Showing posts with label Nishati. Show all posts
Showing posts with label Nishati. Show all posts
SERIKALI YAFIKISHA UMEME KATIKA MAENEO 582 YA WACHIMBAJI WADOGO, KILIMO NA VIWANDA TANZANIA BARA

SERIKALI YAFIKISHA UMEME KATIKA MAENEO 582 YA WACHIMBAJI WADOGO, KILIMO NA VIWANDA TANZANIA BARA

September 02, 2026 Add Comment




Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Salome Makamba, amesema Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) imetekeleza Mradi wa Usambazaji Umeme katika maeneo 582 ya wachimbaji wadogo, kilimo na viwanda Tanzania Bara, kwa gharama ya Shilingi bilioni 115.

Mhe. Makamba ameyasema hayo leo Bungeni jijini Dodoma alipokuwa akijibu swali la Mhe. Mwanahamisi Athumani, Mbunge wa Viti Maalumu, aliyetaka kujua ni lini Serikali itatekeleza Mpango Mkakati Maalumu wa kuhakikisha maeneo ya wachimbaji wadogo yanafikishiwa umeme wa kutosha kwa lengo la kupunguza gharama za uzalishaji.



Akijibu swali hilo, Mhe. Makamba amesema kuwa mradi huo ulianza kutekelezwa Aprili, 2023 na kwa sasa umefikia hatua za mwisho za utekelezaji.

Aidha, amesema Wizara ya Nishati kwa kushirikiana na Wizara ya Madini inaendelea kuainisha maeneo ya kipaumbele yatakayofikishiwa huduma ya umeme katika hatua zinazofuata, kwa kuzingatia upatikanaji wa fedha.

Sambamba na hilo, Mhe. Makamba amesema Serikali kupitia TANESCO, kwa kutumia fedha za ndani, inaendelea kutekeleza miradi ya kuimarisha miundombinu ya usafirishaji na usambazaji wa umeme pamoja na ujenzi na uboreshaji wa vituo vya kupoza umeme katika mikoa mbalimbali nchini, hususan maeneo yenye changamoto ya low voltage.

Amesema hatua hizo ni sehemu ya juhudi za Serikali kuhakikisha maeneo yote ya uzalishaji yanafikiwa na huduma ya umeme ya kutosha na ya uhakika.

Mhe. Makamba amesisitiza kuwa lengo la Serikali ni kuhakikisha wachimbaji wadogo, wakulima, viwanda na maeneo mengine ya uzalishaji yanapata umeme wa kutosha na wa uhakika wakati wote, ili kupunguza gharama za uzalishaji, kuongeza tija na kuchochea ukuaji wa shughuli za kiuchumi nchini.   


TANESCO YABAINI MATUKIO YA WIZI WA UMEME KINONDONI KASKAZINI

September 02, 2026 Add Comment



NA MWANDISHI WETU - DAR ES SALAAM


Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limebaini matukio ya wizi wa umeme katika eneo la Visiwani, Mwananyamala na Mivumoni, zilizo Wilaya ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam, wakati wa operesheni ya ukaguzi wa mita na miundombinu ya umeme inayoendelea katika maeneo mbalimbali ya Mkoa huo.


Operesheni hiyo inalenga kudhibiti matumizi yasiyo halali ya umeme, kulinda miundombinu ya Shirika na kuhakikisha huduma ya umeme inaendelea kutolewa kwa usalama na ufanisi kwa wananchi.


Akizungumza wakati wa operesheni hiyo, Afisa Usalama wa TANESCO, Bi. Lilian Nizim, amewataka wananchi kuzingatia sheria na taratibu za matumizi ya umeme na kuepuka vitendo vya kuingilia au kuchezea mita za umeme.


“Mteja anapobaini changamoto yoyote inayohusiana na mita yake, anapaswa kutoa taarifa TANESCO ili ipatiwe ufumbuzi. Ni muhimu wananchi waepuke kabisa kuingilia mita kwa njia yoyote, kwani ni kinyume cha sheria na kunaweza kuhatarisha usalama wa maisha na mali,” amesema Bi. Nizim.

Kwa upande wake, Mhandisi wa TANESCO Mkoa wa Kinondoni Kaskazini, Mha. Underson Manyika, amesema wakati wa ukaguzi katika eneo la Visiwani, timu ya wataalamu ilibaini baadhi ya wateja wakiwa wamechepusha nyaya za umeme, hali iliyosababisha mita kutosoma matumizi halisi ya umeme.


“Ukaguzi wetu umebaini kuwepo kwa miunganisho isiyo halali iliyokuwa ikiathiri usomaji sahihi wa mita. Hatua stahiki zinaendelea kuchukuliwa kwa mujibu wa sheria na taratibu za Shirika,” amesema Mha. Manyika.

Amesema vitendo vya wizi wa umeme husababisha hasara kwa Shirika, kuhatarisha usalama wa wananchi na kuathiri ubora wa huduma ya umeme, hivyo ametoa wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana na TANESCO kwa kutoa taarifa za vitendo hivyo ili viweze kudhibitiwa kwa wakati.


TANESCO inaendelea kufanya ukaguzi wa mara kwa mara wa mita na miundombinu ya umeme katika maeneo mbalimbali nchini ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuimarisha utoaji wa huduma ya umeme ya uhakika, salama na endelevu kwa wananchi.



