TRA KARIAKOO YASHIRIKI MKUTANO MKUU WA JWK, YASISITIZA UWASILISHAJI WA RITANI KWA WAKATI

April 25, 2026
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Kikodi Kariakoo imeshiriki kikamilifu katika Mkutano Mkuu wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Kariakoo (JWK) uliofanyika katika ukumbi wa soko la Kariakoo, jijini Dar es Salaam.

Timu ya TRA iliyoshiriki mkutano huo ilijumuisha Meneja wa Elimu kwa Mlipakodi, Bw. Paul Walalaze, Kaimu Meneja wa Mkoa, Bw. Edson Issanya, Kaimu Meneja wa Huduma kwa Mlipakodi, Bw. Fredrick Charles, pamoja na Meneja wa Ukaguzi (Audit), Bw. Liami Haule.

Katika mkutano huo, Bw. Paul Walalaze alipata nafasi ya kuzungumza kama mwakilishi rasmi wa TRA, ambapo aliwasilisha salamu za Kamishina Mkuu na kusisitiza umuhimu wa kuendeleza ushirikiano kati ya TRA na Jumuiya ya Wafanyabiashara wa Kariakoo.

“Tunashukuru kwa umoja huu na tuendelee kushirikiana kwa karibu. TRA imeanzisha Dawati la Uwezeshaji Biashara kwa ajili ya kushughulikia kodi za ndani pamoja na kodi za forodha, likiwa na lengo la kuwahudumia wafanyabiashara kwa ukaribu zaidi, hususani wafanyabiashara wa Kariakoo. Tunawahimiza kutumia fursa hii kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili,” alisema Bw. Walalaze.

Aidha, aliwashukuru wafanyabiashara kwa ushirikiano waliouonyesha katika mwaka 2025 na kusisitiza umuhimu wa kuwasilisha ritani kwa wakati, akiwahimiza kufanya hivyo kabla ya tarehe 1 Julai, 2026 ili kuepuka usumbufu usio wa lazima.

Pia alieleza juhudi zinazoendelea kufanywa na TRA katika kuboresha huduma za kodi, kuongeza uwazi, na kurahisisha mifumo ya ukusanyaji wa mapato ili kuwahudumia walipakodi kwa ufanisi zaidi, huku akihimiza uwajibikaji na ushirikiano kwa maendeleo endelevu.

Wajumbe wa mkutano huo walipokea mawasilisho hayo kwa uzito na kuvutiwa, wakionesha kuthamini mchango wa TRA pamoja na uwakilishi thabiti wa timu hiyo.

Share this

Related Posts

Latest
Previous
Next Post »