Na: OWM – TAMISEMI, Dodoma
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM-TAMISEMI), Mhe. Prof. Riziki Shemdoe, amesema zaidi ya wadau wa sekta ya afya 3000 kutoka nchi mbalimbali Duniani watashiriki katika Mkutano wa pili wa Kimataifa wa Huduma za Afya ya Msingi (IPHCC), jijini Arusha.
Prof. Shemdoe amesema hayo mapema leo Septemba 06, 2026 akiwa jijini Dodoma, kabla ya kuelekea Arusha na kuwakaribisha washiriki hao kwenye mkutano huo utakaofanyika kuanzia tarehe 9 hadi 11 Septemba, 2026 katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC).
Prof. Shemdoe amesema, yeye binafsi atashiriki katika mkutano huo wenye tija katika kuboresha utoaji wa huduma za afya msingi nchini na afrika kwa ujumla.
Prof. Shemdoe amesema mkutano huo umelenga kutoa uzoefu wa Tanzania katika uboreshaji wa huduma za afya ya msingi, ikiwamo afua zilizopelekea kupunguza vifo vya akina mama na watoto ambapo Tanzania kupitia jitihada za Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imekuwa ni kinara katika eneo hilo barani Afika.
Prof. Shemdoe amefafanua kuwa, mkutano huo umelenga pia kubadilishana uzoefu wa maboresho mbalimbali yanayoendelea kufanyika katika huduma za afya ya msingi duniani pamoja na kuandaa mikakati ya pamoja ya kuboresha huduma za afya ya msingi ili kufikia malengo ya kitaifa na Kimataifa, ikiwamo upatikanaji wa Huduma za Afya kwa wote na malengo endelevu ya maendeleo.
Mkutano huo wa kihistoria utawakutanisha washiriki zaidi ya 3000 kutoka Tanzania na mataifa mengine duniani wakiwamo; wataalam wa afya wanaofanya kazi ya kutoa huduma za afya ya msingi, watunga sera, wadau wa maendeleo, watafiti, wahadhiri, wanafunzi, asasi za kiraia na sekta binafsi, ambapo washiriki hao wamejisajiri kupitia tovuti ya https://iphcconference.tamisemi.go.tz .

EmoticonEmoticon