
Na Mwandishi Wetu, Manyara
Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Mhe. Queen Sendiga, amekabidhi pikipiki ya umeme ya magurudumu matatu iliyotolewa na Mati Foundation kwa binti mwenye ulemavu, Bertina Francis, aliyepoteza wazazi wake wote wawili kufuatia maporomoko ya tope yaliyotokea Wilaya ya Hanang’ mwezi Desemba 2023.
Bertina Francis, ambaye kwa sasa anaishi katika moja ya nyumba zilizojengwa na Serikali kwa ajili ya waathirika wa maporomoko hayo katika eneo la Waret wilayani Hanang’, ameelezwa kuwa anajishughulisha na biashara ndogo ya uuzaji wa vitafunwa. Kupatikana kwa pikipiki hiyo ya umeme kunatarajiwa kumrahisishia shughuli zake za kiuchumi hususan katika usambazaji wa bidhaa zake na hivyo kuongeza kipato na kujitegemea.
Akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano, Mhe. Sendiga amesema msaada huo ni matokeo ya ushirikiano mzuri uliopo kati ya Serikali na sekta binafsi, akisisitiza kuwa ushirikiano huo una mchango mkubwa katika kugusa maisha ya wananchi wenye uhitaji. Amempongeza mwekezaji David Mulokozi kupitia taasisi yake ya Mati Foundation kwa moyo wa kujitolea na kusaidia makundi maalum katika jamii.
“Serikali inaendelea kuhamasisha wawekezaji na taasisi binafsi kushiriki katika maendeleo ya jamii. Msaada huu ni mfano mzuri wa namna sekta binafsi inavyoweza kushirikiana na Serikali kuwainua wananchi walioko katika mazingira magumu,” amesema RC Sendiga.
Kwa upande wake, Bertina Francis ameishukuru Serikali pamoja na Mati Foundation kwa msaada huo, akieleza kuwa pikipiki hiyo itamfungulia fursa zaidi za kiuchumi na kumpa matumaini mapya ya maisha. Ameiomba taasisi hiyo kuendelea kuwasaidia watu wenye uhitaji ili nao wajisikie kuwa sehemu ya jamii na kuchangia katika maendeleo yao binafsi na ya Taifa.
Pikipiki hiyo ya umeme ni sehemu ya mpango unaoendelea wa kampuni ya Mati Super Brands Ltd kupitia taasisi yake ya Mati Foundation wa kugawa pikipiki za magurudumu matatu kwa watu wenye ulemavu zaidi ya 2,000 kote nchini. Mpango huo ulianza rasmi mwezi Septemba 2025 ukiwa na lengo la kuwawezesha watu wenye ulemavu kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi na kijamii.
Hatua hiyo imeelezwa kuwa ni mchango muhimu katika juhudi za Serikali za kuhakikisha makundi maalum yanapata fursa sawa za maendeleo na kujitegemea kiuchumi, hususan kwa waathirika wa majanga mbalimbali nchini.



EmoticonEmoticon