VIJANA WAASWA KUTAFUTA FURSA KWENYE KILIMO CHA KIENYEJI

October 18, 2024

 Na Linda Akyoo -Moshi


Katika juhudi za kukuza kilimo cha kienyeji na endelevu,Taasisi ya Vijana Yenye Uwezo (TYC) iliandaa tukio la utoaji mafunzo kwa vijana kuhusu kilimo salama na rafiki wa mazingira.Tukio hilo lilifanyika Wilaya ya Moshi Mkoani Kilimanjaro,ambapo vijana wengi walihudhuria kwa lengo la kujifunza njia bora za kilimo ambazo zinazingatia mazingira.

Akizungumza Mkurugenzi wa Taasisi ya TYC,Bi Josephine Onesmo amesema kuwa mafunzo hayo yalilenga kuwajengea vijana uwezo wa kuanzisha na kuendesha miradi ya kilimo endelevu inayoheshimu mazingira,kupunguza matumizi ya dawa za kemikali na kuongeza tija katika uzalishaji wa mazao.

Aidha Bi.Josephine amesema kuwa vijana walijifunza mbinu za kilimo cha asili kama vile matumizi ya mbolea za asili, kudhibiti wadudu kwa njia ya asili, na umuhimu wa kutunza udongo ili kuepuka uharibifu wa mazingira.

Sambamba na hilo wakufunzi walioshiriki katika tukio hilo walitoa mifano halisi na mafunzo ya vitendo ili vijana waweze kuelewa na kutekeleza mbinu hizo kwa ufanisi. Vijana pia walipata fursa ya kutembelea mashamba ya mfano ambayo yalikuwa yanatumia mbinu hizo za kilimo salama na rafiki wa mazingira.

Kwa upande wao vijana waliohudhuria mafunzo hayo walihamasika na walikuwa tayari kuanza kutekeleza maarifa waliyopata katika kilimo chao. Walionyesha azma ya kutumia njia bora za kilimo kwa lengo la kulinda mazingira na kuongeza uzalishaji wa mazao yao.

Hata hivyo tukio hilo lilikuwa ni mwanzo wa safari ya vijana hao kuelekea kwenye kilimo endelevu,walikuwa na matumaini makubwa ya kufanikiwa katika jitihada zao za kilimo salama na rafiki wa mazingira.

Afisa Maendeleo vijana Wilaya ya Hai amewatoa hofu vijana wanaotaka kufanya shughuli za ujasiriamali, kilimo pamoja ufugaji wasisite kuanzisha shughuli zao kwani Serikali ya awamu ya sita chini ya uwongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan wametoa mikopo ya Halmshauri zote nchini ili kuwawezesha vijana, akina mama, na watu wenye ulemavu kunufaika na mikopo hiyo.

TYC ilionyesha dhamira yake ya kuwajengea vijana uwezo wa kujitegemea kiuchumi na kuwa mawakala wa mabadiliko katika sekta ya kilimo.





Share this

Related Posts

Previous
Next Post »