*📌RC Tanga aipa kongole REA kuuza majiko ya gesi kwa bei ya ruzuku*
*📌Majiko ya gesi 500 kuuzwa kwa bei ya ruzuku katika Maadhimisho ya Wiki ya Chakula*
*📌REA imetoa mkopo nafuu wa uwezeshaji wa ujenzi na uendeshaji vituo vidogo vya Petroli na Dizeli Vijijini*
📍Tanga
Mkuu wa mkoa wa Tanga, Mhe. Balozi. Dkt. Batilda Buriani ameipongeza Wakala wa Nishati Vijijini (REA), kwa kuuuza majiko ya gesi ya kilo 6 kwa bei ya ruzuku (ya shilingi 17500) ili wananchi waweze kutumia nishati safi na salama hapa nchini.
RC Buriani amesema hayo leo Oktoba 11, 2025 wakati wa ufunguzi wa Maadhimisho ya Wiki ya Chakula Duniani 2025 ambayo kitaifa yamefanyika katika viwanja vya shule ya Msingi Usagara jijini Tanga.
Aidha, amewaasa wananchi wanaoshiriki maadhimisho hayo kutumia fursa ya uwepo wa REA kuhakikisha wanachangamkia fursa hiyo ya majiko ya gesi kwa bei ya ruzuku.
Kwa upande wake, Mhandisi wa Miradi kutoka REA, Ramadhani Mganga amesema katika maadhimisho hayo REA inatarajia kuuza majiko ya gesi ya kupikia ya kilo sita 500 ili watanzania watumie nishati safi na salama.
Vile vile, REA inatumia fursa hiyo kueleza fursa mbalimbali zilizopo REA ikiwemo mkopo nafuu wa uwezeshaji wa ujenzi na uendeshaji wa vituo vidogo vya bidhaa za mafuta (Petroli na Dizeli) maeneo ya vijijini.
Ushiriki wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) katika maadhimisho hayo ni muhimu katika mpango mahsusi wa kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia ili kuhakikisha kila kaya na taasisi zinazohudumia watu zaidi ya 100 zinatumia nishati safi na salama.
EmoticonEmoticon