mwandishi Wetu, Bumbuli

SHULE ya Sekondari Vuga Bazo iliyopo Kata ya Soni, Halmashauri ya Bumbuli, Mkoa wa Tanga, imenufaika na ujenzi wa hosteli ya wavulana pamoja na matundu 14 ya vyoo, hatua inayotarajiwa kuondoa changamoto ya uhaba wa vyoo na umbali mrefu wa safari kwa wanafunzi.

Mradi huo umefadhiliwa na Shirika la Better World Canada kwa kushirikiana na  Shirika la Vuga Development Initiative kutekeleza mradi huo kwa  kwa gharama ya shilingi Milioni 93.

Akizungumza kuhusu manufaa ya mradi huo, Mkuu wa Shule ya Sekondari Vuga Bazo, Mathias Chambwite, alisema shule hiyo ilikuwa ikikabiliwa na changamoto kubwa ya uhaba wa matundu ya vyoo pamoja na kukosekana kwa hosteli kwa wanafunzi wanaotoka maeneo ya mbali.

Alisema kabla ya msaada huo, shule ilikuwa na matundu 12 ya vyoo, hali iliyosababisha wanafunzi kusubiri kwa muda mrefu ili kupata nafasi ya kutumia vyoo kutokana na idadi kubwa ya wanafunzi.

Chambwite alisema kwa sasa shule imeongezewa matundu 14 na kufanya jumla ya matundu ya vyoo kufikia 26, ambayo yanakidhi mahitaji ya wanafunzi 390, wakiwemo wasichana 210 na wavulana 180.

Alisema ujenzi huo umeondoa changamoto iliyokuwa ikiathiri mazingira ya kujifunzia na kwamba uwepo wa hosteli utawasaidia wanafunzi wanaotoka maeneo ya mbali kupata nafasi nzuri ya kulala, kupumzika na kujisomea.

“Tunawashukuru sana wafadhili wa Better World Canada kwa kutusaidia kujenga hosteli na vyoo. Changamoto kubwa tuliyokuwa nayo ilikuwa miundombinu, lakini kupitia msaada huu tunaamini wanafunzi watapata mazingira mazuri ya kusoma na kufikia malengo yao,” alisema Chambwite.

Alisema kwa upande wa Serikali, shule hiyo haina changamoto kubwa ya walimu, kwani ina walimu wa kutosha, walimu wa masomo ya sayansi pamoja na mtaalamu wa maabara.

Hata hivyo, aliwaomba wadau wengine kuendelea kuisaidia shule hiyo, hasa kwa kuongeza vitanda vya hosteli, kujenga jengo la utawala na kuongeza nyumba za walimu ambazo bado hazitoshelezi mahitaji ya watumishi waliopo.

Alisema shule hiyo ina idadi kubwa ya wanafunzi wa kike ambao wanahitaji mazingira bora ya kujifunzia ili waweze kutimiza ndoto zao, akibainisha kuwa jitihada za kuwawezesha wasichana kuendelea na masomo ni muhimu katika kukabiliana na changamoto zilizokuwa zikiwakwamisha hapo awali.


Mratibu wa Shirika la Vuga Development Initiative, Rama Kaoneka aliwataka watu walisoma katika  shule hiyo watambue nyumbani ni nyumbani hivyo ni vizuri wakumbuke na kurudisha fadhila zao ili wanafunzi waweze kusoma sehemu nzuri.

Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Vuga, Jumaa Dhahabu, alisema wanamshukuru Mungu na wafadhili kwa kufanikisha ujenzi wa hosteli hiyo, akieleza kuwa awali wanafunzi walikuwa wakitembea umbali wa zaidi ya kilomita 18 kwenda na kurudi shuleni kila siku.

Alisema hali hiyo ilikuwa ikiathiri maendeleo ya kitaaluma ya wanafunzi na kuchangia matokeo yasiyoridhisha, kutokana na uchovu waliokuwa wakipata wakati wa safari.

