Mratibu wa Shiriki la EngenderHealth Mkoa wa Tangam, Loveness Malisa.
Na Dotto Mwaibale, Tanga
SHIRIKA la
EngenderHealth kupitia mradi wa SuFP kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais-Tawala
za Mikoa na Seikali za Mitaa (TAMISEMI) na Wizara ya Afya (MoH) ambalo linatoa huduma
za afya uzazi kwa wanawake, vijana, watu wenye ulemavu, na jamii kwa ujumla
kupitia utoaji wa huduma zinazozingatia mahitaji ya makundi mbalimbali katika
jamii
limetoa mafunzo kwa watoa huduma takribani 78 Mkoa wa Tanga.
Hayo yamebainishwa na Mratibu wa Shirika hilo Mkoa wa Tanga, Loveness Malisa wakati wa maadhimisho ya Siku ya Watu Wenye Ulemavu Duniani yaliyifanyika mkoani hapa jana Desemba 3, 2024.
Alisema mafunzo hayo yalihusu utoaji wa huduma shirikishi na jumuishi ambapo pia watoa huduma wa ngazi ya jamii takribani 23, wamepata mafunzo ya aina hiyo.
“ Huduma hizi zinasaidia jamii katika kupanga uzazi kwa njia salama, kupunguza matukio ya ukatili wa kijinsia, na kuongeza uelewa na upimaji wa VVU. Vilevile, mradi wa SuFP unatoa huduma jumuishi na shirikishi kwa watu wenye ulemavu,” alisema Malisa.
Alisema katika utekelezaji wake, shirika hilo linafanya kazi katika mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara ikiwemo Mkoa wa Tanga, likizingatia utoaji wa huduma jumuishi na shirikishi, kuimarisha mifumo ya afya, na kuwajengea uwezo watoa huduma za afya.
Malisa akizungumzia Maana na Malengo ya Siku ya Watu Wenye Ulemavu Duniani alisema huadhimishwa kila mwaka Desemba 3, yakilenga kukuza uelewa kuhusu haki na ustawi wa watu wenye ulemavu, Kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa kuwajumuisha watu wenye ulemavu katika kila nyanja ya maendeleo, ikiwemo afya, elimu, na ajira.
Malisa
alitaja malengo mengine kuwa ni kutathmini maendeleo katika utekelezaji wa sera
na mikakati ya kuhakikisha usawa na ujumuishaji wa watu wenye ulemavu na kuwa
ni jukwaa maalum la kuwawezesha watu wenye ulemavu kuweza kuonesha vipaji vyao
na kueleza changamoto wanazokumbana nazo katika maisha ya kila siku.
Alisema wakati wakiadhimisha siku hiyo wanakumbushwa kuwa ujumuishaji na ushirikishaji wa watu wenye ulemavu si jukumu la mtu mmoja, bali ni jukumu la watu wote.
Malisa akizungumzia mchango wa Shirika la EngenderHealth Kupitia Mradi wa Scaling Up Family Planning (SuFP) alisema kwa kutambua umuhimu wa ujumuishaji na ushirikishaji wa huduma za afya, hususani afya ya uzazi, kama mradi wamekuwa wakitoa huduma za Afya ya uzazi ambazo ni jumuishi na shirikishi ambazo hazibagui mtu yeyote.
Alisema ili kuhakikisha watu wenye ulemavu wanapata huduma sawa na wengine katika vituo vya afya haki ya upatikanaji wa huduma wamekuwa mstari wa mbele kuhakikisha huduma za afya ya uzazi zinapatikana wakati wote, kwa kila mtu, bila kujali hali ya mtu.
Malisa alitaja baadhi
ya changamoto kuwa ni idadi ya watoa
huduma waliopata mafunzo ya huduma jumuishi na shirikishi kuhusu watu wenye
ulemavu bado ni ndogo sana na hivyo kushindwa kutimiza mahitaji kama
inavyostahili.
