Showing posts with label hab. Show all posts
Showing posts with label hab. Show all posts
BANDARI YA MBAMBA BAY KUCHOCHEA BIASHARA YA MIKOA YA KUSINI NA NCHI JIRANI

BANDARI YA MBAMBA BAY KUCHOCHEA BIASHARA YA MIKOA YA KUSINI NA NCHI JIRANI

November 21, 2026 Add Comment

Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, amesema Serikali itaendelea kusimamia kwa karibu ujenzi wa Bandari ya Mbamba Bay wilayani Nyasa, mkoani Ruvuma, ili ukamilike kwa wakati na viwango vinavyotakiwa kwa lengo la kukuza biashara na uchumi wa ukanda wa Kusini na nchi jirani za Malawi, Msumbiji na Zambia

Prof. Mbarawa amesema hayo wakati wa ziara yake ya kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayosimamiwa na Wizara ya Uchukuzi kwa kutembelea mradi wa ujenzi wa Bandari hiyo uliofikia asilimia 78 ya utekelezaji, ambao Serikali imewekeza Shilingi bil 75.85 na kusema kuwa bandari hiyo itakuwa na uwezo wa kuhudumia meli mbili zenye uzito wa tani 5,000 kila moja kwa wakati mmoja, hivyo kuongeza ufanisi wa usafirishaji wa mizigo kupitia Ziwa Nyasa na kukuza uchumi wa kikanda

Aidha, amesema Serikali inapitia ombi la kuongeza safari za ATCL kwenda Songea kutoka nne hadi tano kwa wiki, kulingana na mahitaji ya soko, pamoja na ombi la kuongeza vyombo vya usafiri katika Ziwa Nyasa na kumtaka mkandarasi kuzingatia usanifu na viwango vya kitaalamu ili kuhakikisha mradi unadumu na kutoa thamani ya fedha zilizowekezwa

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Brigedia Jenerali Ahmed Abbas , amesema bandari hiyo itachochea shughuli za kiuchumi, kuongeza ajira na kipato cha wananchi pamoja na mapato ya Serikali huku akiipongeza Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuimarisha miundombinu na kufungua fursa za kiuchumi mkoani humo ikiwa ni ahadi yake ya kuifanya Ruvuma kuwa kitovu cha uchumi wa kusini

Awali, Meneja wa mradi kutoka TPA, Mh. John Paul, amesema ujenzi wa Bandari ya Mbamba bay unatarajiwa kukamilika Februari 26, 2027 na kueleza kuwa miundombinu yake itajumuisha gati la mita 115, yadi yenye uwezo wa kuhifadhi makasha 4,000, jengo la abiria 400 na maghala matatu ambapo Kukamilika kwake kutarahisisha usafirishaji wa madini, mazao na bidhaa za viwandani na kuimarisha biashara kati ya Tanzania, Malawi, Msumbiji na Zambia.

NEMC YATAKIWA KUONGEZA UFANISI KATIKA UKAGUZI WA MAZINGIRA

September 18, 2026 Add Comment
NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhandisi Hamad Yusuf Masauni, amezindua na kukabidhi magari matano kwa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), hatua inayolenga kuimarisha shughuli za ukaguzi, ufuatiliaji na upimaji wa mazingira nchini.
TBS YABANA BIDHAA HATARISHI, YATAKA MAENEO YA BIASHARA YA CHAKULA NA VIPODOZI KUSAJILIWA

TBS YABANA BIDHAA HATARISHI, YATAKA MAENEO YA BIASHARA YA CHAKULA NA VIPODOZI KUSAJILIWA

August 17, 2026 Add Comment

Meneja wa Usajili wa Bidhaa na Majengo wa TBS, Bw.Habakuki Kalebo,akiwasilisha mada wakati wa kikao kilichoandaliwa na BRELA cha Maafisa Biashara pamoja na Wakuu wa Idara za Viwanda na Biashara kinachofanyika kwa siku mbili jijini Dodoma.

Na.Mwandishi Wetu-DODOMA 

Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limesisitiza umuhimu wa kusajili maeneo yote yanayohusika na uuzaji, usambazaji na uhifadhi wa bidhaa za chakula na vipodozi, likieleza kuwa hatua hiyo ni muhimu katika kuhakikisha wananchi wanapata bidhaa salama na bora, kulinda afya zao.

Meneja wa Usajili wa Bidhaa na Majengo wa TBS, Bw.Habakuki Kalebo, amesema hayo wakati wa kikao kilichoandaliwa na BRELA cha Maafisa Biashara pamoja na Wakuu wa Idara za Viwanda na Biashara, akieleza kuwa TBS inashirikiana na Ofisi ya Rais–TAMISEMI kupitia mamlaka za serikali za mitaa katika kusimamia usajili wa maeneo hayo.

Kalebo amesema usajili huo unalenga kuhakikisha bidhaa zinazouzwa, kusambazwa au kuhifadhiwa ni salama, bora na zimethibitishwa na TBS, huku mazingira yanayotumika kuhifadhi na kuuza bidhaa yamekidhi masharti ya usalama na usafi. Amesema kwa bidhaa za chakula, hatua hiyo inasaidia kuzuia uchafuzi kwa kuhakikisha chakula hakihifadhiwi au kuchanganywa na bidhaa nyingine zinazoweza kuhatarisha ubora wake.

Aidha, amesema usajili huo unasaidia kudhibiti usalama wa vipodozi vinavyoingizwa sokoni, kwa kuhakikisha havina viambata vyenye madhara kwa watumiaji. Ameongeza kuwa ukaguzi katika maeneo hayo pia husaidia kubaini na kuondoa bidhaa zilizomaliza muda wake kabla hazijawafikia wananchi, hivyo kupunguza hatari zinazoweza kujitokeza kutokana na matumizi ya bidhaa zisizofaa.

 "Mfumo wa usajili pia una umuhimu katika ufuatiliaji wa bidhaa sokoni, kwani pale changamoto inapojitokeza, TBS inaweza kubaini bidhaa husika zilipo, kiasi kilichopo na kuchukua hatua za haraka za kuziondoa sokoni. Amesema utaratibu huo unaimarisha udhibiti wa bidhaa na kuongeza uwezo wa Serikali kulinda afya na usalama wa wananchi."amesema Bw.Kalebo 

Amesema ushirikiano kati ya TBS, Maafisa Biashara na Mamlaka za serikali za mitaa ni muhimu katika kuhakikisha wafanyabiashara wanaelewa na kutekeleza matakwa ya Sheria na Viwango vya bidhaa. 

Kalebo amesisitiza kuwa ulinzi wa afya ya wananchi unapaswa kuwa sehemu muhimu ya usimamizi wa biashara, akieleza kuwa mtu mwenye afya njema ana uwezo mkubwa wa kushiriki katika shughuli za uzalishaji na kuchangia uchumi wa taifa.

Amesema matumizi ya bidhaa salama hupunguza hatari za magonjwa na gharama za matibabu, hivyo usajili na udhibiti wa maeneo ya biashara ya chakula na vipodozi ni hatua muhimu katika kulinda afya ya jamii na kuongeza tija ya Taifa.