Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda
***
Tanzania imepata nafasi 150 za ufadhili wa masomo ya elimu ya juu nchini Algeria kwa mwaka 2026, zikilenga wanafunzi waliofanya vizuri zaidi katika masomo ya sayansi.
Akizungumza na waandishi wa habari Septemba 11 jijini Dar es Salaam, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda alisema kuwa Aljeria itagharamia ada za masomo huku Tanzania ikitoa fedha za kujikimu kupitia mpango wake wa Samia Scholarship.
Samia Scholarship imetajwa kuwa ni mpango maalum wa serikali uliowekwa kutoa ufadhili wa masomo ya elimu ya juu kwa wanafunzi waliofanya vizuri zaidi katika mitihani ya kidato cha Sita kwenye masomo ya sayansi, kwa lengo la kukuza wataalam wa ndani na kuongeza fursa za elimu bila kikwazo cha kipato.
Fursa hii adimu inalenga kuwanufaisha wanafunzi wenye uwezo kutoka familia zenye kipato cha chini, wakiwemo watoto wa wakulima na wafugaji, bila kujali uwezo wao wa kifedha.
Imeelezwa kuwa mpango huu unajumuisha pia wanafunzi 10 waliochaguliwa kwenda Moscow, Urusi, huku ukiongezeka kwa kiasi kikubwa kutoka nafasi 45 zilizotolewa na Algeria mwaka jana.
Akizungumza kufuatia taarifa ya Waziri kuhusu fursa hiyo ya elimu, Balozi wa Tanzania Nchini Algeria, Mobhare Matinyi, aliishukuru Algeria kwa kutoa nafasi nyingi mwaka huu 2026 kuliko miaka mingine na kuonesha matumaini kwamba mwakani zitaongezeka zaidi.
"Mwaka jana Algeria ilipokea wanafunzi wa Tanzania 45 lakini mwaka huu kutokana na mpango wa Samia Scholarships inayosimamiwa na Wizara ya Elimu wanakuja wanafunzi 150," alisema Balozi Matinyi.
Aidha, Balozi Matinyi aliongeza kuwa ubalozi kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia uliomba nafasi hizo ili nchi iweze kujipatia wataalam wa kutosha katika nyanja za sayansi na teknolojia zikiwemo sayansi za afya na TEHAMA.
Alisema, wanafunzi watakaoteuliwa watatakiwa kujifunza lugha ya Kifaransa inayotumika katika masomo nchini humo, huku majina yao yakitarajiwa kuwekwa rasmi kwenye tovuti ya wizara.
Serikali imewahakikishia wanafunzi hao kuwa itawaongoza katika hatua zote za kuwasilisha nyaraka na kuwakamilishia taratibu za safari, zikiwemo hati za kusafiria.
Hatua hii imetajwa kudhihirisha dhamira ya dhati ya serikali ya awamu ya sita katika kuimarisha ushirikiano wa kimataifa ili kukuza sekta ya elimu ya juu nchini.
Hata hivyo, utekelezaji wa mpango huu unatarajiwa kuongeza chachu ya ufaulu katika masomo ya sayansi na kuinua kiwango cha wataalam wa ndani kwa ajili ya maendeleo ya taifa.


EmoticonEmoticon