TANZANIA NA JAPAN KUFUNGUA MILANGO MIPYA YA UWEKEZAJI KATIKA SEKTA YA NISHATI

April 30, 2026


Ushirikiano kati ya Tanzania na Japan katika sekta ya nishati unaingia hatua mpya, huku juhudi zikielekezwa zaidi katika kuvutia uwekezaji wa sekta binafsi na teknolojia za kisasa za uzalishaji umeme.

Hatua hiyo imebainishwa jijini Dar es Salaam leo tarehe 30 Aprili,2026 wakati Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati anayeshughulikia Mafuta na Gesi Asilia,Dkt.  James Mataragio alipokutana na Mwakilishi Mkuu mpya wa Japan International Cooperation Agency, Dkt. Kuge Katsuya.

Katika kikao hicho Dkt. Mataragio ameweka wazi Mkakati wa Serikali kuifanya sekta ya nishati kuwa kivutio kikubwa cha mitaji ya kimataifa hususan kutoka Japan.

Amesema  kuwa pamoja na historia ndefu ya ushirikiano kati ya nchi hizo mbili, hatua inayofuata inapaswa kulenga uwekezaji mkubwa zaidi unaoweza kuongeza uzalishaji na upatikanaji wa nishati nchini.

“Huu ni wakati wa kuhamasisha kampuni binafsi na taasisi za kifedha kutoka Japan kuja kuwekeza moja kwa moja katika miradi ya nishati Tanzania,” amesisitiza.

Akizungumzia ushirikiano wa Tanzania na Japan Dkt. Mataragio amesema JICA imekuwa mdau wa muda mrefu katika sekta ya nishati nchini na wameshiriki katika miradi ya  Uandaaji wa Mpango kabambe wa Matumizi ya Gesi Asilia Nchini (Natural Gas Utilization Master Plan -NGUMP),  wametoa fursa za kuwajengea uwezo wataalamu katika Matumizi ya gesi asili pamoja na utekelezaji wa Miradi mbalimbali ya umeme.

Aidha Dkt. Mataragio amembushia ahadi ya muda mrefu ya Japan ya kuwezesha Mradi wa umeme wa megawati 300 mkoani Mtwara.

Kwa upande wake, Dkt. Kuge ameashiria mwelekeo mpya wa ushirikiano utakaojikita katika Mafunzo ya teknolojia ya nishati ya nyuklia, Uzalishaji wa umeme kupitia gesi asilia kwa ufanisi mkubwa zaidi na Kuunganisha Tanzania na wawekezaji binafsi kutoka Japan

Ahadi hiyo inaashiria uwezekano wa Tanzania kunufaika na teknolojia za kisasa zaidi za nishati kutoka Japan, moja ya nchi zinazoongoza duniani katika ubunifu wa nishati.

Mkutano huo umeonesha wazi kuwa ushirikiano kati ya Tanzania na Japan hauishii katika misaada, bali sasa unaelekea kwenye uwekezaji mkubwa na ubadilishanaji wa teknolojia  hatua inayoweza kubadilisha kabisa sekta ya nishati nchini

Share this

Related Posts

Latest
Previous
Next Post »