Mhe. Balozi Dkt. Batilda Burian, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, ameipongeza Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) kwa mchango wake mkubwa katika kuchagiza mageuzi ya sekta ya kilimo kutoka kilimo cha kujikimu kwenda kilimo cha kibiashara.
Mhe. Mkuu wa Mkoa ametoa pongezi hizo alipotembelea banda la TADB katika Maadhimisho ya Wiki ya Huduma za Fedha Kitaifa yaliyofanyika katika Viwanja vya Usagara, jijini Tanga.
Katika banda la TADB, Mhe. Mkuu wa Mkoa alipokelewa na wafanyakazi wa benki hiyo na kupatiwa muhtasari wa maendeleo na ukuaji wa benki, pamoja na huduma mbalimbali zinazotolewa katika minyororo ya thamani ya kilimo, mifugo na uvuvi, hususan katika Mkoa wa Tanga na Kanda ya Kaskazini kwa ujumla.
Aidha, TADB inaishukuru Wizara ya Fedha pamoja na Kamati ya Maandalizi ya maadhimisho hayo kwa kutambua mchango wa benki katika kutoa huduma bora za kifedha kupitia mabanda na utoaji wa elimu ya fedha kwa wananchi wa Mkoa wa Tanga na mikoa ya jirani.
Kutokana na mchango huo, TADB ilitambuliwa kama mshindi wa nafasi ya tatu miongoni mwa mabenki na taasisi za fedha, na kukabidhiwa tuzo maalum.
Maadhimisho ya Wiki ya Huduma za Fedha Kitaifa yamehitimishwa leo tarehe 26 Januari 2026 katika Viwanja vya Usagara, jijini Tanga.





EmoticonEmoticon