TAASISI ZASISITIZWA KUHAMIA KATIKA MATUMIZI YA NISHATI SAFI YA KUPIKIA

October 16, 2026


Morogoro,

Serikali imeendelea kuhamasisha taasisi mbalimbali nchini, zikiwemo shule, hospitali na taasisi nyingine zinazopika chakula kwa idadi kubwa ya watu, kuhamia katika matumizi ya nishati safi ya kupikia ili kupunguza athari za moshi kwa afya za wananchi na kuhifadhi mazingira.


 Mhandisi Amina Almas kutoka Wizara ya Nishati amezikumbusha taasisi kuhusu agizo hilo la Serikali wakati akiwasilisha mada kuhusu Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia wa mwaka 2024–2034 katika mafunzo ya viongozi wa Umoja wa Mama Lishe na Baba Lishe Tanzania (UMALITA), yaliyofanyika mkoani Morogoro.

Mhandisi Almas amesema kuwa, kati ya taasisi 30,000 zinazolengwa kuhamia katika matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini, tayari taasisi 1,472 zimeanza kutumia nishati hiyo, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mkakati huo unaolenga kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa mama lishe na baba lishe kutumia nishati safi ya kupikia katika shughuli zao za kila siku, akieleza kuwa matumizi ya nishati hiyo yanasaidia kupunguza athari za kiafya zinazotokana na moshi, kuokoa muda, kuongeza ufanisi katika shughuli za upishi pamoja na kuchochea fursa za ajira na biashara.

Katika mafunzo hayo, viongozi wa UMALITA pia wamepewa elimu kuhusu Mkakati wa Kitaifa wa Mawasiliano wa Nishati Safi ya Kupikia, unaolenga kuimarisha utoaji wa taarifa, elimu na uhamasishaji ili kuongeza matumizi ya nishati hiyo nchini.

Akiwasilisha mada kuhusu mkakati huo, Afisa Habari kutoka Wizara ya Nishati, Bi. Felista Mganga, amesema mkakati huo umeandaliwa na Wizara kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Mitaji la Umoja wa Mataifa (UNCDF), kwa ufadhili wa Umoja wa Ulaya (EU), na kuzinduliwa Juni 2, 2025, jijini Dodoma.

Amesema mkakati huo unaweka mwelekeo wa pamoja wa kufikisha elimu na taarifa kuhusu nishati safi ya kupikia kwa wananchi kupitia redio, televisheni, magazeti, mitandao ya kijamii, mikutano na maonesho.



Share this

Related Posts

Previous
Next Post »