Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) na Mamlaka ya Usimamizi wa Mazingira Zanzibar (ZEMA) wamekutana Aprili 27,2026 katika ziara ya mafunzo, kwa lengo la kubadilishana uzoefu katika utekelezaji wa majukumu ya kimazingira, hasa mchakato wa ufanyaji wa Tathmini ya Athari kwa Mazingira na jamii katika miradi mikubwa na mchakato wa kupata vyeti vya kimazingira ili kuhakikisha maendeleo yanaendana na uhifadhi wa mazingira.
Akizungumza kwenye ziara hiyo, iliyohusisha wajumbe wa Bodi pamoja na Menejimenti ya pande zote mbili, Mwenyekiti wa Bodi ya NEMC, Mhandisi Mwanasha Tumbo, alisema Bara na Visiwani ni wamoja na hasa ikizingatiwa suala la mazingira ni mtambuka linalohitaji ushirikiano wa karibu kati ya pande zote mbili hatuna budi kutekeleza kwani mashirikiano katika sekta ya mazingira ni muhimu na kwakuwa limepewa kipaumbele katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayolenga kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi na kuhakikisha mazingira yanasimamiwa na kuhifadhiwa kwa ufanisi.
Naye Mwenyekiti wa Bodi kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Mazingira Zanzibar (ZEMA) Bi. Asha Ali Khatib alipozungumza alisema ni muhimu masuala ya mchakato wa ufanyaji wa Tathmini ya Athari kwa Mazingira kuzingatiwa na wawekezaji kuanzia hatua za awali hadi kukamilika kwa miradi ili kulinda mazingira huku akisistiza umuhimu wa kuimarisha ushirikishwaji wa jamii pamoja na matumizi ya teknolojia za kisasa ili kuhakikisha usimamizi na uhifadhi wa mazingira unafanyika kwa ufanisi.
Katika ziara hiyo, washiriki pia walipata wasilisho la kina kuhusu mchakato wa Tathmini ya athari kwa mazingira na jamii, mafanikio yaliyopatikana pamoja na changamoto zinazojitokeza katika utekelezaji wake kwa pande zote mbili yaliyotoa fursa ya majadiliano yenye kujenga kwa maendeleo endelevu ya mazingira.
Aidha, wajumbe hao walitembelea maeneo ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa Bandari ya Mpigaduri pamoja na Hoteli ya Verde iliyofanyiwa ufukiaji (reclamation) hali iliyowasaidia washiriki kuona kwa karibu jinsi tathmini za mazingira zinavyotekelezwa katika miradi mikubwa na umuhimu wake katika kulinda rasilimali za asili.
Ziara hii ni kufuatia makubaliano ya awali yaliyowakutanisha katika kikao cha Tarehe 08/10/2025 chenye maazimio ya kuimarisha mashirikiano katika sekta ya Uhifdhi na Usimamizi wa Mazingira.













EmoticonEmoticon