Wadau mbalimbali wakipata Elimu katika banda la Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) wakati wa maonesho kwenye siku maalum ya Wataalamu wa Uhasibu (NBAA Career Day)
*****************
Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) leo imeshiriki katika maonyesho maalum yaliyoandaliwa na Bodi ya Taifa ya Uhasibu na Ukaguzi (NBAA) kwa ajili ya kuadhimisha Siku ya Wataalamu wa Uhasibu. Maonyesho hayo yamefanyika katika viwanja vya jengo la Mhasibu Posta, jijini Dar es Salaam.
Ushiriki wa TEA katika maonyesho hayo ni sehemu ya jitihada za Mamlaka katika kutangaza shughuli zake pamoja na kuimarisha uhusiano na wadau mbalimbali wa sekta ya elimu kutoka taasisi tofauti.
Kupitia maonyesho hayo, TEA ilitumia fursa hiyo kutoa elimu kwa umma kuhusu majukumu ya Mfuko wa Elimu wa Taifa unaosimamiwa na Mamlaka hiyo pamoja na mchango wa mfuko huo katika kusaidia jitihada za Serikali za kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia nchini.
Akizungumza wakati wa maonyesho hayo Afisa Mawasiliano wa TEA Bi. Eliafile Solla, aliwahimiza wadau wa elimu kushirikiana na Mfuko wa Elimu wa Taifa kwa kutoa michango mbalimbali itakayoongeza uwezo wa mfuko huo kufadhili miradi ya elimu katika maeneo mbalimbali nchini.
Bi. Solla alisema kuwa, lengo kuu la Mfuko wa Elimu wa Taifa unaosimamiwa na TEA ni kuhakikisha kila mtoto wa Kitanzania anapata elimu bora na kwa usawa bila kujali mazingira au hali ya kiuchumi anayotoka.
Kutokana na ushiriki wake mahususi na mchango wake katika maonyesho hayo, Bodi ya Taifa ya Uhasibu na Ukaguzi (NBAA) imeitunuku Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) cheti maalum cha shukrani na utambuzi.
Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) ni taasisi ya umma iliyo chini ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia inayosimamia Mfuko wa Elimu wa Taifa wenye lengo la kukusanya rasilimali fedha na vifaa kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya elimu, ikiwemo ujenzi wa madarasa, mabweni, maabara za Sayansi na nyumba za walimu, ili kuongeza upatikanaji wa elimu bora kwa usawa nchini.
Mdau akipatiwa elimu katika banda la Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) na Bi. Eliafile Solla wakati wa maonesho na kongamano maalum la Siku ya Wataalamu wa Uhasibu Jijini Dar es Salaam
Mdau wa sekta ya Elimu CPA Victorius Kamuntu akiongea na maafisa wa Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) alipotembelea banda la Mamlaka hiyo wakati wa maonesho na kongamano maalum la Siku ya Wataalamu wa Uhasibu Jijini Dar es Salaam.

Wadau na walaalamu wa Uhasibu wakifurahia picha ya pamoja na maafisa wa TEA walipotembelea banda la Mamlaka hiyo wakati wa maonesho na kongamano la Siku ya wataalamu wa Uhasibu Jijini Dar es Salaam
Afisa Uhusiano na Mawasiliano kutoka TEA Bi. Eliafile Solla akipokea cheti cha shukrani na Utambuzi katika maonesho na kongamano la Siku Maalum ya Wataalamu wa Uhasibu Jijini Dar es Salaam

Bi. Eliafile Solla, Afisa Uhusiano kutoka TEA akitoa Elimu kwa mdau aliyetembelea banda la Mamlaka hiyo wakati wa maonesho na maadhimisho ya Siku ya Wataalamu wa Uhasibu Jijini Dar es Salaam
Bi. Bestina Magutu, Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano kwa Umma kutoka Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) akitoa elimu kwa mdau aliyetembelea banda la TEA kwenye maonesho yaliyoandaliwa na Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi

Mdau akisaini kitabu cha wageni katika banda la Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA), wakati wa maonesho na kongamano maalum la Siku ya Wahasibu Jijini Dar es Salaam






EmoticonEmoticon