RAIS DKT.SAMIA APONGEZA TIMU YA UIMARISHAJI MPAKA WA TANZANIA NA KENYA.

December 16, 2025

 

Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe. Balozi Dkt. Batilda Burian akihutubia baada ya kuzindua rasmi kikao cha Kamati ya Pamoja ya Wataalamu ya Uimarishaji Mpaka wa Kimataifa kati ya Tanzania na Kenya leo 16/12/2025

Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe. Balozi Dkt. Batilda Burian na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Bi. Lucy Kabyemela wakisalimiana baada ya kuwasili katika kikao cha Kamati ya Pamoja ya Wataalamu ya Uimarishaji Mpaka wa Kimataifa kati ya Tanzania na Kenya kilichofanyika leo 16/12/2025
Kiongozi wa ujumbe wa wataalam kutoka Kenya Bi.Juster Nkoroi akielezea changamoto zinazojitokeza katika  kazi ya uimarishaji wa mipaka wa kimataifa zikiwemo mazingira hatarishi.
Kiongozi wa Timu ya Wataalam kutoka Tanzania Bwana Hamdouny Mansour akielezea jinsi kamati ilivyojipanga kutoa elimu kwa wananchi juu ya kulinda alama zinazojengwa.

Baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Pamoja ya Wataalamu ya Uimarishaji Mpaka wa Kimataifa kati ya Tanzania na Kenya wakifuatilia hotuba za viongozi.


Na Lusajo Mwakabuku-WANMM

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameipongeza Kamati ya Pamoja ya Wataalamu ya Uimarishaji Mpaka wa Kimataifa kati ya Tanzania na Kenya kwa kuhakikisha mpaka unaotenganisha nchi hizo mbili unaimarishwa ambapo hadi sasa kazi hiyo imeshakamilisha kwa asilimia 75.

Rais Samia ametoa pongezi hizo baada ya kupatiwa taarifa na Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe. Balozi Dkt. Batilda Burian kuhusu uwepo wa kikao  cha kamati ya pamoja  kinachojumuisha timu za wataalamu kutoka Tanzania na Kenya alipofika mkoani Mkoani Tanga tarehe 15/12/2025 na kuelezwa uwepo wa kikao hicho.

Akizindua rasmi kikao hicho cha siku tano kinachoendelea katika hoteli ya Tanga Beach Resort, Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe. Balozi Dkt. Batilda Burian amesema, Mhe. Rais ameridhishwa na taarifa za utekelezaji wa kazi hiyo na kuwataka wataalam kuitumia nafasi hiyo kufanya kazi kwa weledi.

"kazi ambayo marais wa  nchi hizi mbili walituma wataalam wakafanye ni muhimu katika kuimarisha uhusiano mzuri baina ya nchi hizi mbili kwani itaimarisha ushirikiano na undugu uliodumu kwa miaka mingi". Alinukuu maneno ya mhe Rais

Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa amesema kuwa,  Serikali ya Tanzania ipo tayari kutoa rasilimali zozote zitakazohitajika katika kuhakikisha kazi hii inafanyika kwa ukamilifu na ufanisi na kwamba uimarishaji mipaka ni ishara ya kuimarisha  ujirani mwema na udugu baina ya serikali mbili na wananchi sambamba na ushirikiano katika masuala mbalimbali kiwemo biashara, uwekezaji na diplomasia.

“Uwepo wa kikao hiki hapa Tanga ni matokeo ya ushirikiano mwema ambao unashuhudiwa na kazi kubwa iliyofanyika hadi sasa ikionesha ushirikiano mwema baina ya nyie wataalam. Naomba niwasihi tuendelee na moyo huu wa ushirikiano, tuendelee kuongozwa na mijadala na utayari wa kuhakikisha tunaimarisha mipaka yetu kwa amani na upendo kama nilivyoona hapa mlivyo” Aliongeza Balozi Batilda Burian.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Bi. Lucy Kabyemela wakati akitoa salamu za utangulizi kabla ya kumkaribisha Mkuu wa Mkoa, alisisitiza wataalam kuhakikisha wanachukua hatua sahihi juu ya mali za wananchi zilizopo katika pande zote mbili za mpaka kwa lengo la kuepusha migogoro na wananchi wakati wa utekelezaji wa kazi hii.

Kiongozi wa ujumbe wa wataalam kutoka Kenya Bi.Juster Nkoroi amesema kazi kubwa imefanyika katika uimarishaji wa mipaka wa kimataifa pamoja na uwepo mazingira hatarishi yenye wanyama wakali na milima pamoja na misitu yenye miba na vichaka ambapo ameweka wazi kuwa,  wataalam wanakutana changamoto hizo lakini bado wametekeleza kazi hii kwa ari kubwa na kuzitaka serikali kuwatia moyo zaidi kwa kile kinachofanyika.

Kiongozi wa Timu ya Wataalam kutoka Tanzania Bwana Hamdouny Mansour amesema, pamoja na mafanikio yote yaliyopatikana, kumekuwa na matukio kadhaa ya kuharibiwa kwa nguzo hizi hususan maeneo ambayo shughuli za kibinadamu zinatekelezwa.

Hata hivyo, amesema katika kukabiliana na hilo, timu ya wataalam ikishirikiana na viongozi wa vijiji husika wamekuwa wakitoa elimu kwa wananchi katika kuhakikisha miundombinu inayojengwa inalindwa na wanachi wenyewe.

Tanzania na Kenya zinaendelea na zoezi la uimarisha mpaka wa kimataifa baina ya nchi hizo kwa  kuboresha alama zilizofutika na kujenge nguzo zinazoonekana zaidi.

Hadi hivi sasa kwa upande wa mpaka wa nchi kavu, zaidi ya kilometa 564 kati ya 753 km zimeimarishwa tayari, na Tanzania imetekeleza kazi yake kwa wastani wa karibu 75 % katika awamu ya kwanza hadi tano (Ufukwe wa Ziwa Victoria hadi ndani ya hifadhi ya Mkomazi) ya mradi huu lengo likiwa ni kuweka mipaka wazi zaidi kwa usalama, usimamizi wa ardhi na kuondoa changamoto kwa wenye shughuli za mpaka.

=====MWISHO=========

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »