WIZARA , TAASISI ZATAKIWA KUCHUKUA HATUA KUKABILIANA NA MVUA ZA EL NIÑO

September 11, 2026

 




OWM –TAMISEMI, Dar es Salaam

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi leo Septemba 11, 2026 amezitaka Wizara, Mamlaka na Taasisi zinazohusika na majanga kuchukua hatua za haraka kujiandaa ili kuzuia na kupunguza athari zinazoweza kusababishwa na mvua za El Niño zinazotarajiwa kuanza mwezi Oktoba hadi Desemba 2026.

Makamu wa Rais ametoa maagizo hayo kwa taasisi hizo katika kikao kilichofanyika Ofisi ya Makamu wa Rais Jijini Dar es Salaam, ambapo kwa upande wa Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI yamepokelewa na Waziri Mhe. Prof. Riziki Shemdoe, mara baada ya ofisi yake na taasisi zinazohusika kuchukua hatua za haraka, kuwasilisha taarifa ya utayari na maandalizi ya Serikali katika kukabiliana na madhara ya mvua hizo, kufuatia tahadhari iliyotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania.

Katika kikao kazi hicho, Makamu wa Rais, Mhe. Ndejembi ameagiza wataalamu kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, Wizara ya Ujenzi pamoja na Taasisi zilizo chini ya Wizara hizo kuhakikisha zinafanya kampeni maalum ya usafi katika miundombinu ya barabara na mifereji ya maji.

“Ifanyike kampeni ya haraka, mikondo na mifereji ya maji izibuliwe, na barabara ziandaliwe,” amesisitiza Makamu wa Rais.

Aidha, Makamu wa Rais Mhe. Ndejembi, ameelekeza taka, tope na udongo unaotolewa baada ya kuzibua mitaro na mifereji katika maeneo mbalimbali kuondolewa mara moja na kutupwa katika maeneo yaliyotengwa, badala ya kuachwa kandokando ya barabara ambako taka, tope na udongo huo zinaweza kurejea kwenye mifereji wakati mvua zinapoanza.

Makamu wa Rais pia amezitaka Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, Wizara ya Ujenzi pamoja na Taasisi zilizo chini ya Wizara hizo, kufanya kazi kwa pamoja ya kujiandaa ili kuzuia na kupunguza athari zinazoweza kusababishwa na mvua za El Niño.

Akipokea maagizo hayo kwa ajili ya utekelezaji, Waziri wa Nchi, OWM – TAMISEMI Mhe. Prof. Riziki Shemdoe amemueleza Mhe. Makamu wa Rais kuwa ofisi yake imeshaanza kutekeleza maelekezo ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuboresha usafi wa mazingira katika majiji aliyoyatoa Septemba 02, 2026 wakati akiwaapishwa Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala aliowateua Agosti 27, 2026.

Prof. Shemdoe amemtaarifu Makamu wa Rais Mhe. Ndejembi kuwa, Septemba 07, 2026 alifanya kikao kazi na Wakuu wa Mikoa yenye majiji, viongozi wa majiji na manispaa za Mkoa wa Dar es Salaam na kuwataka kuhakikisha wanatekeleza kampeni maalum ya wiki mbili ya usafi wa mazingira katika majiji ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo ya Mheshimiwa Rais.

Akianisha namna ofisi yake itakavyotekeleza maelekezo ya Makamu wa Rais ya kujiandaa na kukabiliana na athari za mvua za El Niño, Prof. Shemdoe amewasilisha kwa Makamu wa Rais Mhe. Ndejembi, mkakati wa ofisi yake kupitia TARURA ulioandaliwa kwa ajili ya kujiaanda, kuzuia na kupambana na madhara ya uharibifu wa miundombinu ya barabara unaoweza kutokana na mvua za El Niño, ambao umeanisha namna utakavyotekelezwa.     


Share this

Related Posts

Previous
Next Post »