NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhandisi Hamad Yusuf Masauni, amezindua na kukabidhi magari matano kwa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), hatua inayolenga kuimarisha shughuli za ukaguzi, ufuatiliaji na upimaji wa mazingira nchini.
Magari hayo, yakiwemo Hard Top moja na Prado nne, yanatarajiwa kuongeza uwezo wa NEMC kufikisha huduma karibu na wananchi, kufanya ukaguzi kwa ufanisi na kushughulikia changamoto mbalimbali za kimazingira.
Masauni alizindua na kukabidhi magari hayo wakati wa ziara yake katika Ofisi za NEMC jijini Dar es Salaam, ambapo pia alipokea taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Baraza na kuipongeza Bodi ya Wakurugenzi kwa hatua zinazochukuliwa katika kusimamia na kuhifadhi mazingira.
Aidha, Masauni amepongeza utekelezaji wa shughuli za kimkakati za Baraza, ikiwemo uzinduzi wa Mfumo wa Ufuatiliaji wa Uchafuzi wa Mazingira (TOCEMS), maendeleo ya ujenzi wa Kituo cha Uelimishaji kuhusu Zebaki mkoani Geita na maandalizi ya ujenzi wa ofisi za kudumu za NEMC jijini Dodoma.
Amesema pia anapongeza hatua zinazoendelea za kulibadilisha NEMC kuwa Mamlaka ya Taifa ya Usimamizi wa Mazingira (NEMA), akisisitiza umuhimu wa kuendelea kuimarisha usimamizi wa mazingira kwa manufaa ya wananchi na maendeleo endelevu ya Taifa.
Akitoa taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Baraza, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya NEMC, Mhandisi Mwanasha Tumbo, amesema Baraza litaendelea kutekeleza majukumu yake kwa weledi na uwajibikaji, huku likiimarisha usimamizi wa mazingira na kushirikiana na wadau.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dkt. Immaculate Sware Semesi, amesema Baraza litaendelea kushirikiana na Serikali na wadau katika kuhakikisha mazingira yanalindwa na wananchi wanapata huduma bora.
Masauni ameitaka Menejimenti ya NEMC kuhakikisha magari hayo yanatumika kwa madhumuni yaliyokusudiwa, yanatunzwa vizuri na kugawanywa kulingana na mahitaji ya maeneo husika.

EmoticonEmoticon