Na Mwandishi Wetu, Masasi
Msimu wa Korosho 2026/2027 umezinduliwa rasmi wilayani Masasi, Mkoa wa Mtwara, huku Emmanuel Shilatu, aliyemwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Masasi katika uzinduzi huo, akiwaonya viongozi wa Vyama vya Ushirika vya Msingi (AMCOS) kuepuka vitendo vya kuhujumu zao hilo na kuwataka kusimamia kwa uadilifu shughuli za msimu huo.
Shilatu ameyasema hayo wakati wa kikao cha uzinduzi wa msimu wa Korosho 2026/2027 kilichowakutanisha wadau mbalimbali wa zao hilo, wakiwemo viongozi wa vyama vya ushirika, wakulima na watendaji wanaohusika katika mchakato wa ununuzi na uuzaji wa korosho.
Amesema wakulima wa korosho wanathamini juhudi zinazofanywa na Serikali katika kuhakikisha zao hilo linaendelea kuwa na umuhimu kiuchumi, akiwataka wadau wote kushirikiana katika kulinda maslahi ya wakulima na kuhakikisha mchakato wa msimu huo unaendeshwa kwa uwazi na uadilifu.
“Wakulima wa korosho wanamshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa namna anavyoliheshimisha zao la korosho. Serikali haitamvumilia mtu yeyote atakayefanya mzaha au kujaribu kuhujumu kazi nzuri iliyofanywa na Rais Samia kwa kutaka kuhujumu zao la korosho kwa namna yoyote ile. Hatua kali zitachukuliwa dhidi yake, ikiwemo adhabu ya kufungwa,” amesema Shilatu.
Amesisitiza kuwa viongozi na watendaji wanaohusika na usimamizi wa zao hilo wanapaswa kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa, huku wakihakikisha wakulima wanapata haki zao kwa wakati.
Kwa upande wake, Mrajisi Msaidizi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Mtwara, Robert Nsunza, amewataka makarani wanaohusika katika mchakato wa ununuzi wa korosho kutumia mizani ya kidijitali, kuzingatia ubora wa zao na kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu.
Nsunza amesema matumizi sahihi ya mizani na uzingatiaji wa viwango vya ubora ni miongoni mwa mambo muhimu katika kuhakikisha wakulima wanapata haki zao na kuondoa malalamiko yanayoweza kujitokeza wakati wa mchakato wa ununuzi wa korosho.
Naye Kiongozi wa Chama Kikuu cha Ushirika cha MAMCU, Bi. Biadia Matipa, amesema chama hicho kimejipanga kikamilifu kwa ajili ya msimu wa Korosho 2026/2027 na kwamba maandalizi yote muhimu yamekamilika.
Matipa amesema watahakikisha wakulima wanalipwa fedha zao kwa wakati, akieleza kuwa lengo ni kuhakikisha malipo yanafanyika ndani ya siku saba tangu kufanyika kwa mnada wa korosho.
Amesema hatua hiyo inalenga kuwawezesha wakulima kupata fedha zao kwa wakati na kuendelea na shughuli zao za kiuchumi bila kuchelewa.
Kwa upande wao, viongozi wa AMCOS wameahidi kusimamia msimu huo kwa kuzingatia uadilifu, uwajibikaji na utendaji kazi wenye viwango, huku wakiahidi kushirikiana na wadau wengine kuhakikisha zao la korosho linanunuliwa na kuuzwa kwa kuzingatia sheria na taratibu zilizowekwa.
Msimu wa Korosho 2026/2027 unatarajiwa kuwa sehemu muhimu katika kuimarisha shughuli za kilimo na biashara ya korosho, huku wadau wakisisitiza umuhimu wa ushirikiano, uwazi na uadilifu katika kila hatua ya mchakato huo.




EmoticonEmoticon