Mawaziri wa nchi wanachama wa Umoja wa Afrika wapendekeza Rais Samia kutangazwa rasmiUmoja wa Afrika umetambua juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kuendeleza na kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia ndani na nje ya nchi, na kumpendekeza kutangazwa rasmi kuwa kinara wa Umoja wa Afrika wa ajenda hiyo.
Hatua hiyo imefikiwa katika Mkutano wa 5 wa Mawaziri wa Nchi wanachama wa Umoja wa Afrika wanaoshughulikia Nishati na Uchukuzi uliofanyika jijini Johannesburg, Afrika Kusini, tarehe 30 Aprili 2026. Katika mkutano huo Waziri wa Nishati, Mhe. Deogratius Ndejembi, ameongoza ujumbe wa Tanzania katika ngazi ya Mawaziri.
Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ametambuliwa na kupendekezwa kuwa kinara wa Afrika kutokana na mchango wake mkubwa katika kusukuma sera, mikakati na ushirikiano wa kimataifa unaolenga kupanua upatikanaji wa nishati safi ya kupikia, kupunguza athari za kiafya na kimazingira, pamoja na kuboresha maisha ya waafrika, hususan wanawake na watoto.
Akizungumza katika mjadala kuhusu Programu ya Nishati Safi ya Kupikia Afrika, Waziri Ndejembi amesema kuwa mafanikio ya Tanzania katika sekta hiyo yametokana na uongozi madhubuti wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kusukuma ajenda ya nishati safi ya kupikia ndani na nje ya nchi.
Amesema kuwa chini ya uongozi wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, nishati safi ya kupikia imepewa kipaumbele cha kitaifa na kuingizwa katika Dira ya Taifa ya 2050, ikiwa ni sehemu muhimu ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Katika juhudi za kimataifa, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ameendelea kuhamasisha agenda ya nishati safi ya kupikia kupewa kipaumbele katika mipango ya mataifa mbalimbali kupitia majukwaa ya kimataifa ikiwemo mkutano wa COP28 mwaka 2023, pamoja na Mkutano wa Nishati Safi ya Kupikia Barani Afrika uliofanyika Paris mwaka 2024, ambapo zaidi ya dola za Marekani bilioni 2.2 ziliahidiwa kusaidia sekta hiyo.
Kutokana na hatua hiyo ya mapendekezo ya Mawaziri yaliyoanzia katika ngazi ya wataalamu wa Umoja wa Afrika, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuthibitishwa na kutangazwa rasmi kuwa Kinara wa Umoja wa Afrika wa Nishati Safi ya Kupikia katika Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika utakaofanyika.








.jpg)
EmoticonEmoticon