KILIMANJARO IPO TAYARI KUKABILIANA NA MADHARA YA EL NINO

October 03, 2026


 


Na Mwandishi Wetu-Kilimanjaro

 

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Mhe. Nurdin Babu amesema, Mkoa wa Kilimanjaro umejiandaa na kujipanga kukabiliana na madhara ya mvua za El Niño zinazotarajiwa kuanza hivi karibuni kwa mujibu wa taarifa kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA).

 

Mhe. Babu ameyasema hayo leo ​Octoba 03, 2026 katika Ofisi za Mkuu wa Mkoa wake wakati akiongoza kikao kazi cha kujadili utekelezaji wa maelekezo yaliyotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na wenye Ulemavu) kwa Mikoa kuhusu Kujiandaa na Kukabiliana na Madhara ya El Niño.

 


“Mkoa wa Kilimanjaro unathamini umuhimu wa mvua katika shughuli za kiuchumi ikiwemo kilimo, lakini mvua hizi zikiwa nyingi huleta madhara kwa wananchi na kiuchumi, tunahitaji mvua za wastani zitakazosaidia wananchi wetu” ameeleza Mhe. Babu

 

Aidha, Mhe. Babu amesema kuwa, Mkoa wake upo tayari kabla na hata baada ya mvua hizo kwani umejipanga kikamilifu katika kukabiliana na madhara yatakayojitokeza.

 


Vilevile, Mhe. Babu amewataka wananchi wanaoishi katika maeneo hatarishi kuhama mara moja ili kuepusha madhara mbalimbali yatakayojitokeza katika mvua hizo na kuhimiza wananchi kutodharau taarifa zinazotolewa na TMA.

 


“Tumetenga maeneo ya makazi kuhakikisha kama kutatokea dharura ya basi yatasaidia wananchi watakaoathirika, tumesafisha mifereji, tumezibua makalvati, hatutupi taka hovyo hii itasaidia kuimarisha miji yetu” ameeleza Mhe. Babu.

 


Mbali na hayo Mhe. Babu ameishukuru Ofisi ya Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na wenye Ulemavu) kwa kuwapatia vifaa vitakavyosaidia wakati wa madhara mbalimbali yatakapojitokeza katika mvua hizo

 

Kwa upande wake Mratibu wa Maafa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu Bi. Janeth Msimbe amebainisha kuwa, Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kushirikisha wizara, taasisi, Mamlaka za Mikoa, Mashirika ya Kiserikali na yasiyo ya Serikali iliratibu maandalizi ya Mpango wa Dharura wa Taifa wa Kukabiliana na Madhara ya El Nino kwa kipindi cha Julai, 2026 hadi Juni, 2027.

 


“Mipango iliyoandaliwa katika ngazi za mikoa, wizara na taasisi ilijumishwa katika maadalizi ya mpango wa taifa, pia rasilimali za utekezaji wa mpango huu zitatoka katika bajeti za sekta husika” ameongeza Bi. Janeth

 

Aidha, ameeleza kuwa, majukumu katika usimamizi wa maafa  yamegawanywa katika kongani 15 ambapo kila kongani ina jukumu mahsusi linalopaswa kuratibiwa na kutekelezwa na idara au taasisi yenye jukumu hilo kwa mujibu wa katiba, sheria, miongozo au miundo ya serikali iliyopo.

 


Kikao hicho kimewakutanisha mamlaka na taasisi mbalimbali zikiwemo TARURA, TANESCO, TANROADS, RUWASA, MUWSA, Bonde la Pangani, RED CROSS ambapo taasisi hizo zimewasilisha mada ya jinsi zilivyojipanga katika kukabiliana na madhara ya mvua hizo.



Share this

Related Posts

Latest
Previous
Next Post »