DKT. MWIGULU: VIZIMBA VYA SOKO LA MLANDIZI WAPEWE WAFANYABIASHARA

November 21, 2026






▪ Aonya viongozi kujigawia vizimba na kuwakodishia wafanyabiashara

▪ Aagiza ushuru wa awali uwe mdogo ili biashara ziweze kuimarika

▪ Ataka ujenzi wa soko la Sh. bilioni 7.71 ukamilike Desemba

WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba, ameitaka Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha kuhakikisha vizimba vya Soko la Kisasa la Mlandizi vinagawiwa moja kwa moja kwa wafanyabiashara watakaovitumia, badala ya viongozi kuvichukua na kuwakodishia kwa gharama kubwa.

Dkt. Mwigulu ametoa maelekezo hayo leo (Novemba 21, 2026), wakati akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye Viwanja vya Shule ya Msingi Mtongani, wilayani Kibaha, mkoani Pwani, baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa soko hilo.

“Vizimba hivi wapewe watu wanaofanya biashara wao wenyewe,” amesema Waziri Mkuu, akionya dhidi ya tabia ya baadhi ya viongozi kujigawia maeneo ya biashara katika masoko yanayojengwa na Serikali na kisha kuwakodishia wafanyabiashara.

Aidha, ameitaka Halmashauri kupanga ushuru mdogo kwa wafanyabiashara watakaohamia katika soko hilo, ili kuwapa nafasi ya kuimarisha biashara zao na kujenga wateja katika eneo jipya.

Amesema kuweka ushuru mkubwa tangu mwanzo kunaweza kuwaathiri wafanyabiashara wadogo na kuwafanya washindwe kuendesha shughuli zao kwa faida.

Waziri Mkuu pia amesisitiza ujenzi wa soko hilo ukamilike ndani ya mwezi mmoja, ili kuwezesha wafanyabiashara wanaofanya shughuli zao katika maeneo yatakayoathiriwa na ujenzi wa miundombinu ya barabara kupata sehemu mbadala ya biashara.

Amesema kukamilika kwa soko hilo ni muhimu katika maandalizi ya ujenzi wa barabara kubwa inayopangwa kupita Mlandizi, ambayo itahitaji baadhi ya maeneo yanayotumiwa sasa na wafanyabiashara.

Awali, wakati wa ukaguzi wa mradi huo, Dkt. Mwigulu alihoji usanifu wa vizimba 770 vya biashara vilivyojengwa kwa muundo unaofanana, akitaka kufahamu namna vitakavyokidhi mahitaji ya wafanyabiashara wa bidhaa mbalimbali.

Akitoa ufafanuzi, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha, Regina Lazaro Bieda, alisema usanifu huo umezingatia mahitaji ya wafanyabiashara wa soko la zamani, huku Halmashauri ikiwa na mpango wa kuongeza maeneo kwa biashara zinazohitaji nafasi kubwa zaidi.

Kwa mujibu wa taarifa ya utekelezaji wa mradi, ujenzi wa soko hilo wenye gharama ya Sh. bilioni 7.71 umefikia asilimia 93 na umepangwa kukamilika Desemba 31, 2026.

Soko hilo lina majengo manne yenye vizimba 770 vya biashara, maeneo 42 ya huduma za chakula, maduka 31, duka la dawa, eneo la supermaketi na mashine mbili za kutolea fedha (ATM).




Share this

Related Posts

Latest
Previous
Next Post »