Ushindi wa maendeleo katika nchi yetu upo mikononi mwa walimu ambao wao wana uwezo mkubwa wa kuzalisha wataalamu wenye ujuzi, maarifa na ubobezi wa fani mbalimbali zenye kuleta tija kwa taifa letu la Tanzania.
Hayo yamesemwa leo mjini Iringa na Dkt. Lyabwene Mutahabwa kamishna wa Elimu nchini kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia alipokuwa akizungumza na walimu zaidi ya 80 wa masomo ya Sayansi na Hisabati kutoka shule 9 za Halmashauri ya wilaya ya Iringa (Iringa vijijini) wanaoshiriki katika awamu ya pili ya mradi wa mafunzo ya kuboresha mbinu za ufundishaji wa masomo haya (CL4STEM) yaliyoandaliwa na Chuo Kikuu Huria cha Tanzania na washarika wake.
"Walimu ni nguzo muhimu sana katika maendeleo kwani bendera ya ushindi ipo mikoni mwenu na mkitambua hili basi tayari nchi yetu itakwenda kwa kasi zaidi katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi. Tujitahidi pia kushirikiana na wazazi katika kutambua vipaji vya watoto mapema na kisha kuviendeleza vipaji hivyo." Alisema Dkt. Mutahabwa.
Aidha, aliendelea kueleza kwamba walimu wa masomo ya Sayansi na Hisabati wanapowapenda wanafunzi inakuwa ni njia ya kuwafanya wanafunzi kuyapenda masomo hayo kuliko hivi sasa ambapo wengi wa wanafunzi huogopa masomo ya Sayansi na Hisabati kwa madai kwamba ni magumu. Dkt. Mutahabwa amesema,
"Nawaomba sana walimu wetu hebu ongezeni upendo kwa wanafunzi na msiwatamkie maneno kwamba Sayansi na Hisabati ni ngumu. Hii inawatia woga na kukata tamaa ya kusoma masomo haya muhimu kabisa kwa maendeleo ya taifa letu. Naomba kila mmoja akitoka hapa pamoja na uwezo mtakaojengewa na Chuo Kikuu Huria cha Tanzania mkawajenge wanafunzi kupenda masomo ya Sayansi na Hisabati."
Dkt. Mutahabwa alikuwa mgeni rasmi kwenye hafla ya uzinduzi wa mradi huu wa CL4STEM kwa walimu awamu ya pili uliofanyika Chuo Kikuu Huria cha Tanzania Tawi la mkoa wa Iringa. Amekipongeza sana Chuo kwa mradi huu muhimu wenye lengo la kuwaimarisha zaidi walimu wa masomo ya Sayansi na Hisabati kwa kuwapa mbinu mpya za ufundishaji na ujifunzaji kwa kutumia mifumo ya kisasa kama MOODLE, Zoom na Mobile CoPs (Whatsapp).
Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Chuo Prof. Elifas Bisanda ameeleza kwamba, Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kipo msitari wa mbele katika kuhakikisha taifa linapata walimu bora wenye ujuzi na mbinu zote muafaka za kufundisha ikiwa ni pamoja na kutumia vishikwambi vilivyotolewa na serikali kwa walimu wote. Amesema,
"Mradi huu ni sehemu ya jitihada za Chuo chetu katika kuendeleza walimu katika nchi yetu. Kigoda cha UNESCO katika Mitaala cha Chuo Kikuu Huria cha Tanzania ndicho kinachoshughulikia mafunzo haya kwa ufadhili wa IDRC, Canda. Ambapo baada ya kuona ufaulu wa masomo ya Sayansi na Hisabati kwa wahitimu wa shule za sekondari na matumizi ya elimu hiyo katika maisha ya kawaida si mazuri sana, tukaja na mradi huu ambapo tulifanya awamu ya kwanza na sasa tupo awamu ya pili inayozinduliwa leo."
