Wito huo umetolewa leo Aprili 23, 2026 jijini Dar es Salaam na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano), Deus Sangu wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maadhimisho ya Siku ya Usalama na Afya Mahala pa Kazi Duniani.
Amesema maadhimisho hayo kitaifa yatafanyika Aprili 28, 2026 mkoani Njombe, yakilenga kuongeza uelewa kuhusu umuhimu wa usalama na afya kazini.
Akitoa takwimu za kimataifa, Sangu amesema ripoti ya International Labour Organization (ILO) ya mwaka 2022 inaonesha kuwa zaidi ya wafanyakazi milioni 970 duniani wanakabiliwa na matatizo ya afya ya akili yanayohusiana na kazi.
Ameongeza kuwa kwa mujibu wa International Labour Organization kwa kushirikiana na World Health Organization (WHO), changamoto hizo zimeongezeka na kusababisha hasara kubwa ya kiuchumi inayokadiriwa kufikia zaidi ya dola trilioni moja kila mwaka.
Kwa upande wa usimamizi wa mifumo ya usalama na afya kazini, amesema vihatarishi vya kisaikolojia vinapaswa kupewa uzito sawa na vihatarishi vya kimwili kutokana na athari zake kwa ajali, magonjwa na utendaji wa taasisi.
“Vihatarishi hivi hutokana na namna kazi inavyobuniwa, kusimamiwa pamoja na mazingira ya kijamii ya mahali pa kazi. Athari zake hujikita zaidi katika afya ya akili lakini pia huathiri usalama, tija na ustawi wa wafanyakazi,” amesema.
Akizungumzia takwimu za ajali kazini, amesema kwa mujibu wa ILO, takribani wafanyakazi milioni tatu hufariki kila mwaka duniani kutokana na ajali na magonjwa yatokanayo na kazi, huku milioni 395 wakipata majeraha kila mwaka.
Kwa upande wa Tanzania, amesema ajali zilizoripotiwa katika kipindi cha Julai 2023 hadi Juni 2025 zimefikia 3,557, ambapo kati ya hizo vifo ni 169.
Kuhusu maadhimisho ya mwaka huu, Serikali kwa kushirikiana na wadau itaendesha kampeni maalum za uhamasishaji kupitia mafunzo kwa makundi mbalimbali, ikiwemo wajasiriamali wadogo.
Aidha, kutakuwa na utoaji wa Tuzo za Usalama na Afya Kazini (OSHA 2026) kwa waajiri wanaotekeleza vyema Sheria ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi, Sura Na. 297 Toleo la 2023.
Mbali na hilo, wananchi wamealikwa kushiriki kikamilifu katika maadhimisho hayo yatakayofanyika kuanzia Aprili 24 hadi 29, 2026 katika viwanja vya Saba Saba Grounds, ambapo pia kutakuwa na huduma za uchunguzi na matibabu zinazotolewa na madaktari bingwa kutoka hospitali mbalimbali nchini.
EmoticonEmoticon