Na: Mwandishi Wetu, Tanga
Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan imedhamiria kuboresha maisha ya wananchi kupitia ukuzaji wa maendeleo ya sekta mbalimbali. Miongoni mwa sekta hizo ni kilimo cha baharini cha zao la Mwani.
Kutokana na umuhimu wa zao hili la Mwani linalolimwa baharini na katika vyanzo vingine vya maji, viongozi wamepewa maelekezo ya kuhakikisha wanalipa kipaumbele ili liweze kuwa mkombozi kwa wananchi. Mbunge wa Jimbo la Tanga Mjini, Ummy Mwalimu, kwa upande wake, amechukua jitihada za kuinua zao hili la mwani kwa kutoa mafunzo ya kilimo hiki kwa kuanza na wakulima 200.
![]() |
Bahari yetu mgodi wetu, Mwani wetu dhahabu yetu. Hayo ni maneno ya Ummy Mwalimu, Mbunge wa Tanga Mjini na Balozi wa zao la Mwani, ambaye ana ndoto ya kuona kilimo cha mwani kikiwa mkombozi wa wananchi wa Tanga Kwa kuwakomboa kiuchumi. Sababu moja wapo ya Ummy Mwalimu kukipa msukumo kilimo cha zao la Mwani ni uwepo wa mazingira mazuri ya bahari katika kufanikisha na kukuza zao hili la Mwani.
Kutokana na umuhimu wa zao la Mwani, Ummy Mwalimu ametafuta ufadhili wa taasisi isiyo ya kiserikali ya Korea iitwayo Good Neighbourhood Foundation ili iweze kuwajengea uwezo wakulima wa mwani wapatao 200 ili waweze kulima kisasa, ambapo hadi sasa wakulima 100 wameshawezeshwa kimafunzo na pia kupewa kamba ambazo ni nyenzo muhimu katika kilimo cha Mwani.
Katika mafunzo ya kilimo cha mwani yaliyofanyika mwaka jana 2024 kwa awamu mbili tofauti, Ummy Mwalimu alisema "Tunataka mlime Mwani kisasa, lakini si tu mlime lakini pia mpate faida kwa sababu mwisho wa siku tunataka mpate pesa za kujenga nyumba, kusomesha watoto na kufanya shughuli nyingine za maendeleo."
RAIS SAMIA AGAWA BOTI 50 TANGA KUINUA KILIMO CHA MWANI
Februari 26, 2025, katika ziara yake wilayani Pangani mkoani Tanga, Rais Samia aligawa boti 50 zitakazotumika katika kilimo cha Mwani mkoani Tanga. Boti hizi ni kichocheo kizuri cha kukuza kilimo cha Mwani ambacho Ummy Mwalimu amekuwa akikipigia chapuo sana na kukipa msukumo mkubwa kwa kuamini kuwa bahari ndiyo shamba na mgodi wa wananchi wa Tanga.
Hivyo basi, ugawaji wa boti za kufuatilia kilimo cha Mwani baharini ni mwelekeo mzuri wa serikali kukuza zao hili na kuwawezesha wananchi kuinuka kiuchumi na kuchangia pato la nchi yao. Ni maono ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kuona maisha ya wananchi yakiwa bora zaidi kupitia kilimo cha Mwani.
Ummy Mwalimu ameonyesha jitihada za wazi, wengine pia wapiganie zao la Mwani, liwakomboe wananchi. Kwa hakika, ziara ya Rais Dk. Samia mkoani Tanga imeleta neema ya kuinua zao la Mwani ambalo ni muhimu katika kukuza vipato vya wananchi na uchumi wa nchi yetu kwa ujumla.
EmoticonEmoticon