“Tunawashukuru sana wafadhili kwa kuona changamoto iliyokuwa ikiikabili shule yetu. Tunaamini hosteli hii itabadilisha matokeo ya wanafunzi kwa sababu sasa watapata nafasi ya kukaa karibu na shule na kutumia muda mwingi kujisomea,” alisema Dhahabu.

Aliwapongeza Shirika la Better World Canada pamoja na Kaoneka, Mkurugenzi wa Shirika la Vuga Development Initiative, kwa juhudi zake za kuunganisha jamii na wafadhili, huku akitoa wito kwa wadau wengine kujitokeza kusaidia ujenzi wa mabweni zaidi ili wanafunzi wengi waweze kupata huduma hiyo.

Naye Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Bumbuli, Magreth, aliishukuru Better World Canada kwa kuendelea kushirikiana na halmashauri katika sekta za elimu na afya, akizitaja kuwa ni maeneo muhimu yanayogusa maisha ya wananchi.

Alisema pamoja na hosteli ya wavulana na matundu 14 ya vyoo, halmashauri inaomba wadau hao waendelee kusaidia miradi mingine ya maendeleo, ikiwemo ujenzi wa hosteli ya wasichana katika shule hiyo.

Aidha, alisema halmashauri inahitaji shule nyingine ya sekondari yenye masomo ya sayansi kwa ngazi ya kidato cha tano na sita, ili kuwasaidia wanafunzi wanaofaulu kidato cha nne lakini wanashindwa kuendelea na masomo katika maeneo ya mbali kama Arusha, Kigoma na Dar es Salaam kutokana na changamoto za kifedha kwa wazazi.

Alisema upatikanaji wa shule hiyo utasaidia wanafunzi wengi kuendelea na masomo ya sayansi, kufikia elimu ya juu na baadaye kuwa wataalamu watakaolisaidia eneo hilo.

Pia aliomba msaada wa ujenzi wa jengo la utawala na upatikanaji wa vitanda ili hosteli hiyo iweze kuanza kupokea wanafunzi kuanzia Januari mwakani.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Lushoto ambaye pia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Bumbuli, Zepahia Sumaye, aliwashukuru wafadhili na Shirika la Vuga Development Initiative kwa juhudi za kuunganisha halmashauri na wadau wa maendeleo.

Sumaye alisema mchango huo ni mkubwa katika kuboresha miundombinu ya elimu, akibainisha kuwa pamoja na juhudi zinazofanywa na Serikali katika ujenzi wa madarasa, vyoo na hosteli, bado kuna mahitaji mengine yanayohitaji ushirikiano wa wadau.

Alisema hosteli hiyo itawasaidia wanafunzi kupata sehemu salama ya kulala, kupumzika na kujisomea, hivyo kuongeza uwezekano wa kufanya vizuri katika masomo yao.

Aliwataka wananchi kutambua umuhimu wa maendeleo yanayoletwa na wadau na kuhakikisha wanatunza miundombinu inayojengwa kwa manufaa ya jamii.

“Tunawaomba wanafunzi na wananchi wote kutunza majengo haya, hosteli na matundu ya vyoo 14 ili yaweze kudumu na kuwa na thamani. Wafadhili wanapokuja kuona matumizi mazuri ya miradi waliyoigharamia, wanapata moyo wa kuendelea kutusaidia,” alisema Sumaye.

Pia alimshukuru Kaoneka kwa jitihada zake za kutafuta marafiki na mashirika ya maendeleo, akieleza kuwa ushirikiano huo umechangia kupatikana kwa miradi mbalimbali katika eneo la Bumbuli.

Aidha, alimwomba Diwani wa Kata ya Vuga kuratibu harambee ya kuchangisha fedha kwa ajili ya ununuzi wa vitanda vya hosteli, huku akiahidi kuchangia katika zoezi hilo.

Alisema ushirikiano kati ya Serikali, wananchi na wadau wa maendeleo ni muhimu katika kuhakikisha shule hiyo inapata miundombinu inayokidhi mahitaji ya wanafunzi na kuboresha kiwango cha elimu katika eneo hilo.









Share this

Related Posts

Previous
Next Post »