MHE. SALOME ASHIRIKI MKUTANO WA 21 WA MAWAZIRI WA NISHATI AFRIKA MASHARIKI

April 30, 2026

 





Na Mwandishi Wetu, Cairo

Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Salome Makamba, ameiwakilisha Tanzania katika Mkutano wa 21 wa Baraza la Mawaziri wa Nishati wa Ukanda wa Mashariki mwa Afrika, uliofanyika Aprili 29, 2026 jijini Cairo, Misri, ukiwa na lengo la kuimarisha ushirikiano wa kikanda katika sekta ya umeme.

Katika mkutano huo wa nchi wanachama wa Umoja wa Nishati Mashariki mwa Afrika (EAPP), uamuzi muhimu umefikiwa wa kuichagua rasmi Jamhuri ya Kiarabu ya Misri kuwa mwenyeji wa kudumu wa kituo cha uendeshaji wa soko la umeme la pamoja kwa nchi wanachama.

Mkutano huo uliongozwa na Waziri wa Umeme na Nishati Jadidifu wa Misri, Mhe. Dkt. Mahmoud Esmat, ambaye pia ni mwenyekiti anayemaliza muda wake, uliwakutanisha Mawaziri wa Nishati kutoka nchi 13 wanachama kwa lengo la kukamilisha mfumo wa kiutawala na kiuendeshaji wa soko la umeme la pamoja na endelevu.

Mbali na kuichagua Misri, Baraza hilo pia limepitisha nyongeza ya muda wa miezi miwili kwa nchi wanachama kukamilisha mchakato wa kuridhia hati za makubaliano ya ushirikiano baina ya serikali na mashirika ya umeme.

Aidha, mkutano huo umeridhia Jamhuri ya Shirikisho la Kidemokrasi ya Ethiopia kuchukua nafasi ya uenyekiti wa Baraza la Mawaziri, kufuatia kumalizika kwa muda wa uongozi wa sasa, kwa mujibu wa katiba ya umoja huo inayotaka uongozi kuzunguka kwa wanachama kila mwaka.

Akihitimisha mkutano huo, Mwenyekiti wa EAPP, Mhe. Dkt. Esmat, amesisitiza umuhimu wa kuendeleza umoja, ushirikiano, uwazi na kuheshimiana miongoni mwa nchi wanachama ili kufikia malengo ya kuwa na soko la umeme la kikanda lenye tija.

Akizungumza kuhusu mkutano, Mhe. Salome amesema maazimio yaliyofikiwa ni hatua muhimu katika kuleta mageuzi makubwa katika biashara ya umeme na kuimarisha soko la nishati la pamoja kwa nchi za ukanda huo.

Katika mkutano huo, Mhe. Makamba ameambatana na Balozi wa Tanzania nchini Misri, Meja Jenerali Richard Makanzo, Kamishna Msaidizi wa Maendeleo ya Umeme kutoka Wizara ya Nishati, Mhandisi Styden Rwebangila, Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO anayeshughulikia uzalishaji umeme, Mhandisi Anthony Mbushi, pamoja na wataalamu kutoka Wizara ya Nishati, TANESCO na EWURA.
Shar

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »