TANZANIA YAIPONGEZA NORWAY KWA KUENDELEA KUUNGA MKONO MAENDELEO

October 05, 2025

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo, ameipongeza Serikali ya Ufalme wa Norway kwa mchango wake mkubwa katika kuunga mkono juhudi za maendeleo ya Tanzania katika sekta za nishati, elimu, kilimo, na usimamizi wa fedha za umma.


Akizungumza kando ya Mkutano wa 22 wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Nchi za Afrika na nchi za Nordic uliofanyika mjini Victoria Falls, Zimbabwe, tarehe 2–3 Oktoba 2025, Mhe. Kombo alisema kuwa Norway imekuwa mshirika wa mfano katika kusaidia utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) na Ajenda ya 2030 kupitia miradi mbalimbali ya kimkakati nchini.

Mhe. Kombo alisema tangu mwaka 2010, Serikali ya Norway imechangia zaidi ya kronor bilioni 1.1, sawa na shilingi bilioni 300, kusaidia sekta muhimu zikiwemo nishati vijijini, elimu, mafuta na gesi, mabadiliko ya tabianchi, na usimamizi wa misitu. Alisisitiza kuwa msaada huo umechangia kuboresha huduma na kukuza uchumi wa wananchi wa Tanzania.

“Serikali ya Tanzania inatambua na kuthamini mchango mkubwa wa Norway katika kusaidia miradi ya maendeleo nchini, hususan katika nishati vijijini kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA), uwezeshaji wa wanawake wahandisi, na uwekezaji wa kampuni ya Equinor katika gesi asilia,” alisema Mhe. Kombo.


Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Norway, Mhe. Espen Barth Eide, alieleza kuwa nchi yake itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kukuza teknolojia ya nishati safi, elimu bora, na uwekezaji unaolenga kukuza uchumi wa kijani. Alisema Norway inaamini katika ushirikiano wa muda mrefu unaojengwa katika misingi ya uwazi, usawa na maendeleo endelevu.

Mhe. Kombo alihitimisha kwa kusema kuwa Tanzania itaendelea kudumisha uhusiano wa kihistoria na Norway, huku ikiahidi kuweka mazingira bora ya uwekezaji na ushirikiano wa kimaendeleo kwa manufaa ya wananchi wa mataifa yote mawili.

Share this

Related Posts

Latest
Previous
Next Post »