WAHITIMU MZUMBE WATAKIWA KUJENGA MITANDAO IMARA YA UHUSIANO WA KITAALUMA

December 04, 2025
NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

WAHITIMU wa Chuo Kikuu Mzumbe Ndaki ya Dar es Salaam wametakiwa kujenga mitandao imara ya Uhusiano wa kitaaluma ili fursa zaidi ziweze kuwafikia kuliko kusubiri Chuo kiwatafutie.

Ameyasema hayo leo Desemba 04,2025 Jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Chuo hicho, Rais Mstaafu wa Zanzibar na Mwenyekiti Mstaafu wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein, wakati wa mahafali ya 24 ya Chuo hicho Ndaki ya Dar es Salaam ambayo yamefanyika Mlimani City Jijini Dar es Salaam.

Amesema kuna baadhi ya wanafunzi wa somo la Sheria walipata fursa ya kushiriki katika mashindano ya Mahakama Igizi ambayo ni mashindano ya Kimataifa ya Usuluhishi wa migogoro ya kibiashara yaliyofanyika Vienna Austria.

"Mashindano ya namna hii ambayo yanakusanya wanafunzi kutoka vyuo mbalimbali duniani ni nafasi nzuri ya kujifunza mambo kadhaa ya kitaaluma, kitaalamu, mila na utamaduni". Amesema

"Ni nafasi inayokuwezesheni wanafunzi kuunda mitandao ya Uhusiano katika nyanja zenu za elimu". Amesema

Kuhusu tatizo la wanafunzi wa somo la sheria kutopata nafasi za kufanyia mazoezi kwenye taasisi, amesema inabidi Chuo kifanye utafiti japo mdogo wa kutambua kiini cha tatizo hilo.

"Kama itahitaji wanafunzi wetu wawahi kabla ya nafasi hazijajazwa na wanafunzi kutoka sehemu nyingine, tuweze kurekebisha ratiba zetu". Amesema

Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Prof. William Mwegoha amesema kwa sasa Chuo Kikuu Mzumbe Ndaki ya Dar es salaam ina jumla ya wanafunzi 1793, ambapo wa Shahada ya Umahiri ni 1027 na 766 ni wa Shahada ya Awali.

Amesema Wanafunzi wakiume ni 854 sawa na asilimia 47.6 na wanawake ni 939 sawa na asilimia 52.4 kwa mantiki hii muitikio wa wanafunzi wa kike kujiendeleza kielimu ni mkubwa.

Aidha amesema kuwa Ndaki ya Dar es Salaam imekuwa mstari wa mbele katika kutoa huduma kwa jamii “outreach service” imeendesha semina mbalimbali baadhi ya huduma hizo ni pamoja na semina ya kuwajengea uelewa wanawake zaidi ya 200 wa mtaa wa Tegeta jinsi ya kutumia Baraza la Usuluhishi la Kata katika kutatua migogoro ya ndoa, Jinsi ya kutunza hesabu na kutafuta masoko kwa wafanyabiashara wa Ice Cream za azam kwa Matawi ya magomeni, Kingamboni na Chanika.

Vilevile amesema Ndaki imeendelea kuwajengea uwezo wahitimu wa vyuo Vikuu na vya kati Tanzania ili waweze kujua mbinu za kushiriki katika usajili mbalimbali, imetoa elimu ya matumizi ya Maktaba Mtandao kwa Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Kijitonyama Sayansi.

Huduma zote hizo zimefanywa bure na wafanyakazi wa Ndaki ya Dar es Salaam.

Kwa upande wa miundombinu, amesema Chuo kimekuwa kikiendelea kuboresha miundombinu mbalimbali ya kujisomea, kujifunzia na utendaji kazi, ikiwemo mifumo ya TEHAMA na miundombinu yake, ujenzi wa viwanja vya michezo Tegeta, ukarabati wa majengo ya Ndaki eneo la Upanga pamoja na ujenzi wa vimbweta eneo la Tegeta umekamilika.

"Lakini pia miradi mbalimbali ya maendeleo kwa kutumia fedha zilizotolewa na Serikali pamoja na mapato ya ndani, tumefanikiwa kuanza ujenzi wa jengo la taaluma katika Ndaki ya Dar es Salaam kituo cha Tegeta, jengo ambalo litakuwa na madarasa na ofisi lenye thamani ya shilingi bilioni 4.8, ujenzi umefikia asilimia 15". Amesema 

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »