MAMBO YA KUSTAAJIBISHA AMBAYO YANAPATIKANA TANZANIA

June 26, 2017
                     Na Jumia Travel Tanzania

Inastaajabisha kuona watu wa mataifa ya nje wanajua vitu vingi zaidi vinavyopatikana Tanzania kuliko watanzania wenyewe. Sijui ni ile hulka ya kutopenda kufuatilia mambo au ni dhana kwamba waache wageni waje kushangaa maana hivyo vitu vitaendelea kuwepo tu.

Nchi yetu imebarikiwa na inaendelea kubarikiwa kugunduliwa kwa mambo mengi zaidi ya kustaajabisha ambayo hayapatikani kwingineko duniani. Jumia Travel ingependa kukufumbua macho kwamba yafuatayo ni baadhi tu ya mambo yanayopatikana na unaweza kuyashuhudia ukiwa nchini Tanzania.


Mti mrefu zaidi barani Afrika. Hivi karibuni mtafiti kutokea Chuo Kikuu cha Byreuth cha nchini Ujerumani, Dkt. Andreas Hemp baada ya utafiti wa takribani miaka 20 amethibitisha kuwa Tanzania ina mti mrefu zaidi kuliko yote barani Afrika ukiwa na urefu wa mita 81.5. Mti huo kwa jina la kitaalamu unajulikana kama ‘Entandrophragmaexcelsum’, ni aina adimu sana ya miti na inaweza kuwa na umri wa zaidi ya miaka 600. Ili kuweza kuuona mti huo unaopatikana katika safu ya misitu ya Mlima Kilimanjaro na kuwa kivutio kikubwa kwa watalii hivi sasa, itakupasa utembee umbali wa masaa 2.30 mpaka kutokea kijiji cha Tema ili kuufikia.

Twiga mweupe aonekana kwa mara ya kwanza.  kubisha kwamba hiko kitu hakiwezekani lakini ndio maajabu ya Mungu hayo, twiga mweupe ameonekana Tanzania. Takribani mwaka mmoja uliopita, mwanzilishi na mwanasayansi katika Taasisi ya Misitu Asilia katika hifadhi ya taifa ya Tarangire inayopatikana mkoani Manyara, Dkt. Derek Lee alimuona twiga mwenye rangi nyeupe. Twiga huyo ambaye alikuwa na umri wa miezi 15 amepewa jina la ‘OMO,’ rangi yake inaonekana kama vile imechubuliwa tofauti na rangi asilia ya twiga tunaowajua. Mtafiti huyo amesema kuwa twiga huyo anasumbuliwa na ‘leucism,’ ni hali inayosababisha kupotea kwa baadhi ya rangi. Licha ya utofauti huo na wenzake lakini bado mnyama huyo anajichanganya na wengine na wenzie kutojali utofauti huo kabisa.   
 
Asilimia 30% ya ardhi ya Tanzania ni hifadhi za wanyama pori. Kama ulikuwa haujui basi ni kwamba nchi ya Tanzania sehemu ya asilimia 30 ya ardhi yake ni hifadhi za wanyama pori wa aina mbalimbali duniani. Tanzania inazo hifadhi za taifa 16 ambazo zinasimamiwa na Mamlaka ya Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) ambapo kwa ujumla wake zina ukubwa wa kilometa za mraba takribani 42,000. Kwa mfano, hifadhi ya taifa ya mbuga ya Serengeti ni mojawapo ya mbuga maarufu na inayopendwa zaidi duniani, ni makazi ya aina mbalimbali za wanyama zaidi ya milioni moja. Pia imetangazwa kuwa ni Eneo la Urithi wa Dunia na kutajwa mojawapo ya sehemu ya Maajabu Saba ya Dunia.
 
Takribani wanyama milioni 2 hushiriki tukio la kuhama linalotokea kila mwaka mbuga ya Serengeti. Kila mwaka watalii hushuhudia tukio la kipekee la uhamaji wa makundi ya wanyama wa aina ya pundamilia na nyumbu zaidi ya milioni 1.5. Tukio hilo hutokea kati ya Kusini mwa bonde la mbuga ya Serengeti nchini Tanzania kuelekea eneo la Kaskazini mwa mbuga ya Masai Mara iliyopo Kenya. Lengo kubwa la tukio hilo ni katika harakati za kutafuta malisho mazuri kwa wanyama hao ambalo hutukia mnamo miezi ya Mei mpaka Desemba ingawa muda huwa unaweza kubadilika. Sehemu inayosisimua zaidi ni pale wanyama hao wanakatisha mto Mara kuuvuka kuelekea Masai Mara, wanyama hao kwa makundi na ujasiri mkubwa huvuka licha ya kuwa na mamba wakali.   
 
Mbuyu unaweza kuishi mpaka miaka 1,000. Mibuyu ni miti mikubwa na inayovutia zaidi, hapa nchini Tanzania unaweza kuiona vizuri zaidi ukitembelea hifadhi ya taifa ya Tarangire. Kama ulikuwa haufahamu ni kwamba baadhi ya aina ya miti ya mibuyu huweza kuishi kwa takribani miaka 1,000 au zaidi. Inasemekana mbuyu mkongwe zaidi unapatikana nchini Afrika ya Kusini ni unaaminika kuwa na miaka takribani 6,000.  
 
Uwepo wa vitu hivyo Tanzania ni uthibitisho wa namna nchi hii ilivyobarikiwa na vivutio mbalimbali ambavyo watu wengi hawavifahamu bado. Kwa hayo machache Jumia Travel inaamini utakuwa umejifunza na kupata shauku ya kutembelea maeneo hayo pamoja na kukuongezea ari ya kujifunza mengineyo zaidi.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »