CCM YAFANYA BONANZA KUHAMASISHA WANANCHI KUSHIRIKI UCHAGUZI KWA AMANI

October 07, 2025 Add Comment



Mgeni rasmi katika bonanza hilo alikuwa Mwenyekiti wa UWT Taifa, Mary Pius Chatanda,mgombea ubunge wa Jimbo la Segerea, Bonnah Kamoli na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (MNEC) na Mratibu wa Kampeni za CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Richard Kasesela kwa pamoja walihimiza kufanya mazoezi kila siku na kupiga kura siku ya uchaguzi mkuu kwa amani na utulivu

Mgeni rasmi katika bonanza hilo alikuwa Mwenyekiti wa UWT Taifa, Mary Pius Chatanda,mgombea ubunge wa Jimbo la Segerea, Bonnah Kamoli na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (MNEC) na Mratibu wa Kampeni za CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Richard Kasesela kwa pamoja walihimiza kufanya mazoezi kila siku na kupiga kura siku ya uchaguzi mkuu kwa amani na utulivu

Na Fredy Mgunda.


Chama cha Mapinduzi (CCM) kimeandaa Bonanza Maalum katika Jimbo la Segerea, mkoani Dar es Salaam, kwa lengo la kuhamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 29, kwa njia ya amani na utulivu.

Mgeni rasmi katika bonanza hilo alikuwa Mwenyekiti wa UWT Taifa, Mary Pius Chatanda, ambaye aliwataka wananchi kutumia haki yao ya kidemokrasia kwa kupiga kura kwa amani, akisisitiza kuwa kiongozi anayechaguliwa leo ndiye atakayekuwa na mamlaka ya kuleta maendeleo kwa miaka mitano ijayo.

“Kupiga kura ni haki ya msingi kwa kila Mtanzania. Tuchague viongozi wanaotuletea maendeleo ya kweli,” alisema Chatanda.

Akimnadi mgombea urais wa CCM, Dkt. Samia Suluhu Hassan, Chatanda alisema kuwa serikali ya awamu ya sita imeitekeleza ilani ya CCM ya mwaka 2020-2025 kwa asilimia 100, na hivyo anastahili kupewa tena ridhaa ya kuendelea kuongoza nchi.

Aidha, alitoa wito kwa wananchi kumchagua mgombea wa CCM katika nafasi ya urais, ubunge na udiwani ili kuimarisha juhudi za maendeleo nchini.

Kwa upande wake, mgombea ubunge wa Jimbo la Segerea, Bonnah Kamoli, alisisitiza kuwa mojawapo ya sera zake ni kuhamasisha mazoezi ya mara kwa mara kwa wananchi, ili kuboresha afya ya mwili na akili.

“Afya bora ni msingi wa maendeleo. Tukifanya mazoezi tutakuwa na nguvu za kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa taifa,” alisema Kamoli.

Kamoli aliwaomba wakazi wa Segerea kumpigia kura nyingi pamoja na kumpa kura ya kishindo Dkt. Samia Suluhu Hassan, ili kuendeleza kasi ya maendeleo katika jimbo hilo.

Naye Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (MNEC) na Mratibu wa Kampeni za CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Kasesela, aliwataka wananchi kupuuza wanasiasa na wanaharakati wanaotumia mitandao ya kijamii kuchochea vurugu na hofu wakati huu wa uchaguzi.

“Wachochezi wengi wapo nje ya nchi. Vurugu zikitokea, ni Watanzania waliopo hapa ambao watateseka. Amani ni tunu ya taifa letu,tuilinde,” aliongeza Kasesela.

Katika bonanza hilo, wananchi walishiriki katika michezo mbalimbali, burudani, na kupata elimu juu ya umuhimu wa kushiriki uchaguzi kwa njia ya amani.

DKT. NCHIMBI AHITIMISHA KAMPENI ZA KUMUOMBEA KURA DK.SAMIA MKOANI TABORA

October 07, 2025 Add Comment


Na Mwandishi Wetu

MGOMBEA mwenza wa Urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Emmanuel John Nchimbi amehitimisha mikutano yake ya hadhara ya kampeni katika Mkoa wa Tabora huku akiacha ujumbe kuwa ifikapo Oktoba 29 mwaka huu wananchi wa mkoa huo wampigie kura mgombea urais wa Chama hicho Dk.Samia
Suluhu Hassan.