MHE. SALOME: WIZARA YA NISHATI INA WAJIBU WA KUHAKIKISHA WANANCHI WANAPATA UMEME WA UHAKIKA

September 01, 2026 Add Comment


Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Salome Makamba, amesema jukumu kuu la Wizara ya Nishati ni kuhakikisha wananchi wanapata umeme wa uhakika na wanapatiwa taarifa kwa wakati pindi changamoto zinapojitokeza.

Mhe. Makamba ameyasema hayo leo, tarehe 01 Septemba 2026, wakati akijibu Swali lanMhe. Exaud Silaoneka Kigahe, Mbunge wa Jimbo la Mufindi Kaskazini, aliyetaka kufahamu lini Serikali itabadilisha mkataba wa usambazaji wa umeme kwa wananchi kutoka Mwenga Power kwenda TANESCO, ili Mwenga Power ibaki kuwa mzalishaji wa umeme.

Akijibu swali hilo, Mhe. Makamba amesema utoaji na usimamizi wa leseni za uzalishaji na usambazaji wa umeme nchini ni jukumu la kisheria la Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA), kwa mujibu wa Sheria ya Umeme ya mwaka 2008 na taratibu za utoaji wa leseni hizo.

“Jukumu namba moja la Wizara ya Nishati ni kuhakikisha wananchi wanapata umeme wa uhakika na wanapata taarifa kwa wakati kunapotokea changamoto,” amesema Mhe. Makamba.

Ameeleza kuwa uamuzi wowote wa kubadili muundo wa leseni ya usambazaji umeme katika eneo hilo unapaswa kuzingatia matakwa ya sheria na taratibu zilizowekwa.

Hata hivyo, Mhe. Makamba amesema Serikali, kwa kutambua kuwa kumekuwa na malalamiko kuhusu ubora wa huduma inayotolewa na Mwenga Power, tayari taasisi zake za EWURA, TANESCO na REA zimeanza kufanya tathmini ya kina ili kubaini uwezekano wa kufanya mabadiliko hayo bila kuathiri uwekezaji uliopo.

Amesema tathmini hiyo itafanyika kwa haraka ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya umeme yenye uhakika na inayokidhi mahitaji yao.

Aidha, akihitimisha, Mhe. Makamba amesema yupo tayari, pindi Vikao vya Bunge vitakapokamilika, kuongozana na Mhe. Exaud Silaoneka Kigahe, Mbunge wa Jimbo la Mufindi Kaskazini, kwenda kusikiliza na kufahamu kwa kina changamoto zinazowakabili wananchi katika eneo hilo.

RAIS SAMIA AZINDUA RASMI KITUO CHA KUZALISHA UMEME CHA BWAWA LA JULIUS NYERERE

August 22, 2026 Add Comment



Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan amezindua rasmi Kituo cha Kuzalisha Umeme cha Julius Nyerere (JNHPP) chenye uwezo wa kuzalisha megawati 2,115 leo, tarehe 22 Agosti 2026, katika eneo la mradi lililopo Rufiji, mkoani Pwani.


Viongozi mbalimbali wameungana na Rais Samia katika uzinduzi huo, akiwemo Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi,Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba; Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Kiarabu ya Misri, Mhe. Moustafa Madbouly; Waziri wa Nishati, Mhe. Deogratius Ndejembi; pamoja na viongozi wengine.


Uzinduzi wa JNHPP ni kilele cha utekelezaji wa mradi mkubwa wa kimkakati uliotekelezwa kwa kutumia fedha za ndani za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mradi huo umegharimu takribani shilingi trilioni 7.452, sawa na dola za Marekani bilioni 3.35. Ujenzi wake ulianza Juni 2019 na kukamilika Machi 2025.


JNHPP imeongeza uwezo wa uzalishaji wa umeme nchini na kuimarisha usalama wa nishati. Kwa sasa, uwezo wa mitambo ya kuzalisha umeme nchini umefikia takribani megawati 4,075, ambapo JNHPP pekee inachangia zaidi ya nusu ya uwezo huo.












TANZANIA,RWANDA ZAKUBALIANA KUIMARISHA USHIRIKIANO KATIKA SEKTA YA MAFUTA

August 17, 2026 Add Comment




Waziri wa Nishati, Mhe. Deogratius Ndejembi, amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Biashara na Viwanda wa Jamhuri ya Rwanda, Mhe. Antoine Kajangwe, yaliyolenga kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Rwanda katika maendeleo ya sekta ya nishati, hususan katika sekta ndogo ya Mafuta.

Mawaziri hao wamekutana leo, tarehe 17 Agosti 2026, katika Ofisi za Wizara ya Nishati zilizopo katika Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma, ambapo wamejadili masuala mbalimbali yanayohusu ushirikiano kati ya Tanzania na Rwanda, hususan katika sekta ya mafuta.

Kikao hicho kimehudhuriwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati anayeshughulikia Mafuta na Gesi, Dkt. James Mataragio, Kamishna Mkuu (High Commissioner) wa Jamhuri ya Rwanda nchini Tanzania, Mhe. Jenerali Patrick Nyamvumba pamoja na Kamishna wa Mafuta na Gesi wa Wizara ya Nishati, Goodluck Shirima.