Na Oscar Assenga, TANGA
MKUU wa Mkoa wa Tanga, Balozi Dkt. Batilda Burian, amewataka watumiaji wa barabara kuu ya Segera–Tanga kupanga safari zao mapema kufuatia kufungwa kwa barabara hiyo kwa muda wa saa nne kesho, Jumanne, ili kupisha ukarabati wa madaraja ya Hale na Maguzoni.
Burian alisema barabara hiyo itafungwa kuanzia saa mbili asubuhi hadi saa sita mchana, huku akiwataka madereva wa magari makubwa ya mizigo, wasafirishaji, wafanyabiashara na watumiaji wa magari madogo kuzingatia muda huo ili kuepuka usumbufu na msongamano wa magari.
Akizungumza na waandishi wa habari mkoani hapa, alisema hatua hiyo ni muhimu ili kumpa mkandarasi nafasi ya kufanya kazi za ukarabati wa madaraja hayo ambayo yamekuwepo kwa muda mrefu.
Alisema barabara ya Segera–Tanga ni kiungo muhimu cha shughuli za kiuchumi katika ukanda wa Afrika Mashariki, ikihudumia magari ya mizigo, magari ya mafuta na usafirishaji unaohusisha mikoa mbalimbali pamoja na nchi jirani.
“Tunawaomba wananchi, wafanyabiashara, wachukuzi na watumiaji wengine wa barabara hii kupanga safari zao mapema. Wanaweza kuanza safari baada ya saa sita mchana au kuondoka kabla ya saa mbili asubuhi ili kuepuka usumbufu,” alisema Burian.
Aliongeza kuwa madereva wanaotoka Arusha, Dar es Salaam na maeneo mengine wanapaswa kuzingatia taarifa hiyo, kwani watakapofika Segera katika muda ambao barabara imefungwa hawataweza kuendelea na safari kuelekea Tanga hadi kazi itakapokamilika.
Aidha, aliwataka wananchi ambao hawana ulazima wa kusafiri katika muda huo kuchelewesha safari zao ili kupunguza msongamano katika eneo la Segera.
Burian alisema ukarabati huo unahusisha madaraja ya Hale na Maguzoni, akieleza kuwa kazi hizo zimepangwa kufanyika wakati wa mchana ili kumwezesha mkandarasi kufanya kazi kwa ufanisi na katika mazingira salama.
Kwa upande wake, Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Tanga, Mhandisi Msama K. Msama alisema magari madogo yanaweza kutumia njia mbadala kupitia Maguzoni, Mnyuzi, Rwengera na Old Korogwe hadi Korogwe mjini.
Alisema pia vibao vya maelekezo vitawekwa katika maeneo ya Pongwe na Segera ili kuwasaidia madereva kufahamu maeneo ya vizuizi na kupanga safari zao.
Naye Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Almachius Muchunguzi, alisema Jeshi la Polisi litaweka askari katika maeneo ya Tanga na Segera kusimamia magari na kuzuia msongamano wakati wa utekelezaji wa kazi hizo.
Alivitaka vyombo vya usafiri na watumiaji wengine wa barabara kuzingatia maelekezo yatakayotolewa na mamlaka husika hadi barabara itakapofunguliwa tena.

EmoticonEmoticon