SERIKALI YAIMARISHA HATUA ZA KUDHIBITI BEI ZA MAFUTA

April 30, 2026



Serikali imeendelea kuchukua hatua madhubuti za kudhibiti mwenendo wa bei za mafuta nchini, ikiwa ni jitihada za kulinda uchumi wa wananchi na kuhakikisha upatikanaji wa mafuta unaendelea kuwa wa uhakika.

Hayo yameelezwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati anayeshughulikia Mafuta na Gesi, Dkt. James Mataragio, wakati wa kikao cha wadau wa sekta ya mafuta na taasisi za Serikali.

Amesema ni muhimu kwa taasisi zote zinazohusika kuonesha dhamira ya dhati katika utekelezaji wa mikakati ya Serikali ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Aidha, Dkt. Mataragio amesisitiza umuhimu wa uwazi, usahihi wa taarifa na utunzaji wa kumbukumbu sahihi katika utekelezaji wa mifumo ya udhibiti wa mafuta, akieleza kuwa nyaraka sahihi zitakuwa msingi wa mafanikio ya hatua hizo.

Amepongeza kampuni za mafuta (OMCs) kwa mchango wao mkubwa katika kuhakikisha upatikanaji wa mafuta unaendelea kuwa thabiti licha ya changamoto za soko la kimataifa.

“Tumeshuhudia ushirikiano mkubwa kutoka kwa wadau wa sekta ya mafuta, hasa katika kipindi hiki kigumu ambacho hakijawahi kujitokeza hapo awali. Mmeendelea kusimama pamoja na Serikali kuhakikisha mafuta yanapatikana wakati wote,” amesema Dkt Matagio

Kwa upande wake, Kamishna wa Petroli Wizara ya Nishati, Godluck Shirima, amepongeza ushirikiano wa OMCs, akibainisha kuwa licha ya mabadiliko makubwa ya bei za mafuta duniani na ongezeko la gharama za uagizaji, kampuni hizo zimeendelea kuonesha uwajibikaji na ushirikiano wa hali ya juu kwa Serikali. Amesema juhudi hizo zimechangia kudumisha upatikanaji wa mafuta nchini bila kuyumba kwa kiasi kikubwa.

Naye Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (PBPA), Erasto Simon, amesema Serikali itaendelea kushirikiana kwa karibu na wadau wa sekta hiyo kupitia mikutano ya mara kwa mara ili kujadili changamoto na kuweka mikakati madhubuti ya kuimarisha zaidi sekta ya mafuta nchini.

Kikao hicho kimehudhuriwa na wataalamu kutoka Wizara ya Nishati, PBPA, Bank Kuu ya Tanzania (BoT), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), pamoja na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), sambamba na wadau mbalimbali wa sekta ya mafuta.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »