WAZIRI NDEJEMBI:GHARAMA ZA UMEME HAZIJAPANDA KWA MIAKA 10

January 21, 2026


📌*Lengo ni Wananchi wamudu gharama za matumizi ya umeme*


Na Mwandishi Wetu, Dodoma


Licha ya kuongezeka kwa gharama za vifaa vya umeme ikiwemo nguzo, waya na mita, Serikali imeendelea kuhakikisha gharama za matumizi ya umeme kwa wananchi hazipandi kwa kipindi cha miaka 10 kuanzia mwaka 2016.

Akizungumza Januari 21, 2026 jijini Dodoma katika kikao cha pili kati ya Wizara ya Nishati, taasisi zake na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Waziri wa Nishati, Mhe. Deogratius Ndejembi, amesema hatua hiyo imelenga kila mwananchi apate  huduma ya umeme kwa gharama nafuu.

Amesema kiwango cha uunganishaji wa umeme nchini kimefikia asilimia 52, huku Serikali ya Awamu ya Sita ikiweka lengo la kufikia asilimia 75 ifikapo mwaka 2030 linalotekelezwa kupitia Mpango wa Nishati uliosainiwa Januari 2025 wakati wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika.

Akizungumzia suala la mita janja, Waziri Ndejembi amesema kuwa zoezi la uunganishaji wa mita hizo linaendelea nchi nzima na zitamwezesha mwananchi kupata umeme mara moja baada ya kununua token bila kutumia kifaa cha ziada cha kuingiza namba (CIU), hatua itakayopunguza changamoto zilizokuwepo katika mfumo wa awali.

Kuhusu upatikanaji wa umeme wa Gridi mkoani Rukwa, Waziri Ndejembi amesema mradi wa njia ya kusafirisha umeme wa kilovoti 400 unaendelea kutekelezwa kupitia mkandarasi TBEA na itawezesha mkoa huo kupata umeme wa uhakika na wa kuaminika.

Aidha, ametaja mradi wa kuimarisha upatikanaji wa umeme katika mikoa ya Mtwara, Lindi, Tabora na Simiyu, unaotekelezwa na mkandarasi Kalpataru.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Mhe. Subira Mgalu, amepongeza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa kazi kubwa wanayoifanya katika kuhakikisha wananchi wanapata nishati ya umeme ya uhakika.

Amesema mafanikio hayo yametokana na maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kupitia utekelezaji wa miradi mikubwa ya uzalishaji umeme ikiwemo Mradi wa Julius Nyerere (JNHPP) wa megawati 2,115, mradi wa umeme wa jua wa Kishapu unaotarajiwa kuanza kuzalisha megawati 50, pamoja na mradi wa Malagarasi wa megawati 49 unaoendelea kutekelezwa.

Mhe. Mgalu ameongeza kuwa kuimarika kwa upatikanaji wa umeme kumechangia kwa kiasi kikubwa ukuaji wa uchumi na ongezeko la mapato ya Serikali, hususan katika sekta za viwanda na migodi, hali iliyoisaidia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuvunja rekodi ya makusanyo kwa kufikia Sh.trilioni 4.13 mwezi uliopita.


Vilevile, amepongeza REA kwa kuwapa kipaumbele wakandarasi wa ndani katika miradi ya usambazaji umeme pamoja na kampeni ya kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia, akisisitiza umuhimu wa elimu hiyo kufika hadi ngazi ya shule za awali.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »