KILWA YATAKA UWEKEZAJI ZAIDI KATIKA NISHATI SAFI YA KUPIKIA

September 06, 2026




Kilwa, Lindi.


Katibu Tawala wa Wilaya ya Kilwa, Yusuph Mwinyi, amesisitiza umuhimu wa Serikali kuendelea kuwekeza katika nishati safi ya kupikia ili kuongeza upatikanaji wa nishati hiyo kwa wananchi na kuharakisha utekelezaji wa ajenda ya Taifa ya nishati safi ya kupikia.


Mwinyi alitoa kauli hiyo wakati wa ziara ya ujumbe wa Wizara ya Nishati uliotembelea mradi wa nishati safi ya kupikia unaotumia teknolojia ya haidrojeni ya kijani katika Wilaya ya Kilwa, mkoani Lindi.


Amesema uwekezaji katika nishati safi ya kupikia ni muhimu kutokana na nafasi ya nishati hiyo katika maisha ya kila siku ya wananchi, akieleza kuwa Serikali inapaswa kuendelea kuweka mazingira yatakayowezesha teknolojia mbalimbali za nishati safi kupatikana na kutumika kwa upana zaidi.


Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Nishati Safi ya Kupikia wa Wizara ya Nishati, Nolasco Mlay, amesema Serikali inaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuendeleza teknolojia za nishati safi ya kupikia, ikiwemo teknolojia bunifu kama haidrojeni ya kijani, ili kuongeza wigo wa chaguo la nishati kwa wananchi.


Mlay amesema kuendelezwa kwa teknolojia hizo ni sehemu ya jitihada za Serikali za kuhakikisha wananchi wanapata nishati safi ya kupikia inayokidhi mahitaji yao, huku akisisitiza umuhimu wa ubunifu, uwekezaji na ushiriki wa sekta binafsi katika kufanikisha azma hiyo.


Amesema teknolojia ya haidrojeni ya kijani inaonesha fursa katika safari ya Taifa ya kuelekea kwenye matumizi ya nishati safi ya kupikia, hivyo ni muhimu kuendelea kufanya tathmini na kutoa elimu kwa jamii kuhusu matumizi yake salama na yenye ufanisi.


Mlay amesisitiza kuwa ushirikiano kati ya Serikali, sekta binafsi, wataalamu na wananchi ni muhimu katika kuongeza kasi ya upatikanaji na matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini, sambamba na kufikia lengo la asilimia 80 ya Watanzania kutumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »