SERIKALI KUPITIA BENKI YA NMB KUTOA MIKOPO YA BILIONI 18.5 KWA WAFANYABIASHARA NDOGONDOGO NCHINI

October 18, 2024


Pamela Mollel,Arusha

Wafanyabiashara ndogondogo nchini wanatarajia kuanza kunufaika na mikopo kutoka mfuko wa uwezeshaji uliotengwa na serikali yenye thamani ya Sh18.5 Bilioni kupitia kwenye benki ya NMB.

Wafanyabiashara hao wanatarajia kuanza kunufaika na mikopo hiyo yenye riba ya asilimia saba pekee kupitia benki ya NMB iliyoingia makubaliano na serikali ya kuratibu fedha hizo kwa kutumia dhamana ya kitambulisho cha kielekroniki kitakachowatambulisha.

Vitambulisho hivyo vilivyozinduliwa ugawaji wake leo Octoba 17,2024 jijini Arusha na Waziri wa maendeleo ya jamii, jinsia, wanawake na makundi maalum, Dk Dorothy Gwajima vinalenga kuwatambua, kuwasajili na kuwapatia vitambulisho wafanyabiashara ndogondogo nchini.

Wafanyabiashara walengwa ni pamoja na machinja, mama na baba ntilie, waendesha boda boda, daladala, guta, sambamba na wasusi na vinyozi pia wajasiriamali wadogo wadogo.

Akizungumza katika Uzinduzi wa vitambulisho hivyo, Dk. Gwajima alisema kuwa serikali imetenga jumla ya Sh18.5 Bilioni kwa ajili ya kuwapatia wafanyabiashara hao mitaji Ili kuwakuza kiuchumi wao binafsi na Taifa kwa ujumla.

" Tumesaini mkataba wa ushirikiano wa benki ya NMB kwa ajili ya kupitisha na kuratibu fedha hizo ambazo wafanyabiashara wote wenye vitambulisho hivi vya kielekroniki wataweza kutumia kama dhamana kwa ajili ya kupata mikopo huo" alisema Gwajima.

Alisema kuwa kitambulisho hicho cha miaka mitatu vitaanza kugaiwa kwa wafanyabiashara ndogondogo walioweza kujisajili kupitia fomu maalum kutoka kwa Mtendaji wa kata itakayojazwa taarifa binafsi ikiwemo namba za NIDA na namba za simu pamoja na makazi kwa gharama ya Shilingi 20,000 tu.

"Matarajio ya Rais ni kuona fedha hii inakuwa endelevu na kuwafikia wafanyabiashara ndogondogo wengi zaidi, na sio kuona watu wanakopa na kushindwa kurejesha fedha waliyokopeshwa, na kuwanyima wengine fursa ya kukopa na kuboresha biashara zao,” alisisitiza.

Nae Katibu Mkuu mwenye dhamana ya Maendeleo ya Jamii, Dk. Seif Shekalaghe, aliwataka wafanyabiashara ndogondogo kuchangamkia fursa ya kujisajili kupata vitambulisho hivyo na kukopa fedha za mfuko huo kwa malengo ya kukuza biashara zao na kurejesha kwa wakati Ili kuwezesha na wengine kupata fursa zaidi.

Pia aliipongeza benki ya NMB kwa kuingia makubaliano hayo na serikali baada ya kushinda zabuni ya kuomba kupitishwa kwa mikopo hiyo kwao.

“Mchakato wa kupata benki ya kufanya nayo kazi ulikuwa na ushindani mkubwa, lakini hatimaye NMB ilishinda zabuni hii kati ya wote waliioomba, tunatarajia watafanya kazi kubwa kwa uzoefu wao na kuleta Tija ya fedha hizo kwa walengwa ambao ni wafanyabiashara ndogondogo" alisema Katibu mkuu huyo.

Kwa upande wake, Alex Mgeni aliyemwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa benki ya NMB, aliishukuru Serikali kwa kuichagua taasisi hiyo kupitisha fedha hizo kwa miaka miwili na kuahidi kutendea haki fedha hizo kutokana na uzoefu wa kutosha waliyonayo ya kuwahudumia wafanyabiashara ndogondogo.

“NMB ina uzoefu mkubwa wa kuwahudumia wafanyabiashara ndogondogo, ambao tangu mwaka 2020 hadi 2023, imetoa mikopo 129,540 yenye thamani ya Sh 2.03 Trilioni kwa wajasiliamali wadogo wadogo wakiwemo machinga na bodaboda, kwa wastani wa mikopo 2,699 kila mwezi sawa na Sh 42.3 Bilioni kwa mwezi" alisema

Alibainisha ya kwamba mikopo hiyo yenye riba ya asilimia saba pekee itakopeshwa kwa wafanyabiashara ndogo ndogo waliosajiliwa na kupewa vitambulisho hivyo hadi Sh 10 million.

Alisema kabla ya kuidhinisha mikopo, benki hiyo ya NMB itajiridhisha kwa kuwatembelea katika maeneo yao ili kuhakikisha mikopo hii inawafikia walengwa na kupatiwa Elimu ya kifedha Ili kuepuka baadhi kushindwa kulipa baadae.

Mbali na hilo alisema Benki yao inaendelea kubuni masuluhisho mbalimbali ya kifedha kwa ajili ya kuwafikia makundi mengi zaidi na kuwa msaada kwao hasa wa kifedha, bima na uchumi pia.

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda amewataka wafanyabiashara hao kuchangamkia fursa ya vitambulisho hivyo na kuwa na nidhamu ya fedha Ili kuweza kuwainua kiuchumi.

Katibu Mkuu wa shirikisho la umoja wa wamachinga Tanzania (Shiuma), Venatus Anatory alisema kupitia vitambulisho hivyo vya kielekroniki viliyounganishwa na taarifa za NIDA na mifumo ya kibenki itawasaidia kupata fursa nyingi za kukuza uchumi wao ikiwemo mikopo yenye riba nafuu.


Waziri mwenye dhamana ya maendeleo ya jamii, Dr Dorothy Gwajima (kulia) akimsikiliza Mkuu wa kitengo cha bima kutoka benki ya NMB , Martin Masawe juu ya huduma za mikopo kwa wafanyabiashara wakati alipotembelea mabanda katika Uzinduzi wa ugawaji wa vitambulisho vya wafanyabiashara ndogondogo uliofanyika Leo Octoba 17,2024,Jijini Arusha, ikumbukwe benki ya NMB imeingia makubaliano na serikali ya kupitisha fedha sh18.5 Bilioni kwa ajili ya kuwakopesha wafanyabiashara ndogondogo,

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »