KAMATI YA BUNGE YATAKA MABORESHO YA USIMAMIZI WA DAMPO LA PUGU

October 17, 2026
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira imeelekeza kuwepo kwa mpango madhubuti wa kudhibiti na kusimamia Dampo la Pugu Kinyamwezi, Dar es Salaam, ili kupunguza athari za kimazingira na kulinda afya za wananchi wanaoishi jirani na eneo hilo.

Maelekezo hayo yametolewa leo, Oktoba 17, 2026, na Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Prof. Pius Zebhe Yanda (Mb), wakati wa ziara ya kukagua hali ya mazingira katika Dampo la Pugu Kinyamwezi na Mto Ng’ombe, iliyolenga kutathmini utekelezaji wa maagizo yaliyotolewa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, Septemba 18, 2026.

Prof. Yanda amesisitiza umuhimu wa kutathmini afya za wananchi wanaoishi karibu na dampo hilo, pamoja na kuweka uzio utakaosaidia kudhibiti upanuzi wa makazi kuelekea eneo la dampo.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Mhe. Reuben Kwagilwa, amesema Serikali inapaswa kupata mwekezaji atakayeshughulikia uchakataji wa taka katika Dampo la Pugu ili kuboresha usimamizi wake na kupunguza athari za kimazingira kwa wananchi wanaozunguka eneo hilo.

Aidha, ameitaka Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kushirikiana kwa karibu na taasisi zote zinazohusika, ikiwemo Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), kuhakikisha mradi wa dampo hilo unatekelezwa bila kukwama.

Awali, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Albert Chalamila, akiwasilisha taarifa kuhusu hali ya mazingira mkoani humo, amesema Dar es Salaam ina eneo la takribani kilomita za mraba 1,300 na wakazi zaidi ya milioni 5.3 kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022.

Amesema ongezeko la watu na uzalishaji mkubwa wa taka kwa siku, pamoja na changamoto za miundombinu, vimechangia kiasi kidogo cha taka kufikishwa dampo, hali inayohitaji kuimarishwa kwa mifumo ya ukusanyaji, usafirishaji na uchakataji wa taka.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »