NA: MWANDISHI WETU, TANGA
Tarehe 08 Machi ya kila mwaka ni Siku ya Wanawake Duniani. Siku hii imebeba tafakuri ya kina juu ya mchango wa mwanamke katika kuchochea maendeleo ya nyanja zote; kijamii, kiuchumi na kisiasa. Pia, ni siku ya kujadili changamoto zinazowakabili wasichana na wanawake ili kuzitatua kama msingi wa kuharakisha maendeleo. Wanawake ni wadau muhimu wa maendeleo na bila ushiriki wao ipasavyo, juhudi hizo hazitazaa matunda yanayotarajiwa, ndiyo maana jamii inapaswa kuwashirikisha wasichana na wanawake kikamilifu.
Sambamba na hilo, wanawake wamekuwa wakihamasishwa kugombea nafasi mbalimbali za uongozi kama Udiwani, Ubunge na hata Urais ili wapaze sauti zao wenyewe moja kwa moja badala ya kutegemea kusemewa na wanaume au kutegemea uwepo wa nafasi za viti maalum kwenye Udiwani na Ubunge. Ummy Mwalimu, Mbunge wa Tanga Mjini, ni mfano wa wabunge wanawake katika Bunge la Tanzania walioamua kugombea na kushinda ubunge mwaka 2020.
Ummy Mwalimu ambaye kitaaluma ni Mwanasheria, alianza kuwa Mbunge wa viti maalum mkoa wa Tanga kwa vipindi viwili yaani mwaka 2010-2015 na baadaye 2015-2020. Mwaka 2020 aligombea rasmi Ubunge kuwakilisha wananchi wa Jimbo la Tanga Mjini ambapo aliibuka mshindi kwa kishindo kikubwa. Kwa hakika, Ummy Mwalimu ni kielelezo cha wanawake wenye uthubutu na kujiamini katika uongozi.
Kimsingi, Ummy Mwalimu amefanikiwa kuwa Mbunge wa mfano Bungeni kutoka na uchapakazi na uhodari wake wa kujenga hoja akiwasilisha vyema changamoto za wananchi wa Tanga Mjini ili viweze kufanyiwa kazi. Hata Wizara mbalimbali alizohudumu kama Waziri, amekuwa kielelezo kizuri cha uchapakazi uliotukuka.
Kwa mfano, Ummy Mwalimu amewahi kuwa Waziri wa Afya kwa vipindi viwili (2015-2020 na 2022-2024). Vilevile, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) mwaka 2021. Pia, Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Naibu Waziri, Ofisi ya Makamu wa Rais - Mazingira na Naibu Waziri Katiba na Sheria (2010-2015). Nafasi hizo zote amezitumikia kwa ufanisi na kuacha matokeo mazuri kote alipohudumu.
![]() |
Sanjari na hilo, ni katika uongozi wake ambapo Jimbo la Tanga Mjini limepiga hatua kubwa za kimaendeleo hasa katika miradi mikubwa ya kimaendeleo na ya kimkakati. Mathalani, uboreshaji wa huduma za afya, elimu, maji, umeme, barabara, bandari, masoko, kilimo cha mwani, utoaji wa mikopo kwa wanawake, vijana na wenye mahitaji maalum na huduma nyingine nyingi. Ummy Mwalimu amethibitisha uwezo mkubwa wa kiuongozi walionao wanawake katika kuwatumikia wananchi. Huyu ndiye Ummy Mwalimu, kwa jina maarufu "Odo Ummy."
Ikumbukwe kuwa kilele cha Siku ya Wanawake Duniani ni Tarehe 08 Machi ya kila mwaka ambapo kwa mwaka huu 2025, maadhimisho hayo yatafanyika mkoani Arusha, yakichagizwa na kaulimbiu isemayo: Wanawake na Wasichana 2025: Tuimarishe Haki, Usawa na Uwezeshaji; huku Mgeni Rasmi akitarajiwa kuwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.
EmoticonEmoticon