TAEC YAZINDUA BARAZA JIPYA LA WAFANYAΚΑΖΙ, ΥΑΑΝΖΑ SAFARI MPYA YA UWAJIBIKAJI

January 09, 2026


Na Mwandishi Wetu, Dodoma


Tume ya Nguvu za Atomu Tanzania (TAEC) imezindua rasmi Baraza Jipya la Wafanyakazi katika makao makuu yake yaliyopo Kikombo, Wilaya ya Chamwino jijini Dodoma, ikiwa ni hatua muhimu ya kuimarisha uwajibikaji, ushirikiano na ufanisi wa kiutendaji ndani ya taasisi hiyo.

Uzinduzi huo umefanyika wakati wa kikao cha 15 cha Baraza la Wafanyakazi, kilichohudhuriwa na wajumbe 32, na kufunguliwa rasmi na Mkurugenzi Mkuu wa TAEC, Profesa Najat Kassim Mohammed.

VIONGOZI WAPYA WACHAGULIWA

Katika kikao hicho, wajumbe wa baraza walifanya uchaguzi wa viongozi mbalimbali, akiwemo Katibu wa Baraza, Msaidizi wa Katibu pamoja na wawakilishi kutoka vitengo na kurugenzi tofauti za taasisi. Uchaguzi huo umeweka msingi madhubuti wa ushirikiano, uwazi na uwajibikaji katika utekelezaji wa majukumu ya TAEC.

AJENDA KUU: BAJETI NA MPANGO KAZI

Baraza hilo jipya lilijadili na kuweka mezani Mpango Kazi wa Mwaka wa Fedha 2026/2027 pamoja na Bajeti ya Muda wa Kati (MTEF), hatua inayoonesha dhamira ya TAEC kuanza mwaka mpya wa fedha kwa maandalizi thabiti, uwazi na mwelekeo ulio wazi wa kiutendaji.

USHIRIKI WA VIONGOZI WA KITAIFA

Kikao hicho pia kilihudhuriwa na viongozi wa kitaifa akiwemo Bi. Staile Kiko, Katibu wa RAAWU Kanda na Msimamizi wa Baraza kutoka Kanda ya Kati, pamoja na Bi. Honesta Ngolly, Kamishna wa Kazi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu.

Akizungumza katika kikao hicho, Bi. Ngolly alisisitiza wajibu wa wajumbe wa baraza kujiandaa ipasavyo kabla ya vikao, kushirikiana kwa karibu na Mwenyekiti katika maamuzi makubwa ya taasisi, na kuhakikisha maslahi ya wafanyakazi yanazingatiwa na kushughulikiwa kwa haki.

WITO WA MKURUGENZI MKUU

Akihitimisha kikao hicho, Profesa Najat Kassim Mohammed aliwataka wafanyakazi wa TAEC kuendelea kufanya kazi kwa mshikamano, kuheshimiana na kutekeleza majukumu yao kwa weledi na uwajibikaji mkubwa. Alisisitiza kuwa Baraza Jipya la Wafanyakazi ni chombo muhimu cha kuimarisha mshirikiano wa kijamii mahali pa kazi na kuongeza tija katika utekelezaji wa majukumu ya taasisi.

MATARAJIO YA SAFARI MPYA

Uzinduzi wa Baraza Jipya la Wafanyakazi wa TAEC unatarajiwa kuongeza uwajibikaji, mshikamano na ushiriki wa wafanyakazi katika masuala ya maendeleo ya taasisi, sambamba na utekelezaji wa dira na malengo ya TAEC kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027. Hatua hii imeelezwa kuwa mwanzo wa safari mpya ya kuimarisha utendaji kazi na ustawi wa wafanyakazi wa taasisi hiyo muhimu ya kitaifa.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »