Tume ya Taifa ya UNESCO ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeshiriki katika zoezi la ukusanyaji wa maoni ya awali ya wadau kuhusu maandalizi ya Mpango wa Jumla wa Usimamizi (General Management Plan – GMP) wa Hifadhi Hai na Mwanadamu ya Rufiji–Mafia–Kibiti–Kilwa (RUMAKI), ikiwa ni hatua muhimu katika kuweka msingi wa usimamizi endelevu na shirikishi wa eneo hilo.
Zoezi hilo limejikita katika kupata maoni, uzoefu na mapendekezo ya wadau kuhusu namna bora ya kuimarisha uhifadhi wa mazingira na bioanuai, matumizi endelevu ya rasilimali za asili pamoja na maendeleo ya jamii zinazozunguka na kutegemea rasilimali za RUMAKI.
RUMAKI, inayojumuisha Rufiji, Mafia, Kibiti na Kilwa, ni miongoni mwa Hifadhi Hai zilizotambuliwa na UNESCO na kuingizwa katika Mtandao wa Dunia wa Hifadhi Hai (World Network of Biosphere Reserves – WNBR) mwaka 2023, chini ya Mpango wa UNESCO wa Mwanadamu na Hifadhi Hai (Man and the Biosphere Programme – MAB).
Hifadhi hiyo ina mifumo mbalimbali muhimu ya ikolojia ya pwani na bahari, ikiwemo misitu ya mikoko, miamba ya matumbawe na nyasi bahari. Mifumo hiyo ina mchango mkubwa katika kuhifadhi bioanuai, kulinda mazingira ya pwani, kusaidia shughuli za kiuchumi za jamii na kuongeza uwezo wa kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Maoni ya wadau yaweka msingi wa mpango
Ukusanyaji wa maoni ya awali ni sehemu muhimu ya mchakato wa kuandaa Mpango wa Jumla wa Usimamizi wa RUMAKI. Kupitia mchakato huo, wadau wanapata nafasi ya kueleza hali halisi ya eneo, changamoto zinazokabili uhifadhi na matumizi ya rasilimali, pamoja na fursa zinazoweza kuendelezwa kwa manufaa ya jamii na mazingira.
Miongoni mwa wadau wanaohusishwa katika mchakato huo ni viongozi wa Serikali za Mitaa na vijiji, taasisi za Serikali, jamii zinazozunguka Hifadhi Hai, wavuvi, Vitengo vya Usimamizi wa Fukwe (Beach Management Units – BMUs), taasisi za utafiti, wataalamu na wadau wengine wa maendeleo.
Ushirikishwaji wa wadau katika hatua hii unalenga kuhakikisha kuwa mpango utakaotengenezwa unazingatia mahitaji ya uhifadhi pamoja na hali halisi ya maisha ya jamii zinazotegemea rasilimali za eneo hilo.
Kuunganisha uhifadhi na maendeleo ya jamii
Dhana ya Hifadhi Hai na Mwanadamu inalenga kuweka uwiano kati ya uhifadhi wa bioanuai na maendeleo ya jamii. Kwa mtazamo huo, uhifadhi wa RUMAKI unahitaji kwenda sambamba na matumizi endelevu ya rasilimali zinazosaidia maisha ya wananchi, huku ukihakikisha kuwa rasilimali hizo zinalindwa kwa ajili ya vizazi vijavyo.
Katika maandalizi ya Mpango wa Jumla wa Usimamizi, suala la mgawanyo wa maeneo ya Hifadhi Hai linatarajiwa kuwa miongoni mwa maeneo muhimu ya kuzingatiwa. Hii inahusisha maeneo ya msingi ya uhifadhi (Core Areas), maeneo yanayozunguka maeneo hayo (Buffer Zones) na maeneo ya mpito (Transition Areas), kwa kuzingatia malengo ya uhifadhi na maendeleo endelevu.
Mpangilio huo unalenga kuweka uelekeo unaoeleweka kuhusu shughuli zinazoweza kufanyika katika maeneo mbalimbali, namna ya kulinda maeneo yenye umuhimu mkubwa wa kiikolojia na jinsi ya kuwezesha shughuli za maendeleo zinazozingatia mazingira.
Nafasi ya Tume ya Taifa ya UNESCO
Ushiriki wa Tume ya Taifa ya UNESCO katika zoezi hili unaendana na nafasi yake katika kuratibu na kufuatilia utekelezaji wa programu na shughuli za UNESCO nchini Tanzania, kwa kushirikiana na taasisi za Serikali na wadau husika.
Kupitia Mpango wa UNESCO wa Mwanadamu na Hifadhi Hai (MAB), Hifadhi Hai hutumika kama maeneo ya kujifunza na kuonesha namna uhifadhi wa bioanuai, matumizi endelevu ya rasilimali, maendeleo ya jamii, utafiti, elimu na ufuatiliaji vinavyoweza kuunganishwa katika eneo moja.
Kwa upande wa Tanzania, utekelezaji wa dhana hiyo katika RUMAKI unahitaji ushirikiano wa karibu kati ya taasisi za Serikali, mamlaka za Serikali za Mitaa, jamii, wataalamu, taasisi za utafiti na wadau wengine wanaohusika na uhifadhi na maendeleo.
Hatua kuelekea usimamizi endelevu wa RUMAKI
Maoni yatakayokusanywa katika hatua hii yatatoa msingi wa kuendelea na mchakato wa kuandaa Mpango wa Jumla wa Usimamizi wa RUMAKI. Mpango huo unatarajiwa kusaidia kuweka mwelekeo wa pamoja katika uhifadhi wa bioanuai, matumizi endelevu ya rasilimali, maendeleo ya jamii, utafiti, elimu na ufuatiliaji wa mazingira.
Kwa kuwa RUMAKI inahusisha maeneo ya nchi kavu, pwani na bahari pamoja na jamii zinazotegemea rasilimali hizo, usimamizi wake unahitaji mtazamo unaounganisha mahitaji ya uhifadhi na maendeleo.
Ushiriki wa wadau katika hatua za awali, hivyo, ni muhimu katika kujenga uelewa wa pamoja na kuweka msingi wa mpango unaozingatia mazingira halisi ya RUMAKI.
Maandalizi ya Mpango wa Jumla wa Usimamizi wa Hifadhi Hai na Mwanadamu ya RUMAKI yanaashiria hatua muhimu katika kuimarisha utekelezaji wa dhana ya UNESCO ya Mwanadamu na Hifadhi Hai, kwa lengo la kuhakikisha kuwa uhifadhi wa mazingira na bioanuai unaenda sambamba na maendeleo endelevu na ustawi wa jamii.

EmoticonEmoticon