Balozi wa Uturuki nchini Tanzania Dkt. Mehmet Gulluoglu leo Februari 01, 2024 amekutana na kufanya mazungumzo na Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa katika Ofisi za Wizara hiyo zilizopo katika Mji wa Serikali Mtumba Jijini Dodoma ambapo wamejadiliana juu ya namna ambavyo uhusiano wa kidiplomasia uliopo utazinufaisha nchi zote mbili katika sekta za Utamaduni, Sanaa na Michezo.
Akizungumza baada ya majadiliano hayo, Katibu Mkuu Msigwa amesema yapo matumaini makubwa kwa nchi hizo mbili kufungua fursa mbalimbali zinazogusa sekta hizo ikiwemo Wataalam wa lugha ya Kiswahili kufundisha lugha hiyo nchini humo, kujenga kituo kikubwa cha utamaduni pamoja na kuendeleza miundombinu ya michezo hapa nchini Tanzania.
“Kubwa ambacho Serikali ya Uturuki wako tayari ni kujenga Kituo cha Utamaduni hapa Tanzania ili kutangaza tamaduni za pande zote mbili, kuziendeleza na pia kutumia utamaduni kama fursa ya kiuchumi. Makubaliano yakikamilika wako tayari kuanza na ujenzi wa kituo hicho”, amesema Katibu Mkuu Gerson Msigwa.
Aidha, Katibu Mkuu Msigwa amesema Serikali ya nchi hiyo iko tayari kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika Sekta ya Sanaa ambapo Wasanii wa Filamu kutoka nchini Tanzania watapata fursa ya kutembelea nchi hiyo kujifunza zaidi kuhusiana na sekta hiyo na pia wasanii wa filamu wa nchi hiyo kutembelea Tanzania ili kubadilishana uzoefu.
Kwa upande wa sekta ya michezo Msigwa amesema Serikali ya Uturuki imeonesha nia ya kutoa nafasi kwa timu za Taifa kuweka kambi katika nchi hiyo wakati wakati wa maandalizi ya michuano mbalimbali ya kimataifa.
EmoticonEmoticon