Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Mhe. Subira Mgalu, ameipongeza Wizara ya Nishati kupitia Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwa hatua ya kuanza kutekeleza Mradi wa Ujenzi wa Njia ya Kusafirisha Umeme wa Msongo wa Kilovoti 220 kutoka Iganjo mkoani Mbeya hadi Saza mkoani Songwe, akisema mradi huo utakuwa na manufaa ya moja kwa moja kwa wananchi.
Mhe. Mgalu amesema hayo tarehe 11 Septemba 2026 katika eneo la Saza, Mkwajuni, Wilaya ya Songwe, Mkoa wa Songwe, wakati wa hafla ya utiaji saini mkataba wa utekelezaji wa mradi huo.
Amesema Kamati inaamini kukamilika kwa mradi huo kutachochea shughuli mbalimbali za kiuchumi na kijamii, ikiwemo uchimbaji wa madini, kilimo na biashara, sambamba na kuongeza fursa za ajira na kipato kwa wananchi katika maeneo yatakayonufaika na mradi huo.
Mhe. Mgalu amesema Kamati imeendelea kuhimiza utekelezaji wa miradi ya umeme inayolenga kuchochea shughuli za uzalishaji katika maeneo mbalimbali nchini, ikiwemo maeneo yenye shughuli za uchimbaji wa madini.
Ameeleza kuwa Kamati iliielekeza Wizara kuhakikisha umeme wa uhakika unafikishwa katika maeneo ya wachimbaji wa madini ili kupunguza gharama za uzalishaji na kuongeza ufanisi katika shughuli zao, jambo ambalo Wizara ya Nishati imeendelea kulifanyia kazi.
Aidha, Mhe. Mgalu ameishauri Wizara kuangalia uwezekano wa kufikisha umeme wa uhakika mapema katika mkoa huo kupitia miradi mbalimbali wakati wananchi wakiendelea kusubiri Mradi wa Iganjo–Saza unaotarajiwa kutekelezwa kwa kipindi cha miezi 18.
Kuhusu ushauri huo, Serikali tayari ilianza kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo kutekeleza mradi wa njia ya umeme ya msongo wa kilovoti 33 kutoka Mwakibete-Mbeya kuelekea Wilaya ya Songwe, ambao unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi huu.





EmoticonEmoticon