Dk.Nchimbi amehitisha ziara leo Oktoba 6, 2025 katika Mkoa wa Tabora ambapo katika mikutano ya kampeni mbali ya kumuombea kura mgombea urais Dk.Samia Suluhu Hassan, wabunge na madiwani pia ametumia mikutano hiyo kunadi sera na Ilani ya uchaguzi mkuu ambayo imelenga kuleta maendeleo ya watanzaniaL

Akiwa katika mkutano wa kampeni Dk.Nchimbi kabla ya kuanza kuwahutubia Wananchi amesimikwa kuwa msaidizi wa Mtemi, kimila akiitwa 'MTONGI' baada ya mkubwa wake Chifu Hangaya ambaye ni Raisi Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Dkt. Nchimbi amesimikwa na viongozi wa kimila wa Unyanyembe (Tabora) kwenye mkutano wake wa mwisho wa kampeni mkoani humo,katika kata ya Kigwa jimbo la Igalula, wilaya ya Uyui nakupewa jina la "NYUNGU YA MAWE".

Pamoja na mambo mengine,Dkt.Nchimbi aliwanadi wagombea Ubunge wa mkoa huo akiwemo mgombea Ubunge wa jimbo la Igalula, Ndugu Juma Ramadhan Mustafa [KAWAMBA) pamoja na Madiwani.

Aidha Dkt.Nchimbi pia alitumia nafasi hiyo kuwaomba wampigie kura za ushindi wa kishindo Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzani,Dkt.Samia Suluhu Hassan,Wagombea Ubunge na Madiwani kwa ujumla.

Balozi Nchimbi anafikia mkoa wa 18 sasa tangu kuzinduliwa kwa kampeni hizo Oktoba 28,2025 jijini Dar es Salaam,akiendelea kusaka kura za ushindi wa kishindo za Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan,Wabunge na Madiwani.












NGORONGORO NA TANAPA WAPANUA WIGO WA KUNADI UTALII SOKO LA ULAYA

October 07, 2025 Add Comment

 Na Mwandishi Wetu, Barcelona – Hispania

Mamlaka ya Hifadhi ya eneo la Ngorongoro (NCAA) na Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) wameendeleza jitihada za kuitangaza Tanzania kimataifa kupitia ushiriki wao katika maonesho ya utalii (Tourism Road Show) yanayofanyika nchini Hispania.

Onesho hilo lililoandaliwa na kampuni ya usimamizi wa safari (DMC) yenye makao makuu yake nchini Tanzania, (Tanganyika Expeditors) na kufanyika jijini Barecelona Oktoba 06, 2025 , limewaleta pamoja wadau mbalimbali wa sekta ya utalii wakiwemo mawakala wa safari za kitalii pamoja na wawekezaji kutoka maeneo mbalimbali ndani na nje ya jiji hilo. 

Kupitia ushiriki huo, NGORONGORO na TANAPA zimepata fursa kutoa taarifa muhimu za kuwasaidia mawakala wa usafiri kuandaa safari kwa wageni wanaotaka kutembelea Tanzania kujionea vivutio mbalimbali vinavyopatikana hifadhi ya  Ngorongoro na Hifadhi za taifa kama vile Serengeti, Manyara, Tarangire na maeneo mengine ya kipekee yanayosimamiwa na taasisi hizo.

Mbali na NCAA na TANAPA, washiriki wengine kutoka Tanzania ni pamoja na Miracle Experience -Tanzania, Auram Treks, Karafuu Beach Resort and Spa na Malia Hotels International.

Maonesho hayo ya Tourism Road Show yaliyoanza leo tarehe 6 Oktoba yataendelea kufanyika katika majiji mengine ya Hispania, ikiwemo Madrid na Seville ambapo yanatajiwa kuhitimishwa tarehe 8 Oktoba, 2025.






NISHATI YAWASILISHA MIPANGO YA KIMKAKATI KUTEKELEZA DIRA YA TAIFA 2050

October 07, 2025 Add Comment




*📌 Ni katika kikao kazi na Tume ya Taifa ya Mipango.*


*📌Mradi wa usafirishaji umeme Chalinze–Dodoma ni miongoni mwa miradi ya kipaumbele kufanikisha Dira 2050,*


*📌Wizara ya Nishati na Tume ya Mipango kushirikiana kwa karibu kusimamia miradi ya Nishati kufanikisha malengo ya Dira 2050.*


Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba, amekutana na wataalam kutoka Tume ya Taifa ya Mipango wakiongozwa na Naibu Katibu Mtendaji – Menejimenti ya Utendaji na Tathmini, Dkt. Linda  Ezekiel kwa lengo la kujadili namna ambavyo Wizara na Taasisi zake zimejipanga kutekeleza miradi ya kimkakati ya nishati inayochangia katika kufanikisha malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.



Msingi wa kikao hicho umetokana na  Sekta ya Nishati kuainishwa katika Dira 2050 kuwa ni moja ya  vichocheo vitano vitakavyoongeza kasi ya kufikia malengo ya Dira hiyo, ikielezwa kuwa Nishati ya uhakika ni nyenzo muhimu katika kuchochea maendeleo ya viwanda na shughuli mbalimbali za kiuchumi ili kuboresha viwango vya maisha kwa kutoa fursa za ajira kwa maendeleo endelevu katika jamii.

Katika kikao hicho kilichofanyika jijini Dodoma na  kuhusisha Watendaji kutoka Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Nishati, 

Mha. Mramba amesema pande hizo mbili zimejipanga kuimarisha uratibu wa utekelezaji wa miradi ya nishati ili kuhakikisha kuwa  inalingana na vipaumbele vya kitaifa vya maendeleo. 

“Wizara ya Nishati inaendelea kutekeleza miradi mikubwa ya nishati ukiwemo mradi wa  kusafirisha umeme wa kV 400 wa Chalinze–Dodoma, ambao unatarajiwa kukamilika Juni 2026. Huu ni moja ya miradi  itakayoleta chachu ya kuimarisha upatikanaji wa umeme wa uhakika katika mikoa ya Katavi, Kigoma na maeneo mengine ambayo yamekuwa yakikabiliwa na changamoto za upatikanaji wa umeme thabiti." Amesema Mhandisi Mramba

Amesema kukamilika kwa miradi ya kimkakati ya umeme kutawezesha kutimiza moja ya shabaha katika Dira 2050 ambayo inaelekeza kuwa matumizi ya umeme yanapaswa kuongezeka na 

kufikia wastani wa Kwh 3,000 kwa kila mtu kwa mwaka.



“Tunataka kuwa Taifa lenye nishati ya uhakika, nafuu na safi kwa watanzania wote,  ili kutimiza lengo hili Serikali inawakaribisha wadau wa sekta binafsi kuwekeza katika miradi ya nishati  kwa kuwa mafanikio ya sekta hii yanategemea ushirikiano wa wadau wote. " Amesisitiza Mhandisi Mramba

Katika kikao hicho, Wizara pia iliwasilisha taarifa ya utekelezaji wa miradi ya Gesi Asilia na Mafuta,  Nishati Safi ya Kupikia, Umeme na Nishati Mbadala.


Kwa upande wake, Dkt. Linda  Ezekiel kutoka Tume ya Taifa ya Mipango, amepongeza ushirikiano uliopo kati ya Wizara ya Nishati na Tume hiyo akisisitiza kuwa mwelekeo wa miradi iliyoainishwa katika kikao hicho inaendana na malengo ya Dira 2050.

Amesema Tume itaendelea kufuatilia utekelezaji wa miradi hiyo ili kuhakikisha inachangia moja kwa moja katika ukuaji wa uchumi wa Taifa, kuboresha ustawi wa wananchi, na kulinda mazingira.


“DIRA ya 2050 inalenga kuwa na Taifa lenye uchumi wa kisasa, shindani na jumuishi. Sekta ya Nishati ni mhimili wa kufanikisha hayo yote, tunapongeza jitihada za Wizara ya Nishati katika kuhakikisha nishati inakuwa injini ya maendeleo." Ameeleza Dkt. Ezekiel

Kupitia kikao hicho, Wizara ya Nishati na Tume ya Taifa ya Mipango zimekubaliana kuendelea kushirikiana kwa karibu katika kupanga, kutekeleza na kufuatilia miradi yote inayogusa Sekta ya Nishati ili kuhakikisha Tanzania inafikia malengo ya  DIRA ya Maendeleo 2050 kwa ufanisi.

WIZARA YA NISHATI YAKAGUA MATUMIZI YA NISHATI SAFI YA KUPIKIA KWA TAASISI ZINAZOLISHA WATU ZAIDI YA 100 ILEMELA

October 07, 2025 Add Comment


📌 *Lengo ni kuhakikisha Taasisi za Umma na Binafsi zinatekeleza agizo la Serikali la kutumia Nishati Safi ya Kupikia*


📌 *Mkurugenzi wa Nishati Safi ya Kupikia ahimiza Wakurugenzi wa Halmashauri/Manispaa kuhakikisha agizo hilo la Serikali linatekelezwa*


📌 *Awaasa Walimu kufundisha Wanafunzi juu ya Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia*


Mkurugenzi wa Nishati safi ya Kupikia,  Nolasco Mlay pamoja na Wataalam kutoka Wizara ya Nishati   wameanza ziara ya kikazi mkoani Mwanza kwa lengo la kukagua utekelezaji wa agizo la Serikali kwa Taasisi zinazolisha watu zaidi ya 100 kutumia Nishati Safi ya Kupikia.

Ziara hiyo imeanza kwa kukagua  shule tatu za Sekondari katika Manispaa ya Ilemela ambazo zimeanza kutumia Nishati Safi ya Kupikia baada ya kunufaika na mradi wa CookFund kupitia mpango wa kimataifa wa Integrated Approach to Sustainable Clean Cooking Solution unaotekelezwa na Mfuko wa Maendeleo ya Mitaji wa Umoja wa Mataifa (UNCDF) kwa kushirikiana na Umoja wa Ulaya (EU).

Ziara hiyo pia inalenga kufanya tathmini ya matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia kwa taasisi zinazopokea ufadhili kutoka mradi wa CookFund.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Bw. Nolasco Mlay amesema kuwa ziara hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa Mkakati  wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia (2024–2034), ambao unalenga kuhakikisha taasisi za umma ikiwemo shule, zinatumia teknolojia salama na rafiki kwa mazingira katika upishi.

Katika kuhakikisha kuwa agizo hilo la Serikali linatekelezwa kwa mafanikio, Mlay amewasisitiza Wakurugenzi wa Halmashauri na Manispaa ambao bado taasisi katika maeneo yao hazijahama kutoka matumizi ya nishati isiyo safi  ya kupikia kuhakikisha kuwa wanatekeleza Mkakati  wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia.

"Taasisi za Umma na Binafsi katika maeneo yenu kama vile Shule, Hospitali, Magereza pamoja Jeshi zinapaswa kutumia teknolojia salama na rafiki kwa mazingira katika upishi ili kuepusha athari za kiafya na kimazingira kwa nchi." Amesema Mlay

Sambamba na hilo,  Mlay amewahimiza Walimu na Wakuu wa Shule kuwa mstari wa mbele kuwaelimisha wanafunzi juu ya faida ya matumizi ya nishati safi ya kupikia ili wawe mabalozi  wa kuelimisha wengine.

“Tunawaomba walimu kuelekeza wanafunzi kuhusu matumizi ya gesi asilia, majiko banifu na umeme kama njia mbadala za kuni na mkaa kwani watoto hawa wanapojifunza, watasaidia kubadilisha mitazamo ya jamii zao kutoka kwenye matumizi ya nishati isiyo safi na kutumia nishati safi ya kupikia". Amesisitiza  Mlay


Akizungumza kwa niaba ya Afisa Elimu Sekondari Manispaa ya Ilemela, Afisa Elimu Maalum wa Manispaa hiyo amepongeza utekelezaji wa mkakati wa matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia  unaoendelea katika Manispaa ya Ilemela akiahidi kuwa Manispaa hiyo itaendelea kutekeleza agizo hilo ambapo kwa sasa tayari kuna shule kumi ambazo zipo kwenye mpango huo wa matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Vilevile, Walimu Wakuu wa Shule zilizokaguliwa wameeleza kuwa matumizi ya nishati safi ya kupikia yamesaidia shughuli za upishi kufanyika katika mazingira rafiki na salama,  kuokoa muda  na kuwa na gharama nafuu.

Katika hatua nyingine,  Wataalam kutoka Wizara ya Nishati walitembelea shule ambazo bado hazijaanza kutumia nishati safi ya kupikia na kuwaasa Viongozi wa shule hizo zinazotegemea kuni na mkaa kuanza kuboresha mifumo yao ya upishi na kuhamia katika matumizi ya nishati safi ya kupikia.

 


Shule tatu zilizotembelewa katika Manispaa ya Ilemela ambazo zinatumia Nishati Safi ya Kupikia ni pamoja na Shule ya ufundi ya Wavulana ya Bwiru Sekondari, Shule ya Wasichana ya Bwiru Sekondari pamoja na Shule ya Sekondari ya Buswelu.