NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
Kikundi cha We Are Family kinachowahusisha wenza wa majaji nchini, kimetembelea wagonjwa wa saratani katika Ocean Road Cancer Institute jijini Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa dhamira yao ya kufanya matendo ya huruma kwa jamii.
Kikundi hicho chenye wanachama 59 waliosajiliwa, kimeeleza kuwa pamoja na shughuli nyingine, pia kinalenga kuwafikia wenza wa majaji wastaafu na waliopo kazini kwa lengo la kuimarisha mshikamano na kusaidiana katika masuala ya kijamii.
Akizungumza Aprili 26, 2026, Makamu Mwenyekiti wa kikundi hicho, Edivije Nangela, amesema uamuzi wa kutembelea wagonjwa wa saratani ulifikiwa baada ya kufanya tathmini na kufuata taratibu zote muhimu zilizowezesha kuwafikia wahitaji hao.
Amebainisha kuwa, licha ya kulenga kuwafikia wagonjwa 100, wamefanikiwa kuwafikia wagonjwa 39 pekee, hali inayodhihirisha ukubwa wa uhitaji uliopo pamoja na changamoto ya gharama kubwa za matibabu.
“Uhitaji ni mkubwa sana na gharama za matibabu ni kubwa, hivyo kuna umuhimu wa kuendelea kuweka mikakati ya kuwafikia watu wengi zaidi,” amesema Nangela.
Ameongeza kuwa kikundi hicho kinatarajia kufanya kikao maalum kitakacholenga kuweka mikakati endelevu ya kusaidia makundi mbalimbali yenye uhitaji katika jamii.
Kwa upande wake, Mratibu wa Matukio wa kikundi hicho, Beatrice Mdemu, amesema zoezi hilo litakuwa endelevu na kuwahimiza wenza wengine wa majaji kujiunga na kikundi hicho ili kuongeza nguvu katika kufanikisha malengo yao ya kijamii.
Naye Afisa wa Ocean Road Cancer Institute, Karafuu Ally, kwa niaba ya uongozi wa taasisi hiyo, amekishukuru kikundi hicho kwa kutembelea wagonjwa na kutoa faraja, akisisitiza umuhimu wa kuendeleza moyo wa kujitolea kwa jamii.
EmoticonEmoticon