Alitaja changamoto nyingine kuwa ni mfumo wa
kukusanya taarifa za afya (MTUHA) haujaweza kutambua kikamilifu watu wenye ulemavu
wanaopata huduma, hali inayotatiza upatikanaji wa takwimu za watu wenye ulemavu
na mwisho ufanyaji wa maamuzi sahihi.
Shirika hilo ili kuimarisha huduma limetoa mapendekezo ya mafunzo kwenye mitaala ya
vyuo vya afya Serikali iweke mafunzo ya huduma shirikishi katika mitaala ya
mafunzo ya wanafunzi wa kada ya afya.
Alitaja mapendekezo mengine kuwa ni kuboresha miundombinu katika vituo vyote vya afya na viwe na miundombinu rafiki kwa watu wenye ulemavu, Mafunzo kazini (OJT) yatolewe mara kwa mara kwa watoa huduma kuhusu huduma shirikishi kwa watu wenye ulemavu na kufundisha matumizi ya lugha za alama kwa watoa huduma wa afya vituoni.
Malisa kwa niaba ya EngenderHealth, alitumia hiyo kuishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kujenga vituo vingi vya afya vinavyorahisisha upatikanaji wa huduma kwa jamii, wakiwemo watu wenye ulemavu.
Aidha aliishuru Ofisi ya Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tanga, mganga mkuu jiji la Tanga kwa ushirikiano wa karibu katika kuhakikisha huduma za afya ya uzazi zinapatikana kwa watu mbalimbali na kwa wadau wote wa maendeleo kwa mchango wao katika safari ya kuhakikisha huduma za afya ya uzazi zinapatikana kwa usawa.
Kwa upande wake Afisa Utetezi kutoka Youth With
Disability Community Program, Prisca Mwakasendile akitoa mada inayohusu aina za
ukatili wa kijinsia alizitaja kadhaa kuwa ni ukatili wa kingono, uchumi,
vipigo, unyanyapaaji na kueleza kuwa ukati wa aina yoyote ile haukubaliki hata
kidogo.
Lilian Gwido ambaye ni Muuguzi kutoka Kituo cha
Afya, Duga, alielezea umuhimu wa uzazi wa mpango ambao alizitaja baadhi ya njia
za uzazi wa mpango kuwa ni zile za muda mfupi na mrefu ikiwemo ya matumizi ya
mipira ya kiume (kondomu) wakati wa kufanya tendo la ndoa.
Mwansiti Hatibu ambaye ni mlemavu alisema
changamoto kubwa wanayoipata wanapokwenda kutibiwa Hospitali wamekuwa hawapewi
kipaumbele cha kutibiwa na kuachwa muda mrefu kwenye foleni jambo ambalo
linawakwaza.
“Jambo hili ni changamoto kubwa sana kwetu sisi
watu wenye ulemavu utakuta kuna baadhi ya madaktari hawatuonei huruma kabisa na
kuna baadhi ya Hospitali wameandika matangazo yanayo eleza apishwe mzee
akatibiwe lakini kwa walemavu hawaoni kama ni changamoto,” alisema Hatibu.
Hatibu alisema changamoto nyingine ni usumbufu mkubwa wanaoupata wanapofuatilia mkopo wa asilimia mbili unaotoa na Halmashauri ambapo alisema kumekuwa na danadana nyingi za kwenda na kurudi jambo ambalo linawachosha watu wenye ulemavu kutokana na hali zao.
Ernes Hoza ambaye anachangamoto ya kuto sikia
amesema kumeibuka madalali ambao wanachukua kazi kwa watu kwa mapatano ya fedha
kubwa na kuwapa walemavu wenye ujuzi kama wa ufundi umeme, bomba na mwingine ambao
uwapa hela kiduchu pasipo kufanya mizania ya malipo yanayoendana na kazi waliyoifanya.
Afisa Utawi wa Jamii, Doroth Omari kutoka Tanga jiji, akizungumza kwenye maadhimisho hayo aliwata washiriki hao pale wanapokumbana na changamoto mbalimbali wafike ofisi za ustawi wa jamii kupeleka malalamiko yao ili wakapatiwe msaada.
Mwansiti Hatibu
EmoticonEmoticon