Na Mwandishi Wetu
Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Salome Makamba, ameshiriki katika mdahalo wa Mawaziri kuhusu uwekezaji na uimarishaji wa ushirikiano wa kimataifa katika sekta ya mafuta na gesi, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Nishati ya India (India Energy Week – IEW 2026) yanayoendelea kufanyika Goa, India.
Akizungumza katika mdahalo huo uliofanyika leo Januari 28, 2026, Mhe. Makamba ameeleza kuwa Tanzania inaendelea kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji kwa kuzingatia fursa mbalimbali zilizopo katika sekta ya mafuta na gesi.
Amebainisha kuwa tafiti za kuchukua taarifa za mitetemo zinaendelea kufanyika katika vitalu vya Eyasi–Wembere, Lindi na Mtwara, sambamba na kukamilisha majadiliano na wawekezaji mbalimbali kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mikubwa ikiwemo Mradi wa Gesi Asilia Kimiminika (LNG).
Aidha, amesema Serikali inaendelea kuwekeza katika miradi ya usambazaji wa gesi kwa matumizi ya viwandani, uzalishaji wa umeme, matumizi ya majumbani pamoja na kuendesha magari.
“Sekta ya mafuta na gesi ni sekta muhimu na wezeshi katika kukuza uchumi wa taifa. Tanzania, kama zilivyo nchi nyingine zenye rasilimali za gesi asilia na mafuta, imeweka msisitizo mkubwa katika ushirikiano na sekta binafsi ili kunufaika na teknolojia na mitaji,” amesema Mhe. Makamba.
Amefafanua kuwa mahitaji ya nishati nchini yanaendelea kuongezeka kutokana na ukuaji wa kasi wa uchumi, hali inayoongeza uhitaji wa nishati ya uhakika na endelevu.
Pia, amesema jiografia ya Tanzania inaipa nchi fursa ya kuhudumia nchi jirani kupitia bandari zake pamoja na kuunganisha mifumo ya umeme na nchi za Afrika Mashariki na Kusini mwa Jangwa la Sahara, huku ikizingatia ulinzi wa mazingira.
Vilevile, Mhe. Makamba amesema Serikali inasisitiza kuwa mpito kuelekea matumizi ya nishati safi na rafiki kwa mazingira lazima uwe wa haki, usiomwacha mwananchi yeyote nyuma, kwa kuhakikisha upatikanaji wa nishati ya gharama nafuu, salama na ya uhakika.
Maadhimisho ya Wiki ya Nishati ya India (IEW 2026) yanaendelea kutoa fursa kwa Tanzania kujitangaza katika majukwaa ya kimataifa, kuvutia wawekezaji zaidi na kuchochea ukuaji wa uchumi unaoendana na maendeleo ya teknolojia.&&&&




EmoticonEmoticon