Prof. Bisanda ameongeza kwamba, Chuo Kikuu Huria cha Tanzania ni kinara katika kutoa programu za kuendeleza walimu kuanzia ngazi ya astashahada, stashahada, shahada, stashahada ya uzamili, shahada za umahiri na uzamivu. Kupitia mifumo nyumbufu ya usomaji, mitihani na uhitimu, walimu wa masomo ya Sayansi, Hisabati na fani nyingine zote wanaweza kujiendeleza huku wanaendelea na kazi zao shuleni.Chuo kina vituo katika mikoa yote Tanzania Bara na vituo vya uratibu Unguja na Pemba.
Nao Dkt. Kenneth Nzowa kutoka Taasisi ya Elimu Tanzania, Anosta Nyamoga kutoka ofisi ya Rais TAMISEMI na Tina Sanga afisa taaluma upande wa sekondari kutoka halmashauri ya wilaya ya Iringa (Iringa vijijini) wamekipongeza sana Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kwa mradi huu wa walimu katika halmashauri hii na kuisaidia serikali katika kuandaa walimu wa ngazi mbalimbali kwa ujumla na kukitaka chuo kuendelea kubuni miradi mingi zaidi ya namna hii. Wamesema kwamba lengo la serikali na halmashairi zetu ni kuona walimu wa masomo ya Sayansi na Hisabati wanapata mbinu mpya na za kisasa ili kutoa wahitimu wenye msingi mzuri uliolengwa na mabadiliko ya hivi karibuni ya sera na mitaala ya elimu kuliwezesha taifa kufikia uchumi wenye viwanda vingi.
Naye mratibu wa mradi huu Dkt. Edephnce Nfuka ambaye pia ni Mkurugenzi wa huduma za Ushauri wa Kitaalamu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania ametanabahisha kwamba lengo kuu ni kuhakikisha walimu wetu wanapata mbinu za kufundishia na wanafunzi kujifunzia kwa kutumia zana zinazopatokana katika mazingira yao. Pia, kutumia teknolojia na mifumo yake ili kukuza uelewa wa wanafunzi, kuwaondoa kwenye kukariri, kuwajumuisha wenye mahitaji mbalimbali na kutomwacha nyuma mwanafunzi yoyote kwa sababu zozote zile. Haya ndiyo malengo ya mradi huu wa CL4STEM kwa walimu wa sayansi na hisabati na tunalenga walimu katika maeneo yote mijini, maeneo ya pembezoni na vijijini. Mafunzo haya kwa walimu ambayo pia yanayoendelea Nigeria na Bhutan kwa kushiriana na India yanafanyika kwa siku mbili za tarehe 30 mpaka 31 Januari 2024 ambapo pamoja na mambo mengine walimu watasajiliwa kwenye mfumo wa Ufundishaji na Ujifunzaji Kielektroniki (MOODLE) na kuendelea na mafunzo kwa mwaka mmoja wakiwa kazini na wakiwa wanatumia mbinu hizo moja kwa moja darasani.
Akitoa neno la shukurani Prof. Paul Ikwaba ambaye ni kaimu Mkurugenzi wa Mitihani na Huduma za Ufundishaji wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania amesema kwamba katika shughuli ya leo ya ufunguzi wa awamu ya pili ya mradi amepata kauli mbiu mbili ambazo ni "Bendera ya ushindi ipo mikononi mwa mwalimu," na "Sayansi na Hisabati kwa wote." Ameeleza kwamba kauli mbiu hizi ni za muhimu na kila mwalimu azitekeleze kwa vitendo kwa wanafunzi wake wote katika ufundishaji na ujifunzaji. Jamii pana ya Watanzania na walimu wote nchini wazitekeleze kauli mbiu hizi na iwe ni wimbo wa kutoa hamasa kwa mafanikio ya masomo ya Sayansi na Hisabati kwa maendeleo ya viwanda nchini Tanzania.
Uzinduzi huu pia ulihudhuriwa na mkuu wa Kitivo cha sayansi, teknologia na elimu ya mazingira, Prof Joel Mihale na mkuu wa Kitivo cha Elimu, Dr Theresia Shavega ambao, pamoja na mengine, waliombwa kutengeneza mtaala wa postgraduate diploma na baadae masters katika maeneo ya digital education kama vile instructional design and e-learning technologies ambao utajumuisha baadhi ya maeneo kutoka katika mafunzo haya mafupi.
EmoticonEmoticon